Aibuka na kujiita Mtume!
Mtu anayejiita Mtume, ameibuka mjini hapa na kuwahamasisha wafanyabiashara na wafanyakazi kuchukua fedha zote kweye akaunti zao na kuzitoa sadaka.
Mtu huyo, Damas Mukasa, amekuwa akisema iwapo wafanyabiashara na wafanyakazi watachukua fedha zao zote na kuzifunga akaunti, watabarikiwa zaidi na kufunguliwa milango na baraka za mbinguni.
Alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki wakati akihubiri kwenye Kongamano la Mitume na Manabii mjini hapa. Alisema kitendo cha watu kujilimbikizia mali, ni kuukaribisha umaskini.
Aliwataka matajiri wawe na ujasiri wa kufunga akaunti zao au kutoa sadaka na mali zao zenye thamani kwa Mungu. Alielekeza mali hizo zitolewe kwenye makongamano yanayoandaliwa na Mitume hao ili watoaji waweze kuombewa na kubarikiwa.
Alisema ili mtu awe tajiri na kushiriki vyema mema, ni lazima kumtanguliza Mungu kwa mali zake alizonazo kwa kuzitoa kwa watumishi wa Mungu aliowaita ni mitume na manabii.
Aliwahamasisha wenye viwanja kuviuza na chochote walichonacho kukitoa kwa Mungu.
Alisema wapo ambao wamejaza fedha kwenye akauti zao na kuwa wabahiri katika kumtolea Mungu mali zao, matokeo yake wanajikuta wakiandamwa na mikosi mbalimbali ambayo inawafanya kuwa maskini.
Baada ya hapo, mtu huyo akiwa na wenzake watano, alitenga makundi matatu ya wafanyakazi, wafanya biashara na wanafunzi akiwataka wote walio tayari kufunga akaunti zao benki kutoka mbele ili waombewe.
Wafanyabiashara na wafanyakazi takriban 12, walijitokeza mbele na kuahidi kufunga akaunti zao kwa lengo la kumtolea Mungu mali zao.
Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwa katika mahubiri yake, walimpinga wakidai ni utapeli wa kutumia jina la Mungu ili kujinufaisha.
``Hakuna mafundisho ya Mungu katika Biblia yanayotaka mtu awe maskini, anataka watu wafanye kazi ili wawe na maisha bora... sasa hawa jamaa tunawashangaa wanaposema mtu atoe fedha zake zote kwa Mungu ili abarikiwe,`` alihoji Bi. Aisha Baraka.
Askofu Msaidizi wa Kanisa la Pentekoste, aliyekataa kutaja jina na mahali anapotoa huduma , alisema utoaji wa fedha na kuwashawishi watu wafunge akaunti benki, siyo mafundisho ya Mungu.
Baadhi ya waandishi wa habari waliojiandaa katika mkutano huo kuwahoji Mitume hao juu ya mafundisho yao, walishindwa kutokana na kuwepo ulinzi mkali waliowekewa mitume hao.
Tukio hili limekuja siku chache baada ya Mchungaji mmoja kuibuka mkoani Mara na kuwataka waumini wake kuuza mali zao pamoja na wanafunzi kuacha kwenda shule ili wajiandae kumpokea Yesu atakayekuja mwezi ujao.
SOURCE: Nipashe
2 comments:
Kaka kazi tunayo, hawa jamaa wamedhamiria wanataka utajiri kwa nguvu kama Marekani, ndipo ninapofikiri kuwa wakristo walokole tukae chini na kungalia nafasi ya Roho matakatifu, Maranatha ebu nikuulize, unapotoa fUNGU LA KUMI UNAONGOZWA NA ROHO??
Mimi nadhan hapa kuna tatiz, Fungu la kumi lisingekuwepo kaka hawa watu wasingefungua makanisa kama uyoga!,mimi natoa lakini bado niko kwenye mawazo mazito sana!
kuna tatizo sehemu, tumewaachia huru hawa watu kufanya wanavyotaka, yangekuwepo magazeti kama ya Tanzania daima, mwanahalisi, ya kikristo wafichue maovu mengi tu.
MUKASA HUU NI UTAPELI, KWANNZA MNATAKIWA KUFANYA KAZI NYIE!!1 PAULO ALISHONA MAHEMA NYIE MNATUBIA NA KUTUKAMUA FDHA ZETU, NA BADO MMEBAGUA WATU KULINGANA NA FEDHA ZAO,
HII MAADA NA HAKA KASEHEMU PENGINE KAWE SERIOUS ZAIDI KUWAMULIKA HAWA WATU katika blog hii..............HII HAIKUBALIKI.nimekasirika sana, acha niiishie hapa nisije tenda dhambi.
Kwa kifupi huu ni utapeli na unapaswa kukomeshwa. Inasikitisha watu wa Mungu wanapotoshwa namna hii na wala hakukuwa na mwenye ujasiri wa kukemea uhalifu huo(au labda hilo halikuripotiwa na mwandishi wa habari hiyo)
Post a Comment