Mchungaji Getrude Rwekatare leo asubuhi ameapishwa rasmi kuwa Mbunge wa CCM wa Viti Maalum, nafasi aliyopata baada ya kifo cha aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Salome Mbatia. Mama Rwakatare amewasili kwenye viwanja vya Bunge mishale ya saa 2:04 asubuhi kwa kutumia gari lake la kijani huku akiwa amevalia suti yake ya pinki, akisindikizwa na wapambe wake zaidi ya mia moja. Hata hivyo idadi kubwa ya wapambe hao wakiwemo akinamama waliovalia viremba vikubwa kichwani wamekomea nje ya uzio wa Bunge na Mchungaji Rwakatare akajitoma ndani akiwa na wapambe wanne tu. Miongoni mwa wapambe waliomsindikizwa Mama Rwakatare walikuwa wanaume kadhaa ambao pia wamevalia suti za sare. Baada ya kuwasili Mchungaji Rwakatare alichukuliwa na watumishi wa Bunge moja kwa moja mpaka ukumbini kwa ajili ya liheso ya shughuli ya kuapishwa. Saa 3:00 asubuhi, Bunge lilianza shughuli zake ambapo kwa mara ya kwanza Bunge limeanza kwa kuimba wimbo wa Taifa, kisha ikafuata dua ya kuliombea Bunge. Dua hiyo maalum kwa ajili ya Bunge ilifuatiwa na kiapo cha Mchungaji Rwakatare ambaye alitembea kwa mbwembwe kuelekea mbele ya ukumbi akisindikizwa na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji Profesa Juma Ngasongwa, Mbunge wa Peramiho Bi. Jenesta Mhagama na wabunge wengine wa CCM. Baada ya kula kiapo, Mheshimiwa Rwakatare alipeana mkono na na Spika wa Bunge Mheshimiwa Samwel Sitta, ambaye alimkabidhi papo hapo kitabu cha muongozo wa Bunge. Mchungaji Rwakatare alipotoka kwa Spika akaelekea kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Edward Lowassa kisha kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge) Bi. Batilda Burian kabla ya kuibua shangwe pale alipokata kona na kuelekea kwa wabunge wa kambi ya upinzani na kumpa mkono Mbunge wa Bariadi Mheshimiwa John Cheyo.
Alipotoka kwenye kambi ya upinzani, Mhe. Rwakatare akasindikizwa na wapambe wake mpaka kwenye kiti chake alichoandaliwa. Baada ya Mchungaji Rwakatare kuketi, Spika aliwaomba wabunge wasimame kwa dakika moja kumwombea mbunge wa Kiteto Marehemu Benedict Lusurutia, na kisha bunge likaendelea na kazi zake.
SOURCE: Alasiri
SOURCE: Alasiri
No comments:
Post a Comment