Monday, October 25, 2010

Membe atetea serikali kwa maaskofu

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema CCM imegawanyika makundi mawili, moja likiwa ni lile la viongozi walioshindwa kuupata urais na lingine likiwa ni lile la Kikwete na serikali yake.

Alisema kundi lililoshindwa na Kikwete kupata urais ndilo limekuwa likisambaza ujumbe na taarifa za kumchafua Kikwete na serikali yake kuwa ameshindwa kuwashughulikia mafisadi na kuigeuza nchi hii kuwa ya kidini kwa kuteua viongozi wengi wa ngazi za juu nchini waislamu.

Membe alijikuta akieleza hayo wakati alipokuwa akijibu maswali ya viongozi wa dini na madhehebu ya kikristo kuhusu masuala mbalimbali aliyoyazungumzia kuhusu ufisadi, udini na serikali kujiunga na IOC .

Alisema kutokana na uvumi huo kuenezwa zaidi wakati huu wa kampeni ameanza ziara ya kupita mikoani nchini kuzungumza na viongozi wa dini kusafisha hali hiyo ya hewa.

Katika kikao hicho kilichofanyika Hoteli ya G and G jijini Mwanza juzi na kuhudhuriwa viongozi wa madhehebu ya kikristo zaidi ya 100, Membe alisema alikuwa na mambo manne ya kufafanua ambayo ni tuhuma za kuwepo kwa udini, ufisadi, suala la Tanzania kutaka kujiunga na OIC na pamoja na kuanzishwa ka mahakama ya Kadhi nchini.

“Wakristo wanaonekana kujitenga wakidai kuwa Kikwete kaonyesha mpasuko kwa kupendela waislamu katika serikali yake na kuwa ifikapo mwaka 2015 Tanzania itakuwa imejiunga na OIC na kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi na mengine yakidai kuwa ameshindwa kushuhgulikia ufisadi hapa nchini, mambo haya siyo kweli.” alisema

Ingawa Membe alikanusha Tanzania haijafikia uamuzi wa kujiunga na OIC aliwataka viongozi hao kukubaliana na suala hilo kwa vile zipo faida nyingi ambazo nchi itapata na kutaja mojawapo kuwa jumuiya hiyo inazo fedha nyingi hivyo itawasaidia kutatua matatizo waliyonayo.

Membe alizitaza baadhi ya nchi akidai kuwa zimenufaika na OIC na kusisitiza kuwa kujiunga nayo hakuna masharti ya kuigeuza nchi kuwa ya Kiislamu bali ni kuwa na idadi ya waislamu wasiopungua asilimia 60.

Alikaririwa akidai kuwa serikali haina udini na kwamba kuanzishwa kwa mahakama ya Kadhi hakutaibadili nchi kuwa ya kidini na kubainisha kwamba katika utawala wa Kikwete amekuwa akipambana na ufisadi kinyume na inavyoelezwa na watu.
Kutokana na maelezo hayo ya Membe, kilifika kipindi cha viongozi hao kueleza ya kwao ambapo mchungaji mmoja alianza kuzungumza kwa kutumia msemo wa Biblia kuwa kauli anayoitoa Membe kumsemea Kikwete wakati huu wa uchaguzi ni sawa na ‘Sauti iliayo nyikani’ na kutoboa kuwa Membe hakupaswa kuyaeleza yeye bali Kikwete.

“Hapa tunasikia sauti inalia nyikani, sasa hatumuoni mtu anayelia, wakristo tunataka kumsikia yeye mwenyewe na siyo kutuma mtu bali aseme yeye kwa kinywa chake hadharani kuwa Tanzania hakuna udini na nchi haitajiunga na OIC.” alisema mchungaji mmoja akimueleza Membe.


Kwa upande wa mafisadi mmoja wa viongozi hao wa dini walikaririwa akimuuliza iwapo ana dhamira ya kupambana na ufisadi ni kwa nini ameweza kusimama hadharani na kuwashika mkono akiwaombea kura baadhi ya watuhumiwa, ambao serikali yake imewafikisha mahakamani huku akitolewa mfano wa nchi ya Malawi ambako waziri mmoja amefilisiwa na kukamatwa kutokana na ufisadi.


Mmoja wa viongozi hao wa dini alimtahadharisha Membe kuwa anapaswa kutambua kuwa Watanzania wa sasa siyo sawa na wale wa zamani na kwamba sasa anapaswa kuwajibu vyema wapouuliza.
Walisema iwapo anasema faida ya kujiunga OIC ni kwa ajili ya kupata fedha za kusaidia taifa na kuhoji taifa limeshindwa vipi kunifaika na raslimali zake kama madini kiasi cha kuhitaji fedha za OIC.
“Membe alisema mambo yote ambayo ameyazungumzia na kwao yamezushwa wakati huu wa uchaguzi na kubainisha kuwa wanaozusha ni kundi la waliokosa uongozi ndani ya CCM.


Hata hivyo, nje ya hoteli hiyo Membe alipotakiwa na waandishi wa habari kuzungumzia kikao chake na viongozi wa dini, alikataa na kuwakimbia ambapo alijikuta akiliacha gari lake na kuingia gari la mkuu wa mkoa wa Mwanza ambaye alimkumbusha kuwa hilo halikuwa gari lake na kurudi kuingia gari lake na kuondoka.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa dini na Madhehebu ya Kikristo, Charles Sekelo ambaye ni Askofu wa Kanisa la CECT, alipoulizwa kuhusuna na kikao hicho alikiri kuzungumza kwa mambo hayo na kueleza kwamba Membe alidai alikuwa akimsafisha Kikwete kutokana na kuvuma kwa mambo machafu.


“Kwa maneno yake Membe alisema maduhumuni ya kikao chake nasi ilikuwa ni kusafisha juu ya mambo hayo, alidai yameuwapo mambo mengi mchafu ya kumchafua Kikwete na CCM, na kumbe alikuja kusafisha.” alieleza Askofu Sekelo.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Kanisa la Anglikana katika kikao hicho, Geoffrey Salum alisema, Membe alikuwa akijaribu kuwashawishi viongozi hao kujenga imani na serikali.
“Membe hajafanikiwa kutokana na msimamo wa viongozi wa dini ulivyokuwa ndani ya ukumbi huo, kwani ameshindwa kukidhi haja ya maswali yao na diyo maana wengi wamemweleza wazi kuwa wanataka Kikwete mwenyewe akiri hakuna udini nchini,” alieleza Salum.


Hata hivyo, Mchungaji David Emanuel wa Kanisa la Calvary Assemblies of God, alisema katika kikao hicho wametoa dukuduku lao na kueleza wazi kuwa hawaafikiani na serikali yake.


Source:mwananchi.co.tz

No comments: