Tuesday, July 16, 2013

Bishop Kakobe...

KAKOBE AKUMBUKE ALIPOANGUKIA, ATUBU-MCHUNGAJI

Katika gazeti la Nyakati toleo la Jumapili tarehe 14/7/2013 kuna habari inayozungumzia safari ya kihuduma ya Askofu Kakobe nchini Kanada ambako alifanya mkutano wa injili. Hata hivyo, inadaiwa kuwa safari hiyo imetoa picha kuwa huduma ya Askofu Kakobe imeshuka. Mmoja wa vyanzo vya habari hiyo ambaye ni mchungaji aliyefanya huduma na Askofu Kakobe amefanya mahojiano na mtandao wa fungukasasa, lakini akiomba jina lake lisitajwe. Endelea..
SWALI: Katika mahojiano ambayo sehemu yake imechapishwa katika gazeti la Nyakati la Jumapili tarehe 14/7/2013 ulionesha kutokubaliana na hoja kwamba mwenendo wa huduma ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe ni matokeo ya unabii uliotolewa na Mchungaji Antony Lusekelo wa Kanisa la GRC Kibangu, Dar es Salaam. Kwanza hebu waambie wasomaji tangu mwaka gani ulikuwa mchungaji katika kanisa la FGBF na uliondoka mwaka gani?

