ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amemhisi Rais Jakaya Kikwete, kuvunja ukimya na kuzima mijadala kuhusu nyaraka za kidini, inaoendelea nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana, Askofu Kakobe alisema nyaraka hizo zinaelekea kuwagawa watu na hatua zisipochukuliwa, zinaweza kusababisha vita ambavyo havitakwisha.
“Rais wetu ni mpole sana, mcheshi na ni mtu wa watu, hilo si tatizo kubwa kwake, lakini ukiwa na rais mpole sana ni tatizo, hata ukiwa mkali sana ni tatizo pia, namhisi hili aliingilie kati,” alisema Kakobe.
Kakobe alisema baadhi ya viongozi wa kisiasa, wamekuwa wakiogopa kukemea vitendo vinavyofanywa na viongozi wa dini kwa sababu tu wanawaogopa.
“Napenda kusema kuwa, viongozi wa kisiasa kunyamazia maovu yanayofanywa na viongozi wa dini kwa sababu tu kuwaogopa, kunaweza kuwaingiza watu wote kwenye uovu,” alionya Kakobe.
Mbali na hayo Kakobe amepinga vikali tamko la kiongozi mmoja wa kanisa aliyejibu hoja ya kiongozi mmoja wa kisiasa aliposema wanasiasa hawawezi kuwafundisha kazi maaskofu.
“Nichukue nafasi hii kukemea vikali tamko la kiongozi mmoja wa dini, ambaye alitamka rais akiwa jukwaani kwamba wanasiasa hawapaswi kutufundisha wachungaji. Alitamka maneno hayo kwa jeuri, kuonesha kabisa ana msimamo usioyumba na hataki kushauriwa,”alisema Kakobe.
“Kama tunasema maadili ya viongozi wa serikali yamemomonyoka wa kwanza kukemewa ni viongozi wa dini kwa sababu wao ndio chanzo kikubwa,” alisisitiza.
Pia Kakobe alimpongeza mwanasiasa mkongwe nchini Kingunge Ngombale Mwiru, kwa hatua yake ya kuupinga hadharani, waraka wa Kanisa Katoliki na kwamba kiongozi huyo, anaona mbali.
Alisema kwa huyo hiyo, mzee Kingunge amedhihirika kuwa hata watu wasio na dini, wanaweza kuongoza vizuri.
Source: Mwanachi
No comments:
Post a Comment