Monday, March 8, 2010

Tanesco kupitisha umeme wenye msongo mkubwa Kanisani kwa Kakobe



BAADA ya waumini kulinda majengo ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) kwa takribani siku 77, mpambano na vyombo vya dola sasa umeiva baada ya serikali kuliruhusu Shirika la Umeme (Tanesco) kuendelea na mradi wa kupitisha nyaya za umeme wa msongo wa 132KV juu ya eneo hilo.

Katika siku hizo 77, waumini hao walikuwa wakikesha usiku na mchana kwa lengo la kuzuia wafanyakazi wa Tanesco kupitisha nyaya hizo juu ya kiwanja cha kanisa hilo lililo jirani na eneo la Mwenge wilayani Kinondoni baada ya mkuu wa FGBF, Askofu Zacharia Kakobe kupinga mradi huo na kutangaza eneo hilo kuwa la hatari kwa wafanyakazi wa shirika hilo la ugavi wa umeme.

Askofu Kakobe anadai kuwa mradi huo wa thamani ya Sh34 bilioni kutoka serikali ya Japan haufai kupitishwa juu ya eneo la kanisa hilo kwa kuwa ni hatari kwa afya za waumini wake na unaweza kuharibu mawasiliano ya ndani wakati wa ibada, ambazo alisema hurekodiwa wakati zikiendelea na pia kudai kuwa utavuruga mawimbi ya televisheni kwa kuwa kanisa hilo lina mpango wa kujenga studio ya runinga.

Askofu huyo alidai mradi huo ulipingwa na wakazi wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndio maana ukakwepeshwa hivyo anataka Tanesco pia ikwepeshe nyaya zinazotakiwa kupita juu ya kanisa lake lililo kando ya Barabara ya Sam Nujoma.

Lakini Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alisema kuwa serikali imejiridhisha kuwa mradi huo hautakuwa na athari za kimazingira na afya ya binadamu na hivyo kutupilia mbali ombi la Askofu Kakobe la kutaka nyaya hizo zipitishwe katikati ya Barabara ya Sam Nujoma.

Ngeleja, ambaye wizara yake ilifanya vikao kadhaa na uongozi wa FGBF, alisema eneo la katikati ya barabara hiyo haliwezi kutumika kwa ajili ya nyaya hizo kwa kuwa tayari lina nguzo za taa za barabarani na kuongeza kuwa eneo hilo la kati linakusudiwa kutumika kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kwa kasi.

Kuhusu madai ya mradi wa studio ya televisheni, Ngeleja alisema kuwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewathibitishia kuwa haijapokea maombi yoyote ya kuanzisha kituo cha televisheni kutoka katika kanisa hilo na hivyo kuzingatia suala hilo ni kufanya kazi kwa hisia.

"Hivyo inakuwa vigumu kwa serikali kubadili usanifu wa mradi kwa kuwa hatuna uhakika endapo maombi ya kujenga kituo cha TV na hatujui kama yatakapowasilishwa TCRA yatakidhi vigezo vya kiteknolojia na upatikanaji wa masafa vilivyowekwa na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria,"alisema Ngeleja.

"Hutuwezi kujadili mambo mazito ya nchi kwa hisia. Suala la TV hadi sasa ni ‘hypothetiacal case’ (ni suala la kufikirika) kwa sababu hata maombi yake hayajafikishwa TCRA. Nchi hii ni yetu wote, serikali haifanyi kazi kwa maslahi ya kanisa, dini wala dhehebu fulani... inafanya kazi kwa maslahi ya Watanzania.

"Kutokana na sababu hizo, serikali inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba mradi huo hautakuwa na athari mbaya kwa wananchi na mali zao. Hivyo serikali inaiagiza Tanesco kuendelea na utekelezaji wa mradi huu kama ulivyopangwa."

Alisema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania na wananchi wake, hususan wa Jiji la Dar es Salaam ambako alisema utakuwa mwarobaini wa tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme.

Askofu Kakobe hakupatikana jana kuzungumzia uamuzi huo, lakini aliripotiwa mwishoni mwa wiki akisema kuwa kanisa lake halitakubali kutekelezwa kwa mradi huo ambao alisema umefanywa na maofisa wa serikali ambao ni mafisadi.

Ripoti zinadai kuwa Askofu Kakobe alipingana na ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na kampuni ya Bureau For Industry Cooperation (Bico), ambayo ilieleza kuwa umbali kutoka njia ya umeme hadi katika chumba ambacho itajengwa studio ya TV ni mita 4.8.

Lakini kiongozi huyo wa kiroho alidai kwenye mkutano uliofanyika wizarani tofauti iliyopo ni mita 1.82 tu, hali iliyofanya uongozi wa wizara kuongozana naye hadi kwenye eneo hilo ambako ilibainika kuwa tofauti hiyo ni mita 4.83 kitu kilichomfanya Kakobe ahamie kwenye hoja ya kituo cha televisheni.

Iwapo Kakobe ataendelea kushikilia msimamo wake wa kuzuia mradi huo, hali inaweza kuwa mbaya wakati wafanyakazi wa Tanesco watakapoenda eneo hilo kuendelea na mradi huo ambao umekwama.

Waziri Ngeleja alisema jana kuwa kuchelewa kwa mradi huo kutasababisha kuongezeka kwa gharama za ujenzi, hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo kadhaa kuwa mbaya na uwezekano wa wafadhili kujitoa katika kusaidia miradi mikubwa kama hiyo.

"Hivi ni nani anayependa kuona tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme nchini linaendelea? Kimsingi hakuna, hivyo tunawaomba wananchi, kanisa la FGBF na waumini wake pamoja na Askofu Kakobe watoe ushirikiano ili mradi uweze kumalizika," alisema Ngeleja.

Alisema serikali inazitaka mamlaka zote zinazohusika kushirikiana na Tanesco kuhakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa manufaa na ustawi wa taifa.

Ngeleja alieleza kuwa Machi 6 aliitisha kikao na wadau wa mradi huo, ambao ni pamoja na Tanesco, TCRA, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Ewura, Manispaa ya Kinondoni, Bico, wakala wa barabara Tanzania (Tanroads) na Askofu Kakobe.

Alisema katika kikao hicho askofu huyo alipinga ripoti ya Bico ambayo ilipewa kazi ya kuchunguza kama kuna athari zozote zinazoweza kusababishwa na utekelezwaji wa mradi huo. Ripoti ya Bico ilionyesha kuwa hakuna athari.

Waziri alisema Askofu Kakobe aliendelea kusisitiza kuwa hana imani na ripoti ya Bico, jambo lililowalazimisha wajumbe wa kikao kuhamia eneo la mradi karibu na kanisa hilo Mwenge, ili kupima upya na kuthibitisha.

"Upimaji ulifanyika kwa pamoja na wadau wote na vipimo vilivyopatikana havikutofautiana na vile vya Bico na hatimaye Askofu Kakobe alikiri kuwa tatizo sio vipimo tena lakini akatuomba mradi upite katikati ya barabara," alisema Ngeleja.

Ngeleja alisema Askofu Kakobe hakuwa sahihi katika baadhi ya taarifa zake kwa kuandika vipimo ambavyo vilibainika katika ripoti ya Bico kuwa havikuwa sahihi kulinganisha na vile vilivyofanywa kwa pamoja na wadau.

"Mathalan kutoka katika njia ya umeme huo hadi katika chumba kinachotarajiwa kurusha matangazo ya TV, Kanisa lilisema ni mita 1.82, Bico akasema ni mita 4.80 lakini tulipopima kwa pamoja na wadau tulipata mita 4.83,"alisema Ngeleja.

"Kutoka njia kuu ya umeme huo hadi katika lango nambari moja la kanisa; kanisa lilisema ni mita 0.0, Bico ikasema mita 2.8, lakini tulipopima kwa pamoja na wadau tulipata mita 2.8 na kutoka katika njia ya umeme hadi lango nambari mbili, Kanisa lilisema ni sentimita 24, Bico mita 2.8 na vipimo vya pamoja tulipata mita 2.9," aliongeza Ngeleja.

Ngeleja alifafanua kuwa katika vipimo vya kutoka chumba maalumu cha wageni (VIP) hadi katika njia ya umeme, Kanisa lilisema ni sentimita 40, Bico mita 2.9 na vipimo vya pamoja na wadau vilionyesha ni mita 2.8.

Ngeleja pia alisema hawakuweza kupitisha umeme huo chini ya ardhi kwa sababu fedha hizo ni za ufadhili kutoka Shirika la Maendeleo la Japan (Jica) na kwamba tafiti zote za athari ya mazingira na za afya ya binadamu zilishafanywa na serikali kujiridhisha.

Alisema mtaalamu mshauri alipendekeza vizuizi vilivyowekwa nje ya kanisa hilo, ikiwa ni pamoja na mabango mawili makubwa yaliyo katika hifadhi ya barabara na miti, viondolewe ili, umbali unaokubalika upatikane.

Alisema Tanesco ihakikishe kwamba vitu vyote vipitishavyo umeme, vilivyojengwa chini au karibu ya njia hiyo, pamoja na mfumo wa umeme wa kanisa hilo uwekewe vizuia radi imara na kwamba hiyo ni kazi ya mwenye mali (kanisa).

"Hili ni jukumu la kanisa lenyewe kwa sababu ndio mwenye mali, ila mafundi wanapatikana Tanesco,"alisema Ngeleja.

Alisema Bico ilishauri kuwa Tanesco inatakiwa kutumia mbinu bora na za kisasa katika ujenzi wa mradi huo wa umeme wa msongo wa 132KV, ili kuepuka kona kali kwenye nyaya na hasa kuepuka kuunga nyaya sehemu yoyote kati ya nguzo nambari 18 na 19 ambazo zitakuwa karibu na eneo la kanisa.

Zaidi ya Sh25 milioni zimepotea kutokana na kukwama kwa mradi huo kwa siku 77.

Source: mwananchi na vyombo mbalimbali vya habari

No comments: