Siku chache baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Mzee Reginald Abraham Mengi kutupa kombora la shutuma za madai ya baadhi ya vigogo wa Jeshi la Polisi nchini kutaka kumbambika kesi ya madawa ya kulevya kijana wake wa kiume, mmoja wa waliotajwa amekuwa akishinda na Biblia.
Ilikuwa Alhamisi iliyopita, Septemba 14, 2010 ambayo ilikuwa Kumbukumu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwandishi wetu alifunga safari hadi kwenye ofisi za Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya Nchini na kumkuta mkuu wa kitengo hicho, Kamishna Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa ambaye ni miongoni mwa waliotajwa.
Kamishna Mwandamizi wa Polisi, Godfrey Nzowa.
Akiwa ndani ya ofisi yake, maeneo ya Kilwa road, jijini Dar, Nzowa alikutwa akisoma Kitabu kitakatifu cha Maandiko ya Kikristo ‘Biblia’ ambapo alidai kuna vifungu anavipitia.Bila kupoteza muda, mwandishi alimsalimia Kamishna huyo na kuanza kuongea naye.
Mwandishi : Shikamoo Kamanda Nzowa.
Nzowa: Marahaba.
Mwandishi: Mbona leo Sikukuu ya Kumbukumbu ya kifo cha Nyerere uko ofisini, kwa nini usipumzike?
Nzowa: Nimeona nimuenzi Mwalimu Nyerere kwa kufanya kazi kwani hata yeye alikuwa mchapa kazi. Pia leo nilipatana na baadhi ya wananchi waje kunipa taarifa juu ya maeneo sugu yanayopitisha dawa za kulevya.
Mwandishi: Mbona unasoma Biblia ofisini au mambo ni mazito kiasi cha kukufanya umkumbuke Mungu muda wote?
Nzowa: Hapana, siyo kutokana na taarifa hizo bali ni kawaida yangu kuwa na Biblia ofisini kwangu siku zote na imekuwa ikinisaidia sana kupambana na mambo magumu, pia hunisaidia kufanya kazi bila wasiwasi.
Aidha, Kamishna Nzowa alisema anapopata magumu amekuwa akisoma kutoka kwenye Biblia vifungu vya Zaburi ya 25:
“Eee, Bwana nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu nimekutumaini wewe nisiaibike…”
Afande Nzowa aliendelea kusema kuwa, vifungo hivyo amekuwa akivisoma kila siku ili kujiweka jirani zaidi na Mungu wake.
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Mzee Reginald Abraham Mengi.
“Kila siku nimekuwa nikisoma na siyo hicho tu, bali vipo vingine mfano, Zaburi ya 59, na Zaburi ya 23 inayosema, ‘Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu,” alisema Nzowa.Mwandishi: Ina maana hata asubuhi ukiamka inabidi upitie vifungu fulani vya Biblia?
Nzowa: Ndiyo na siyo asubuhi tu, bali hata usiku, mfano nikiamka nasoma Zaburi ya 3, nikilala napitia Zaburi ya 4.
Nzowa alisema matendo hayo yote anayafanya tangu utotoni kwani ndivyo alivyolelewa na imekuwa ikimsaidia.
Alipoulizwa alijisikiaje siku alipopokea tuhuma dhidi yake, Kamishna Nzowa alisema:
“Sikuwa na wasiwasi, najua Mungu ndiyo kiongozi na mlinzi wangu siku zote, naamini atayamaliza tu”.
Aidha, alisema hana la kusema kwa sasa kuhusu madai dhidi yake kwani tayari kuna Tume imeundwa kuchunguza.
Hata hivyo, mazungumzo kati ya mwandishi wetu na Afande Nzowa yalikatishwa na simu nyingi alizokuwa akipokea siku hiyo ambapo alizitolea ufafanuzi kwamba zinatoka kwa marafiki na ndugu mbalimbali.
Kwa upande mwingine gazeti hili lilipompigia simu Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Kanda Maalum ya Polisi Mkoa wa Dar es Salaam (ZCO), Charles Mkumbo ili azungumze kwa upande wake, alisema hana la kusema, anasuburi matokeo ya tume iliyoundwa na Serikali.
Wakati huo huo, baadhi ya askari wakiwemo Wakuu wa Polisi Wilaya (OCD) na Makamanda wa Mikoa, Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Saidi Mwema, kushughulikia na kuondoa ukiritimba uliopo ndani ya jeshi hilo baina ya maafande wa Usalama Barabarani (Trafiki) na wale wa kawaida.
Wakuu hao wa polisi waliliambia gazeti hili kwamba uongozi ndani ya jeshi hilo jijini Dar ni tofauti kabisa na mikoani kwani askari wa usalama barabarani hawawajibiki chini ya OCD wala RPC bali kwa mkubwa wao kama vile Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa (RTO).
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Saidi Mwema.
Aidha, walidai kwamba licha ya askari hao wa usalama barabarani kuwa na ofisi zao walayani na katika mikoa ya kipolisi jijini Dar es Salaam, wamekuwa na dharau kubwa sana kwa OCD na RPC kiasi kwamba hawawezi kuwauliza jambo lolote kikazi.“Mara nyingi wamekuwa wakituambia kwamba haturuhusiwi kuuliza kitu chochote kile kwa upande wa kesi inayohusiana na magari yanayokamatwa bali wamekuwa wakiwasiliana na wakubwa wao wa mikoa yaani RTO’S, hii hali siyo kabisa ndani ya jeshi letu,” alisema OCD mmoja ambaye hakuta jina lake liandikwe gazetini.
Viongozi hao walisema kwamba inapotokea ulinzi wa kitu chochote ndani ya magari yaliyokamatwa na askari wa usalama barabarani, OCD wa eneo husika huulizwa na wamemwomba IGP Mwema alishughulaikie suala hilo mapema ili kuondoa ukiritimba huo kwani ni hatari ndani ya jeshi hilo hasa kwa polisi waliopo wilayani na mikoani katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
IGP Mwema hakuweza kupatikana jana alipopigiwa simu yake ya kiganjani.
Source: www.globalpublisherstz.info
1 comment:
Thanks for sharing this link, but unfortunately it seems to be offline... Does anybody have a mirror or another source? Please reply to my message if you do!
I would appreciate if a staff member here at sayuni.blogspot.com could post it.
Thanks,
James
Post a Comment