Amani, Upendo na Faraja atoayo Kristo vikae nawe milele.
Siku ya Jumamosi ya tarehe 5 mwezi wa nne 2008 ilikuwa ni siku ya kipekee kwa wana-Fellowship wote wa ICF (Institute of Accountancy Arusha Christian Fellowship) kwa matukio ya huduma.
Hii ni siku ambayo wana-Fellowship hao wanaozidi 70, ambao ni wanafunzi wanaosoma masoma mbalimbali yahuso uhasibu na computer wakiongozwa na viongozi wao wa Fellowship waliungana kwa pamoja na kuamua kwenda kufanya huduma kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya mkoa wa Arusha na mwandishi wa Sayuni aliambatana nao kwa ajili ya huduma na pia kukuletea habari hizi.
Kikundi hiki cha watumishi wa Kristo kiliondoka hapa chuoni saa saba mchana kwa magari maalumu na kwenda hadi hospitali. Baada ya kufika walijigawa makundi makundi kulingana na idadi ya wodi zilizopo hospitalini pale na baada ya maombi ya pamoja, kazi hiyo ya Injili ilianza kama Neema za Mungu zilivyokuwa. Malengo makuu yalikuwa kuwatia moyo wale waliovunjika moyo, kuwaombea uponyaji kutoka kwa Mungu ,kuwaeleze habari za Yesu na kuwaleta kwake na mwisho kuwasaidia kwa mahitaji ya mwili.
Mungu alionekana sana katika hili, watumishi hawa waliweza kutembelea wodi zote, kufanya huduma ya maombezi na kuwasaidia wagonjwa katika mahitaji yao ya mwili, ikiwa ni mali na fedha taslimu kwa wahitaji. Mungu atukuzwe sana kwa sababu idadi kubwa sana ya wagonjwa wakiwemo wenzetu waislamu waliamua kumpa Bwana Yesu maisha yao baada ya kusikia Neno, ingawa wapo waislamu wachache waliokataa kabisa.
Kwa kweli wagonjwa wote walishukuru sana kwa huduma hii, na waliwasihi watumishi hao kuwatembelea sana.
Na kwa kweli hali tuliyoikuta huko ni ya kusikitisha mno, walikuwepo watu waliovunjika moyo sana, na pia wapo watu, hasa wazee waliotelekezwa na watoto na ndugu zao na kuachwa wenyewe hospitalini, hawana pesa wala chakula, hawana pa kwenda, kwa kweli inatia huruma sana. Kutokana na hali hii, tunawahimiza wapendwa kila mahali walipo kutilia maanani sana huduma hii, sasa tunaelewa ni kwa nini Biblia imesema kuwa hii ndiyo dini safi. Hima wandugu, tusiishie tuu madhabahuni kuhubiri upendo ,tuwafikie na wasiofikika na tunawasihi muwaombee hata wale waliookoka ile wadumu hadi mwisho.
Kitendo hiki cha wanafunzi hawa hakika chafaa kuigwa na wote wamngojeao Kristo, Mungu awabariki sana wafanikiwe katika masomo yao yote.
No comments:
Post a Comment