 JIBU: Mimi  niliwekewa mikono na Askofu Kakobe, na kuwa mchungaji tangu tarehe 3-3-1996 na nimekuwa katika utumishi muda wote hadi mnamo mwaka 2010.
SWALI: Ni muda wa kutosha. Katika muda huo wote kihuduma ulikuwa karibu kiasi gani na Askofu Kakobe?
JIBU: Ukaribu wangu na Askofu Kakobe ulikuwa  katika huduma, na zaidi sana yeye ndiye aliyekuwa mzazi na mlezi wangu kiroho, ndio ukaribu wangu na yeye kwa zaidi ya miaka 19.
SWALI: Kwa mtazamo wako kuna tofauti yoyote baina ya Kakobe wa wakati ule wewe ukiwa FGBF na Kakobe wa sasa?
  JIBU: Kama nimelielewa swali lako, nadhani unasema je,  Kakaobe wa sasa na alivyo kuwa zamani, ukweli ni kwamba, Askofu Kakobe alivyo sasa sivyo alivyokuwa miaka ya nyuma, zamani alizingatia sana Neno la Mungu na kuishi katika mapenzi ya Mungu, na ndio sababu Watanzania na Dunia kwa ujumla ilishuhudia uwepo wa Mungu juu yake, kama vile ishara maajabu na miujiza, leo hii, neema hiyo kwake imepotea! Amepoteza mwelekeo na kubaki na jina tu la uaskofu lakini kibali cha Mungu hakipo juu yake. Na hii inatokana kupenda pesa zaidi na kupenda sifa au kutafuta utukufu.
SWALI: Turudi kwenye msingi wa mahojiano haya. Unaamini kwamba huduma ya Askofu Kakobe imeshuka? Unatumia vigezo gani kubaki na mtazamo huo?
JIBU: Ndio naamini kwamba huduma yake imeshuka, kwanza kulikuwa hakuna huduma inayoleta watu wengi kwa Yesu kama huduma ya Kakobe, leo hii imekuwa kinyume, watu wengi wanaondoka katika huduma yake na kwenda duniani au kwenye mafundisho manyonge. Pia zamani ulikuwa ukipita mitaani na sehemu mbalimbali hapa nchini, Kakobe alikuwa ni mtu wa kuheshimiwa, leo ni mtu anayedharauliwa sana na watu, huko ni kushuka kwa huduma! Majuzi hapa alikuwa amekwenda Canada, na siku anaondoka, alisema anakwenda kuwahubiri maelfu ya watu, na akasema sababu mojawapo ya kuanza kwenda kuhubiri huko ni kwavile watanzania wameikataa kweli na wazungu wanaitaka kweli inayo hubiriwa na yeye. Ndugu mwandishi, ili ujue kwamba huduma yake inaelekea ukingoni, fuatilia mkutano wake huko, hakupata matokeo aliyotarajia, na ameshindwa hata kuonyesha picha za matukio ya mkutano wake kwenye ibada ya Jumapili iliyopita! Mungu si wa mchezo anaweza kukupandisha na anaweza kukushusha!
SWALI: Hivi wewe kama mchungaji huwezi kuamini kwamba pamoja na idadi ya watu au waumini kuzidi kushuka FGBC Mwenge, mikutano yake (kama huo wa Toronto, Kanada) kutokuwa na mahudhurio makubwa, lakini watu wengi wanaweza wakaendelea kuokoka na kujikabidhi mikononi mwa Yesu Kristo kutokana na kusoma machapisho yake au kutazama video za huduma yake zilizorekodiwa siku za nyuma? Ni lazima huduma ya Kakobe ifanyiwe tathimini kupitia tu mikutano na mahudhurio ya watu kanisani?
JIBU:  Ni kweli kwamba Askofu Kakobe anayo machapisho ya mafundisho yake kwenye video na kaseti za sauti na machapisho ya mafundisho kwa njia ya maandishi. Ndugu yangu, mtu anapokosa kibali kwa Mungu, hata mafundisho yake mazuri yanakuwa kama si kitu mbele za watu, mvuto na kiu ya yale mafundisho yake, ilitokana na kibali alichokuwanacho kwa Mungu.
SWALI: Wanadamu wanasema huduma ya Askofu Kakobe imeshuka, wengine wanaongeza  wanasema imeshuka sana. Haohao wanadamu wengine wanadai ni unabii wa akina Lusekelo waliomtabiria kuwa atadondoka alipowashambulia kwa kuruhusu waumini wanawake kuvaa suruali zenye kubana matako na nywele za bandia, maarufu kama ‘mawigi’ makanisani. Wewe umesema huna imani na unabii huo, badala yake unasema kuna mambo ambayo Kakobe ameyafanya, Mungu amemkasirikia na anapaswa afanye toba. Ni mambo gani hayo?
JIBU: Jambo ambalo naweza kusema hapa ni kwamba, Kakobe kilicho mfikisha hapo, ni kiburi, Biblia inasema, kijapo kiburi ndipo ijapo aibu, Kakobe amekuwa na kiburi cha juu sana, kwa mfano yeye h ujiona kuwa ndiye mwalimu na mtumishi mwenye mafundisho mazuri kuliko wengine wote, pili kuna wakati alisema yeye amefanya kazi kubwa kuliko Askofu Kulola, na hii aliisema sio kwetu tu wachungaji wake au kanisani, aliyanena hayo kwenye vyombo vya habari (tv) wakati ule alipomaliza kuyatembelea makanisa ya FGBF kote nchini. Huoni kama hicho ni kiburi cha hali ya juu sana!! Tatu hivi karibuni kuna wachungaji wamemshitaki Kakobe mahakamani, lakini watumishi mbalimbali wa Mungu (maaskofu) waliposikia wakamwendea na kumwambia sio vema kwenda kumalizana mahakamani na wachungaji wako, tunaomba tukae na wewe na wachungaji wako tutafute ufumbuzi ( tuwapatanishe), Kakobe alikataa kabisa, je huoni kuwa hicho ni kiburi? Na sio tu kiburi kwa wale watumishi waliomwendea, ni kiburi hata kwa Mungu aliyeagiza na anayemtaka kila mtu kupatana na mwenzake! Pia mambo mengine tunayoweza kusema kuwa ni chanzo cha Kakobe kuwa hivi ni kwamba, Kakobe amewaumiza watu wengi sana katika maisha yao kiroho na kimwili, leo kuna watu wameacha wokovu kwasababu ya Kakobe, leo kuna watu wanaishi maisha ya shida na kutokuwa na chochote
kwasababu ya Kakobe! Leo kuna wachungaji na waumini wa FGBF wanakosa hata nauli au chakula kwasababu ya Kakobe, leo kuna watoto wa washirika na wachungaji, wameshindwa kusoma kwasababu ya Kakobe! Majuzi majuzi hapa nimesikia kutoka kwa mmoja wa watoto wa Kakobe, kuwa baba yake (Kakobe) kuwa hakwenda kwenye mazishi ya mama yake mzazi huko Kigoma kijiji cha Kakonko, ndugu mwandishi, je unadhani hayo ni madogo mbele za Mungu?
SWALI: Pengine wakati msiba unatokea alikuwa kwenye huduma na ataenda kumzika mama yake kama hilo ni kweli. Sasa hebu waambie wasomaji wa mtandao huu, umekuwa mchungaji katika huduma ya FGBF kwa miaka yote hiyo, leo ungepata nafasi ya kukutana na Askofu Kakobe na akawa tayari kukusikiliza kama mtumishi wa Mungu nini ungemwambia?
JIBU: Mimi ningemwambia jambo moja muhimu ambalo ni sawa na maandiko, kumbuka ni wapi ulipoanguka na ukatubu, najua Kakobe anakumbuka mahali alipoanguka, pia ningemwambia, neno la Mungu linasema, nabii atakapotoa  unabii na usitimie, atadharauriwa na watu wote, alitoa unabii kuwa Mrema atakuwa Rais wa Tanzania mwaka 1995, na haikuwa hivyo. Awaombe msamaha aliowambia uongo na Mungu atamsamehe na kumpa heshima kubwa zaidi.
 
Source: http://www.fungukasasa.blogspot.com/2013/07/kakobe-akumbuke-alipoangukia-atubu.html

Thursday, July 4, 2013

Askofu Moses Kulola

WITO umetolewa kwa Watanzania kumuombea Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Moses Kulola ambaye ni mgonjwa na amekimbizwa nchini India kwa matibabu zaidi, Uwazi linakupasha.
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Moses Kulola.
Chanzo chetu cha habari kimesema wito huo umetolewa na familia ya askofu huyo ambapo awali Dk. Kulola alitibiwa katika Hospitali ya Bugando, Mwanza na baadaye Hospitali ya Kairuki jijini Dar lakini mapafu yakawa yanamsumbua na akawa anapumua kwa shida.
Habari zinasema ndugu na jamaa walipoona hali yake inatia simanzi wiki iliyopita wakaamua kumpeleka India katika Hospitali ya Apollo ambako amelazwa.
Kulikuwa na habari kuwa licha ya mapafu, kiongozi huyo wa kiroho alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo na moyo.
Habari zaidi zinasema mara baada ya kufika katika Hospitali ya Apollo, Askofu Kulola alifanyiwa vipimo na kugundulika kuwa ana tatizo la mapafu huku figo na moyo vikionekana havina matatizo.
Mwandishi wetu alizungumza na mtoto wa askofu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Willy Kulola ambaye ameongozana na baba yake India, amesema hali ya baba yake sasa inazidi kuimarika.
“Askofu amelazwa Hospitali ya Apollo na amepata huduma ya hali ya juu hapa na anaendelea vizuri. Ameletwa kutokana na kusumbuliwa na mapafu kwani alikuwa akipata shida kupumua,” alisema Willy.
Akifafanua zaidi alisema  walitarajia jana Jumatatu kupata ripoti maalum ya madaktari lakini vipimo vya awali vimeonesha kuwa hana matatizo katika moyo wake.
“Kinachomsumbua ni mapafu kwa sababu ya kazi kubwa ya kuhubiri lakini sasa ameimarika, amepewa dawa ili kurejesha afya yake lakini tunamshukuru Mungu hali yake ni njema,” alisema.
Kijana huyo aliwashukuru maofisa wa ubalozi wetu nchini India ambao wamekuwa wakimtembelea baba yake hospitali kumjulia hali.
Kabla ya kuugua, Askofu Kulola alikuwa akizunguka sehemu mbalimbali nchini kutangaza Neno la Mungu na alitarajiwa kumalizia ziara yake kwa kufanya mkutano mkubwa katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar.

Source: globalpublishers

Wednesday, July 3, 2013

MCHUNGAJI WA KANISA LA EAGT JIJINI MBEYA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 NA VIBOKO 12 BAADA YA KUBAKA NA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI

MCHUNGAJI WA KANISA LA EAGT JIJINI MBEYA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA 30 NA VIBOKO 12 BAADA YA KUBAKA NA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI



MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12 baada ya kukutwa na makosa mawili ya Kubaka na kumpa mimba Mwanafunzi wa miaka 19.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Mbeya Ndugu Gilbert Ndeuruo amesema Mahakama imemtia hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa na Shahidi namba moja katika kesi hiyo ambaye ni mhanga wa tukio hilo Neema Beni(19).

Amesema Mtuhumiwa huyo ilidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Mwezi Januari 2008 hadi Mwaka 2011 katika eneo la Iwambi kinyume na Sheria kifungu cha 130(2)e na 131 (1) sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwa kosa la ubakaji.

Kutokana na ushahidi huo Hakimu Ndeuruo alidai kuwa Mahakama yake imemkuta Mtuhumiwa na makosa mawili ya Ubakaji na kumpa ujauzito kwa ushahidi uliotolewa na Mhanga mwenyewe pamoja na Mwalimu wa Shule aliyokuwa akisoma ambapo alidai kuwa Shitaka limedhihirishwa pasipo shaka chini ya kifungu cha 235/1985.

Kwa upande wake Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa aliiomba Mahakama hiyo kutoa adhabu kali kutokana na mtuhumiwa kutenda kosa la kinyama tofauti na umri wake na wa binti ambapo Binti anaumri wa Miaka 19 ili hali Mtuihumiwa akiwa na Miaka 57.
Pia alidai kuwa Mtuhumiwa huyo alimharibia masomo na maisha yake binti huyo na vitendo hivyo alikuwa akivifanyia sehemu mbali mbali ikiwemo kanisani , hivyo aliiomba mahakama hiyo kuvitaifisha na kutoa amri ya Matunzo ya Watoto kwa kutumia amri ya kutaifisha.

Hata hivyo Hakimu alimuuliza Mtuhumiwa kuhusu kupunguziwa adhabu ambapo Mshtakiwa huyo aliomba kupunguziwa adhabu kwa madai kuwa ameachiwa watoto na ndugu zake aliozaliwa nao wakiwemo wazazi wake hivyo akifungwa hawatakuwa na msaada.

Aidha kutokana na utetezi huo Hakimu Ndeuruo alimhukumu kifungo cha Miaka 30 na viboko 12 kutokana na kosa la kwanza ili hali katika kosa la pili amehukumiwa kifungo cha Miaka 5 na kuongeza kuwa adhabu hizo zitaenda kwa pamoja na kulipa fidia ya Shilingi Milion 20 kwa fedha za Tanzania kwa familia ya Mhanga.

Ameongeza kuwa Mtuhumiwa anahaki ya kukata rufaa katika Mahakama kuu ya Mbeya kama hatakuwa ameridhika na adhabu aliyopewa na mahakama yake.


MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi akiwa mahakamani kungojea kesi yake

Wananchi Mbalimbali wakisubiri Kusikiliza Kesi ya MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi







MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi aliye vaa koti Jeupe akiwa anatolewa mahakamani Baada ya kusomewa kifungo cha Miaka 30 Jela



Watoto wa MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi wakiwa wanatoka Mahakamani Baada ya Baba yao kusomewa kifungo

Mtoto wa MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi akiwa anaongeaa na waandishi wa Habari baada ya kesi kumalizika

Waumini Mbalimbali wakiwa nje Baada ya kesi kumalizika

Watoto wa MCHUNGAJI wa Kanisa la Evangelical Assemblies of God of Tanzania(EAGT) la Iwambi Jijini Mbeya Daniel Mwasumbi wakiwa nje hawaamini baada ya kusikia Baba yao anafungwa Miaka 30
Binti anaye daiwa kufanyiwa kitendo hicho akilia kwa Uchungu baada ya kesi kwisha


Source: http://mbeyayetu.blogspot.com/2013/07/hot-news-mchungaji-wa-kanisa-la.html