Monday, December 3, 2007

Mchungaji Getrude Rwakatare awa Mbunge


MCHUNGAJI kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God Mikocheni B, Dar es Salaam, Dk. Gertrude Rwakatare, anatajwa kuwa ndiye anayetarajiwa kuirithi mikoba ya ubunge ya Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Joseph Mbatia, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Jumatano iliyopita, Njombe, mkoani Iringa.Mbatia aliyefariki dunia akiwa katika kampeni za kusaka kura za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alipata uwaziri kutokana na kuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).Kwa mujibu wa dodoso za kisiasa, Dk. Rwakatare mwenye umri wa miaka 55, ambaye pia ni mmiliki wa shule za St. Mary's, anapewa nafasi hiyo kutokana na mtiririko katika orodha ya wagombea wa Viti Maalumu vya ubunge kupitia chama tawala, CCM ambao majina yao yalipelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).Katika orodha hiyo iliyotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, jina la Dk. Rwakatare (CCM) linatajwa kuwa lilishika nafasi ya 61 kati ya majina ya wagombea wa Viti Maalumu vya wanawake yaliyopelekwa NEC kwa ajili ya kuthibitishwa kupenya hadi bungeni.Kwa mujibu wa NEC, CCM inawakilishwa bungeni na wabunge 58 wa viti maalumu vya wanawake. Kati ya wabunge hao, 42 wanawakilisha mikoa ya Tanzania Bara, kila mkoa ukiwakilishwa na wabunge wawili na wabunge 10 waliochaguliwa na chama kutokana na kushika nafasi ya tatu nyuma ya wabunge hao 42 kutoka mikoani.Lakini jina la Dk. Rwakatare na wengine kuanzia namba 60 kwenda juu, lilikatwa kutokana na kuwapo viti maalumu 58 vya wanawake vya kuiwakilisha CCM bungeni. UWT ilitoa upendeleo kwa kulipa kila kundi kiti kimoja isipokuwa UVCCM iliyopewa viti viwili.UVCCM ilipewa nyongeza ya kiti kimoja baada ya Baraza Kuu la umoja huo kutaka kupewa kiti kimoja zaidi, likipinga kuwa na mwakilishi mmoja tu katika chombo hicho cha kutunga sheria.Katika mkutano huo, wajumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, waliweka shinikizo kwamba endapo kiti hicho kisingeongezwa, basi hata ile nafasi moja ambayo walipewa wangeikataa.Katika mchakato wa kutafuta wawakilishi wa umoja huo, Lucy Mayenga, alishika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ilichukuliwa na Amina.Dk. Rwakatare hakupatikana kuzungumzia suala hilo, kwani kila alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, ilikuwa haipatikani.Naye, Dk. Ishengoma alipotafutwa kuzungumzia angalau mtu aliyemfuatia, alidai yuko mbali na Dar es Salaam na kwamba hafahamu lolote.Hata hivyo, kulingana na orodha, baada ya Dk. Ishengoma, Mkuu wa Mkoa wa Pwani aliyeirithi mikoba ya hayati Amina Chifupa, anayefuatia ni Dk. Rwakatare."Huyu yupo katika orodha ya waliopendekezwa na CCM, kama ilivyo kwa Dk. Ishengoma, si unakumbuka hata aliyemrithi Amina Chifupa hakutoka UVCCM? Wote hawa ni watu wa CCM, kwa hiyo inawezekana akarithi mtu kutoka katika orodha ya NEC, hasa anayemfuatia Dk. Ishengoma," kilieleza chanzo chetu cha habari.Dk. Ishengoma, baada ya kukabidhiwa mikoba ya Chifupa aliyefariki Juni 26, mwaka huu, aliapishwa Agosti 16, mwaka huu.Dk. Ishengoma, aliapishwa katika siku ya mwisho ya mkutano wa Bunge la Bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2007/2008.

No comments: