Tuesday, January 27, 2009

Jan 2009:KWAHERI NDUGU YETU SEDEKIA.


TUKIO LA JANUARY 2009:

KWAHERI NDUGU YETU SEDEKIA.


Jina la Bwana litukuzwe milele na milele, na tena atukuzwe Yeye ambaye anatuwazia mema kuliko yale sisi tuyawazayo.

Ndugu wana Sayuni popote pale mlipo, nadhani wote mnakumbuka msiba tulioupata wa kutwaliwa kwa ndugu yetu Fanuel Sedekia akiwa kule katika nchi ya baba zetu, Israel.

Mimi nilifuatilia tukio lile na kuhudhuria ibada ya kuuaga mwili wake hapa Arusha ila nilishindwa kuwaletea habari hizi kwa muda kutokana na kubanwa sana na mambo hapa, ila nimezileta leo ili tujikumbushe ikiwa ni tukio kubwa kabisa katika mwezi huu.

Kama wengi tulivyojua, ndugu yetu huyu alifariki akiwa katika safari muhimu sana ya kiroho kule Israel, akiwa pamoja na timu ya huduma ya MANA ya mwalimu Christopher Mwakasege.

Siku hiyo ya kuuga mwili wake na mazishi (January 10) tulikutana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid hapa Arusha, na watu walikuwa ni wengi kiasi ambacho hakikutegemewa. Mwili wake uliingizwa uwanjani, ukiwa umebebwa kwenye gari, na gari lingine lilikuwa likifuata nyumba yake likiwana speakers kubwa huku wakiwa wameweka ule wimbo wa “Bwana ametoa na Bwana ametwaa” aliouimba Sedekia mwenyewe. Hii ikiwa ni baada ya kuwasili jana yake kwa ndege kutokea Israel ambapo mamia ya wakazi wa Arusha walijipanga pembeni mwa barabara ya moshi-arusha huku wakiutazama msafara uliokuwa na mwili wake uliopata magari yasiyopungua 40, na wengine walikwenda hadi hospitali ya mkoa ya Arusha na walisikika wakipiga mayowe ya vilio walipoona jeneza lake. Mara baada ya kuingia uwanjani,ulipokelewa kwa utulivu na timu ya waimbaji wa muziki wa Injili kutoka Dar na maeneo mbalimbali kama unavyoweza kuona katika picha. Baada ya hapo, watu mbalimbali walipewe nafasi ya kuzungumza kwa ufupi namna walivyomfahamu Sedekia. Na hapa kwa ufupi natata nieleze kile alichosema Mwl. Mwakasege.
Mwalimu alielezea namna walivyoondoka na Sedekia hapa uwanja wa ndege wa Arusha, ya kuwa alikuwa amemaliza kutumia doze ya malaria iliyomsumbua muda kidogo na kuwa alisema alikuwa ok kwa safari. Waliondoka hadi Israel walipoanza kutembelea maeneo muhimu ya kibiblia huko, na baada ya siku chache, Sedekia alionekana kuwa mdhaifu na alisema hali yake si nzuri sana. Baadaye, walimua kumpeleka hospitali waliyoshauriwa na madaktari akiambatana naye na daktari waliyekuwa naye safarini pia. Baada ya uchunguzi ilifahamika kuwa alisumbuliwa na Sukari na pia homa ya mapafu (Pneumonia),na hivyo akalazwa katika hospitali ile ya Poriya.

Mwakasege aliendelea kusema kuwa kabla ya Sedekia kuugua, walitembelea kanisa moja huko Israeli na Sedekia alikuwa amekwenda na kinanda chake (japokuwa ilikuwa ni safari ya mafundisho ya ndoa) hivyo alikitoa kinanda chake na akapewa nafasi ya kuimba. Aliimba wimbo ule wa “Bwana Mungu nashangaa kabisa” (Tenzi no. 114) na huo ndio ulikuwa wimbo wa mwisho wa Sedekia kuimba upande huu (kwani upande ule mwingine bado anaimba)
Mwalimu aliendelea kueleza namna Sedekia alivyougua, muda wa safari yao ulipokwisha ilibidi Mwl. Mwakasege abaki Israel kumuuguza Sedekia na wengine kurudi nyumbani.
Alieleza kuwa madaktari walijitahidi na kurekebisha hali ya sukari yake (iliyokuwa juu sana) na mapafu,lakini alipoteza fahamu na hakupata tena fahamu hadi uimbaji wake ulipohamishiwa mbinguni.

Katika ibada ile ileyohudhiriwa na watu wengi kuliko hata anapokuja rais wa nchi yetu huku Arusha, ilijawa na watu wa rika zote, na watu kutoka nchi mbalimbali. Mbunge mmoja alieleza pia namna walivyofahamiana na Sedekia, na mkenya mmoja aishiye Norway alieleza namna walivyokuwa wamepanga kwenda kupeleka Injili katika nchi zaidi ya tano za Afrika wakiwa na Sedekia, na kwamba aliwaambia anakwenda Israel na akirudi ndio wataanza safari hizo.

Ilifahamika kuwa Sedekia alikuwa na maono makubwa sana kwa ajili ya huduma yake kumtukuza Mungu huko mbeleni. Alikuwa na mpango wa kufungua studio yake ya muziki ya Injili, jambo ambalo, wote waliokuwepo siku ile waliazimia kuwa maono haya yasimamiwe na mke wake hadi studio ijengwe. Tukio hili wali walilitumia pia kusisitiza waimbaji waimbe katika roho kama alivyofanya Sedekia, na pia umoja kati yao ulisisitizwa sana jambo ambalo limeonekana kuanza kukua katika msiba ule.

Muda wote wa tukio hili, kwaya ya pamoja “Mass Choir” ilikuwa ikiimba nyimbo mbalimbali alizoimba Sedekia, lakini wimbo wa “Nimemwona Bwana….” Uliimbwa sana.
Tulipewa nafasi ya kutoa michango yetu kwa upendo kama sehemu ya kusema “pole” kwa familia yake.

Kumalizia mazungumzo yake, mwalimu Sedekia alianza kwa kumshukuru Mungu kwa kumpa Neema ya kuwa na Sedekia katika siku zake za mwisho (kwani aliwahudumia wengi lakini Mungu alipenda siku za mwisho wake awe na Mwakasege) na kuwashukuru watu wengine wote.

Alizungumza zaidi na kusema kuwa hakuna awezaye kuyapindisha mapenzi ya Mungu, na ya kuwa, mawazo ya Mungu yapo juu sana kuliko mawazo yetu sisi wanadamu. Ni nani ajuaye kuwa uimbaji wa Sedekia sasa unatakiwa zaidi mbinguni na Mungu kuliko hapa duniani?

Mwalimu Mwakasege alituonya ya kuwa “MUNGU ANAENDELEA KUWA MUNGU HATA KAMA HAKUJIBU TULIVYOTAKA, hivyo: Usimvunjie Mungu heshima yake ndani ya moyo wako, mwache aendelee kuwa Mungu daima” japokuwa Sedekia aliombewa nchi nzima ili asife,lakini Yeye Mungu anajua zaidi yetu.

Alimalizia kwa kutusihi watu wote tulioguswa na msiba huu, kila mtu ajiulize maswali haya matatu na apate jibu lake leo hii.(Ninamnukuu)

1. Kwanza jiulize, ukifa unataka ukumbukwe kwa lipi?
2. Baada ya kifo, zipo sehemu mbili tuu za kwenda, mbinguni na jehanam, je unataka ukifa uende wapi?
3. Je, Yesu Kristo akirudi leo, utanyakuliwa na Yeye au utabaki? (mwisho wa kunukuu)

Mwishoni ilitolewa nafasi ya watu wote kupita kwa mstari kwenda kutoa heshima za mwisho kwa mwili wake. Watu tulijipanga kwenye mistari iliyoanzia mwanzo hadi mwisho wa uwanja lakini watu hawakukata tamaa hata kidogo. Tulijipanga na kuanza zoezi hili ambalo halikuweza kufanikiwa kwani baadhi ya watu walishindwa kujizuia kwa vilio na kufanya hali kuwa ngumu, hali iliyopelekea zoezi hili kusitishwa na mwili wake kuchukuliwa na kupelekwa kuzikwa.

Ile siku ya mwisho, wote tuliookoka tutanyakuliwa na Bwana wetu Yesu Kristo, na tunaambiwa kuwa tutakutana wote ng’ambo ya mto, kama maneno ya ule wimbo wa “Shalll we gather at the river” (Ati twonane mtoni), tutakumbatiana na walioolewa wa vizazi vyetu na kisha tutaungana pamoja na tutakaribishwa kuingia katika karamu iliyoandaliwa katika Mji ule wa Yerusalemu mpya ambao hata sasa upo tayari kwa ajili yetu. Tuliookoka wote tusife moyo, Sedekia yupo na Bwana, na uzuri mmoja ni kwamba ipo siku tutakutana naye na kukaa naye pamoja na Bwana. Kusema ukweli, sasa yupo anaendelea kumwabudu Mungu huko juu kwa Baba yetu. Tushike sana tulichonacho.

Haya ndiyo niliyopenda kuwashirikisha siku hii ya leo.

“KWAHERI KAKA SEDEKIA, KATIKA SAA YA BWANA TUTAKUTANA PALE NG’AMBO YA MTO ULE”



www.lema.or.tz na Sayuni blog inamwomba Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo amtunze mke wake, watoto na familia yote, na Bwana atutie sisi wote NGUVU. Amen.

Frank Lema.
Arusha.

2 comments:

Anonymous said...

Ok, good coverage!

Ninashauri mfanye coverage za namna hii kwa waimbaji ambao wanaendelea na huduma hapa duniani. Coverage ya mwisho wa safari ya hapa duniani namna hii haiwezi kutosha kueleza mazuri yote ambayo mtu akiwa hai alikuwa anayafanya.

Nawatakieni tafakari njema!

Anonymous said...

Mungu akubariki kaka Lema,nilikuwa nasuburi kwa hamu ni lini utaweka habari hii kwa undani zaidi kama ulivyoa ahidi ziku ile ulipoweka habari hii kwa ufupi.Nimetiwa moyo sana kwa yote uliyoandika.Ni tukio ambalo kamwe sitalisahau niko nje ya nchi lakini niliguswa sana kwa msiba huu.Jumla ya yote MUNGU ATABAKIA KUWA MUNGU TU!YEYE NI MWEMA KTK YOTE!
Ahsanteni kwa kazi nzuri wana Sayuni.