SIKU moja baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe kuupinga Waraka wa Kanisa Katoliki na Mwongozo wa Waislamu, Kanisa Katoliki limemgeuzia kibao kiongozi huyo wa kiroho na kumweleza kuwa ni kigeugeu na anajikomba kwa watawala.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Mhashamu Evaristo Chengula, alisema endapo serikali inalipangia kanisa lake jambo gani la kuandikwa na kuhubiriwa, basi aendelee kufanya hivyo na si Kanisa Katoliki.
“Mambo ya dini hatuwezi kwenda kuiuliza serikali, lakini kama yeye anaomba kupangiwa mahubiri, afanye hivyo,” alisema Mhashamu Chengula.
Alisema Askofu Kakobe ana tabia ya kujipendekeza kwa watawala kiasi cha kushindwa kujua mahitaji ya wafuasi wake kiroho na kimwili.
Alisisitiza kuwa, kamwe Kanisa Katoliki haliwezi kupangiwa na serikali mambo ya kuhubiri na kuongeza kuwa, kama kanisa lake linafanyiwa hivyo, basi atekeleze hayo kanisani mwake.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Joseph Selasini alisema, Askofu Kakobe hana budi kutambua kuwa Kanisa Katoliki halijipendekezi kwa watawala, bali linazingatia maslahi ya umma.
“Kanisa halijipendekezi wala kutafuta Cheap Popularity (umaarufu kirahisi) kama Kakobe, hivyo kusema maaskofu wamekosa nidhamu, ni kuonyesha upeo mdogo wa kazi yake ya uaskofu anayoifanya,” alisema Selasini.
Alihoji: “Kakobe huyo anayesema nidhamu, aliwahi kuipigia kampeni TLP alipoona haikuingia madarakani, akahamia CCM, sasa anatapatapa, mara CCM mara TLP. Hiyo ndiyo nidhamu anayopaswa kuwa nayo mtu anayejiita Askofu Mkuu?”
Selasini alimtaka Askofu Kakobe kuachana na mambo hayo kwa sasa ili akomae kiimani kwanza kabla ya kufanya jaribio la kujilinganisha na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, ambaye ni Askofu Mkuu Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
“Kakobe asijilinganishe na Kardinali Pengo kwa kuwa uaskofu wao ni kama mlima na kichuguu, hivyo asitumie heshima wanayompa waandishi kumsikiliza kwa kuchanganya watu, maana uaskofu wake ni kigeugeu wa kutafuta maslahi ya kidunia,” alisema.
Naye mmoja wa waamini wa Askofu Kakobe ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema hakutegemea kuona kiongozi huyo wa kiroho akipinga msimamo wa viongozi wa dini kutochaguliwa mambo ya kuhubiri.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shura ya Maimamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema hata kama Rais Jakaya Kikwete ataliingilia suala hilo kama alivyoshauri Askofu Kakobe juzi, hakuna litakalosaidia kwa sasa.
Akizungumza kwa ufupi na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam mara baada ya kutoka msikitini, Sheikh Ponda alisema sababu ya kusema hivyo ni kwamba, waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki ndiyo umelenga kuwagawa Watanzania na si ule wa Waislamu.
Sheikh Ponda alimgeuzia kibao askofu huyo kwa kumtaka akausome vizuri mwongozo wa Shura ya Maimamu anayoiongoza, na endapo hatauelewa, basi arudi kwa Waislamu wamweleweshe.
Aliusifu mwongozo wa Waislamu kwa kusema kuwa ndiyo pekee unaofaa kwa mustakabali wa taifa na kwamba, tofauti na ule wa Wakatoliki, wa kwao waliuandaa wakiwa wamejiamini.
Nao baadhi ya viongozi wa makanisa ya uamsho wa kiroho jijini Dar es Salaam, wamemjia juu Askofu Kakobe kwa kuushambulia waraka wa Kanisa Katoliki na kumtuhumu kuwa, anatumiwa na mafisadi.
Wachungaji hao pia walishangazwa na hatua ya askofu huyo kumshambulia Kardinali Pengo, na kusema lengo la kiongozi huyo ni kutaka kulitangaza kanisa lake upya baada ya kubaini kuwa limepoteza mwelekeo.
Wakizungumza na gazeti hili, wachungaji hao walitetea kauli ya hivi karibuni ya Askofu Pengo, aliyoitoa mbele ya Rais Kikwete katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mwanza, Anthony Mayalla, na kusema kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki hakuwa na nia ya kumdhalilisha kiongozi huyo wa nchi.
“Tunavyoona sisi katika suala hili ni kwamba, Askofu Pengo hakuwa na nia ya kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete, bali alikuwa akitoa mawazo yake na kumweleza rais kilicho ndani ya moyo wake kulingana na maandiko ya Kitume,” alisema Mchungaji Huruma Choya wa Kanisa la Living God la Mwenge.
Mchungaji huyo alieleza kusikitishwa kwake na kauli hiyo aliyoiita isiyo na baraka za Mungu, ikitolewa na kiongozi huyo wa kanisa, anayeheshimika nchini na kubashiri mwisho wa kanisa lake umekaribia.
Mchungaji wa Kanisa la Glory Tample la Kimara lililopo jijini Dar es Salaam, Andrea Kwayu alisema kilichofanywa na Askofu Kakobe kuchukua hatua hiyo ni chuki dhidi ya Kanisa Katoliki na kwamba anatafuta huruma ya Ikulu kwa maslahi yake binafsi.
Aliongeza kuwa, mazingira ya sasa yanaonyesha wazi kuwa suala la ufisadi na kukosekana kwa uadilifu katika serikali ni matokeo ya kupatikana kwa viongozi wabovu ambao huchaguliwa katika uchaguzi unaoshirikisha wananchi walio wengi.
“Kimsingi Kakobe miaka yote amekuwa na chuki binafsi na Kanisa Katoliki, sasa ameamua kusema hovyo mambo ambayo ni kama analazimisha wananchi waanze kulichukia kanisa hilo,” alisema Mchungaji Kwayu.
Kwa mujibu wa Kwayu, jamii imeanza kutambua uongo na ukweli bila kujali jambo analosema kiongozi yeyote yule, ikiwa ni pamoja na wa dini, mwanasiasa ama msomi.
Mchungaji William Mwamalanga wa Kanisa la Pentekoste lenye makao yake makuu mkoani Mbeya, alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Kakobe kuungana na viongozi wa Shura ya Maimamu katika kuendeleza chuki dhidi ya kanisa hilo la Katoliki.
“Kama kiongozi wa kanisa, alipaswa kutoa msimamo au maoni yake kuhusu waraka wa kanisa na si kuonyesha chuki za wazi kwa Pengo, na kwa kweli ameamua kutumia vibaya sakata la waraka huu, na si kuchangia maoni,” alisema Mchungaji Mwamalanga.
Wakati huohuo, Shirika lisilo la Kiserikali la Peace Building and Human Development (PHD), limemtahadharisha Askofu Kakobe kuepuka njama za kutumiwa na mafisadi kwa lengo la kuupinga waraka wa Kanisa Katoliki.
Mkurugenzi wa PHD, Philoteus Lissanga alisema, amesikitikishwa kuona hata wananchi wakifuatilia maelezo yake, kwani kwa kufanya hivyo watu waovu katika jamii nao wanapata wafuasi wa kuwaunga mkono.
Source: www.freemedia.co.tz
No comments:
Post a Comment