Friday, October 29, 2010

Makanisa yakanusha kuwa na mgombea wao wa Urais

JUKWAA la Wakristo linalojumuisha Taasisi za Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Makanisa ya Pentekoste (PCT) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), wamekanusha uvumi kwamba wanahamasisha Wakristo kuchagua rais wa dini hiyo na kuuita uvumi huo kuwa ni
hujuma.

Pia jukwaa hilo limesema uvumi huo umesambazwa kutokana na anuani ya barua pepe ya Kanisa la PCT kuingiliwa na watu wasiojulikana na kuandika waraka wa kuhamasisha udini na kuliomba Jeshi la Polisi kufuatilia na kuwachukulia hatua wahusika iwapo watabainika.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa PCT, Askofu David Mwasota, alisema barua hiyo yenye uvumi huo ni ya uongo na hakuandikwa na kanisa lake na wala hawahuhusiki.

“PCT tumeingiliwa mawasiliano yetu … hii ni hujuma kubwa kwa jumuiya yetu na Wakristo kwa ujumla, tunalaani kitendo hiki na kuomba Polisi kulishughulikia suala hili mara moja ili kuepusha udini katika Taifa letu,” alisema.

Alisema waandishi wa barua hiyo walikuwa na mpango ambao umelenga kuwanufaisha wasiopenda amani hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na wenye nia ya kuwagawa Watanzania.

Alisema kwa umoja wa makanisa hayo, wanakanusha taarifa hizo ambazo ziliandikwa na magazeti mawili yanayotoka kila siku (si Habarileo) na kudai kuwa Wakristo wanaendesha kampeni za udini nchini.

“Nawaomba Wakristo wote nchini kwa pamoja na jamii ya Watanzania kuamini kuwa taarifa hizi ni za upotoshaji na haziwahusu na walioandika wana nia ya kuwagombanisha Wakristo na vyama vya siasa, serikali na dini nyingine,” alisema.

Aliwaomba wakristo wote kesho kutwa katika siku ya kupiga kura kujitokeza kwa wingi mara baada ya kufanya ibada na kuchagua kiongozi wanaoyeona anafaa.
Source:http://habarileo.co.tz

No comments: