Mtikila kuandamana kupinga mahakama ya kadhi
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ametangaza kuandaa maandamano nchini nzima kupinga uundwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini. Mbali na kuandaa maandamano hayo, Mchungaji Mtikila ametishia kukiburuza mahakamani kituo cha Redio Quraan cha jijijini Dar es Salaam na kuhakikisha kuwa kinafungwa baada ya kutishia kumuua kwa kumkata kichwa. Kauli hiyo ya Bw. Mtikila imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kutoa msimamo wa serikali juu ya uundwaji wa mahakama hiyo hapa nchini kwamba suala hilo halijafikishwa serikalini rasmi. Mahakama ya Kadhi inashughulia masuala ya kutatua migogoro kama ndoa na mirathi kwa Waislamu. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Bw. Mtikila alidai kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu inaashiria kuwa serikali inataka kuingilia kazi ya mahakama na kusema wataandamana ili kushinikiza isianzishwe. `Tumepanga kufanya maandamano nchi nzima kupinga suala hili maana ninaamini kabisa kuwa, kuna Watanzania ambao hawana dini na wanaohitaji ulinzi na utetezi wa sheria ambayo haifungwi na dini yoyote,` alisema. Hata hivyo hakueleza siku ya maandamano hayo wala mkoa yatakapoanzia. Aliendelea kusema kuwa waziri Mkuu anapaswa kuwaomba radhi wananchi waliomweka madarakani kwa kukiuka katiba ya nchi inayokataza utetezi wa kikundi kimoja cha dini. Aliongeza kuwa, ibara ya 20 ya katiba kifungu cha 2(a) na kifungu kidogo (i) inaeleza na kukataza suala hilo. Kuhusu kuishitaki na kuifunga Redio Quraan, Mwenyekiti wa DP alisema ataifungulia kesi ya kuchochea vurugu na kuhatarisha maisha yake katika vipindi inavyorusha hewani. `Jumamosi radio hiyo ilisema ninastahili kukatwa kichwa na maneno hayo nimeyasikia na kuyarekodi? hivyo nitaifikisha mbele ya sheria,` alidai. Mwanasiasa huyo hodari wa kufungua kesi, pia alipinga kauli ya Papa kuisifu Tanzania kwamba ina uvumilivu wa kidini. `Hatuna uvumilivu wowote ndiyo maana tunasikia makanisa yamechomwa moto na mikutano ya Injili kuvurugwa tena wakati mwingine polisi wamehusika,` alidai. Kwa mujibu wa Bw. Mtikila makanisa 16 yamechomwa moto na mikutano zaidi 36 ya Injili kuvamiwa na kuvurugwa bila hatua zozote za kisheria kuchukuliwa kwa wahusika. Wiki iliyopita Mchungaji Christopher Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu kupinga kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment