Thursday, July 4, 2013

Askofu Moses Kulola

WITO umetolewa kwa Watanzania kumuombea Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Moses Kulola ambaye ni mgonjwa na amekimbizwa nchini India kwa matibabu zaidi, Uwazi linakupasha.
Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Moses Kulola.
Chanzo chetu cha habari kimesema wito huo umetolewa na familia ya askofu huyo ambapo awali Dk. Kulola alitibiwa katika Hospitali ya Bugando, Mwanza na baadaye Hospitali ya Kairuki jijini Dar lakini mapafu yakawa yanamsumbua na akawa anapumua kwa shida.
Habari zinasema ndugu na jamaa walipoona hali yake inatia simanzi wiki iliyopita wakaamua kumpeleka India katika Hospitali ya Apollo ambako amelazwa.
Kulikuwa na habari kuwa licha ya mapafu, kiongozi huyo wa kiroho alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo na moyo.
Habari zaidi zinasema mara baada ya kufika katika Hospitali ya Apollo, Askofu Kulola alifanyiwa vipimo na kugundulika kuwa ana tatizo la mapafu huku figo na moyo vikionekana havina matatizo.
Mwandishi wetu alizungumza na mtoto wa askofu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Willy Kulola ambaye ameongozana na baba yake India, amesema hali ya baba yake sasa inazidi kuimarika.
“Askofu amelazwa Hospitali ya Apollo na amepata huduma ya hali ya juu hapa na anaendelea vizuri. Ameletwa kutokana na kusumbuliwa na mapafu kwani alikuwa akipata shida kupumua,” alisema Willy.
Akifafanua zaidi alisema  walitarajia jana Jumatatu kupata ripoti maalum ya madaktari lakini vipimo vya awali vimeonesha kuwa hana matatizo katika moyo wake.
“Kinachomsumbua ni mapafu kwa sababu ya kazi kubwa ya kuhubiri lakini sasa ameimarika, amepewa dawa ili kurejesha afya yake lakini tunamshukuru Mungu hali yake ni njema,” alisema.
Kijana huyo aliwashukuru maofisa wa ubalozi wetu nchini India ambao wamekuwa wakimtembelea baba yake hospitali kumjulia hali.
Kabla ya kuugua, Askofu Kulola alikuwa akizunguka sehemu mbalimbali nchini kutangaza Neno la Mungu na alitarajiwa kumalizia ziara yake kwa kufanya mkutano mkubwa katika Viwanja vya Jangwani jijini Dar.

Source: globalpublishers

No comments: