Monday, November 26, 2007

Imani ya Vitambaa yazua mhadala mkali

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkali wa kiimani jijini Dar es Salaam baina ya redio mbili maarufu zenye mwelekeo wa kipentekoste.Radio hizo ni Praise Power FM na WAPO Radio.

Suala lenyewe lilianza baada ya mchungaji mmoja kijana anayekuja juu hivi sasa mwenye kanisa lake katikati ya jiji la Dar alipoiponda imani ya kuombea watu kwa kutumia vitambaa akisema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kutumia hirizi kitu ambacho Biblia imekikataza.Akihubiri katika radio WAPO FM ,mchungaji huyo aliyeonekana kuungwa mkono na Askofu mmoja maarufu anayemiliki mojawapo ya Radio hizo pia alipinga vikali matumizi ya imani za sumaku na kuwanywesha watu mafuta.

Kwa upande mwingine Wahubiri mbalimbali wanaoonekana kumuunga mkono mchungaji mwingine maarufu jijini anayemiliki mojawapo ya radio hizo ambaye anadaiwa kutumia vitambaa kuendesha maombi huku baadhi ya watu mbali mbali wakikiri kupokea miujiza, uponyaji na mibaraka tele kupitia vitambaa hivyo wakishuhudia kupitia radio hiyo, walikuwa katika mjadala mkali wiki 2 zilizopita wakitoa ushahidi wa kimaandiko kuwa hata mtume Paulo aliviombea vitambaa na kuwapelekea wagonjwa wakaponywa.

Hali hiyo imeleta mgawanyiko miongoni mwa waamini huku tume maalume iliyoundwa na umoja wa makanisa ya kipentekoste nchini (PCT) ikiwa inasubiriwa kwa hamu kubwa kutoa ripoti yake kuhusu imani potofu zinazodaiwa kuwepo nchini tanzania hususani jijini Dar es Salaam.
Kitu cha kujiuliza hapa ni nini majibu au matokeo ya maswali ambayo tume hiyo imejiuliza na kutazamiwa kuyatoa ifikapo mwezi wa 12 mwaka huu.


No comments: