Thursday, August 13, 2009

Ubatizo wa maji mengi au maji machache?

Yohana 3:3 “Yesu akamwambia, "Amen nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu."
Kuhusu ubatizo wa maji:
“Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.” [Yohana 3:5]
Bwana Yesu asifiwe!
Ninaamini kuwa wewe unaendelea vyema na Yesu ni mwema kwako pia, ndiyo, Yesu ni mwema.
Ndugu mmoja aliniandikia na kuomba ufafanuzi kuhusu suala zima la ubatizo kwetu sisi WaKristo. Ndugu huyu ameuliza ni ubatizo upi sahihi, wa maji mengi au maji kidogo? na akauliza je, mtu anatakiwa kubatizwa akiwa mdogo au mtu mzima ajuaye mema na mabaya? Anasema ameuliza hivi kutokana na mapokeo/imani zinazohubiriwa na makanisa mbalimbali tunayosali. Na mimi nimeona nimjibu kwa njia hii ili iwe faida kwa wote. Na nitamjibu kwa kadri Roho Mtakatifu alivyonipa kuelewa na kuamini ndani yangu. Kama ujuavyo, huduma hii ya mtandaoni haifungamani na dhehebu lolote lile.
Ubatizo ni agizo la Mungu kama tusomavyo katika Biblia, kwa mfano Mathayo 28:19:"Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu......" na pia mstari huo hapo juu wa Yohana 3:5.
Tunajua kuwa madhehebu mengi yamekuwa yakihubiri mengi kuhusu uwingi au uchache wa maji ya kubatizwa, lakini sijasikia waliojaribu kufikiri ni kwa nini Mungu anataka maji yatumike katika ubatizo, na isiwe kimiminika kingine chochote, na Bwana Yesu hakulizungumza hili. Lakini ninaamini kiini cha jambo hili ndio kimetajwa katika Waraka wa Kwanza wa Yohana 5:8-9 "Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno na Roho Mtakatifu na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani, Roho na maji na damu, na watatu hawa hupatana kwa habari moja....."
Hakuna mahali Biblia inapotaja tutumie kiasi gani cha maji katika ubatizo, kama tulivyoona, Biblia inasema tuu kuwa tutumie maji. Ili mradi maji yapo, mbatizaji anaweza kuamua atumie maji kiasi gani. Anaweza kubatizia baharini, ziwani, mtoni au kwa matone machache ya maji, mradi tuu maji yawepo pale kwani ni mojawapo ya washuhudiao hapa ulimwenguni.
Ubatizo wa maji kidogo ni sawa, na ubatizo wa maji mengi ni sawa (huo wingi wa hayo maji unatofautiana pia).Hivyo ndivyo tunavyotakiwa kuamini na kutokukubali kuyumbishwa na mtu yeyote pasipo ridhaa yetu.Wazungu wana msemo usemao "A man living by the river never uses spittle of water for washing", yaani mtu aishiye kando ya mto hatotumia matone ya maji kwa kuoshea, kwa sababu anayo maji mengi.Hali kadhalika,Yohana Mbatizaji angeweza kuamua kubatizia watu mtoni kwa sababu alikuwa karibu na mto Yordani. Mtu ana uchaguzi huru wa kuamua kubatizwa kwa maji kidogo au mengi kiasi gani, kama atakavyopenda yeye mwenyewe. Kwa mfano leo, tukiamua sisi tuliookoka wa Tanzania, tukajikusanya na kuamua kwenda kuhubiri injili kule Darfur, Sudan, na tukaambiwa na waandaji wa huduma hiyo kuwa kule tutakapokwenda kuhubiri injili ni jangwa tupu, hakuna maji mengi kama tulivyonayo huku kwetu, je tutafanyaje basi? Je, tutakataa kwenda kuhubiri kwa sababu kule hakuna maji mengi ya kubatizia? Je, tutaacha kufungasha Biblia katika mabegi yetu na badala yake tutabeba maji ili tukifika kule tutengeneze mto wa kubatizia? La Hasha! Ukisoma kitabu cha "A table in the presence" kilichoandikwa na Lt.Carey H. Cash, ambaye ni Mchungaji wa Jeshi la Marekani (Military Chaplain) aliyeshiriki vita ya Iraq, utaona kuna mahali ameeleza habari za Mchungaji mwanajeshi mwingine aliyekuwepo katika vita ya Vietnam, alijiwa na askari wakitaka kubatizwa kabla ya kuelekea kwenye mapambano, lakini wakati huo hakuwa na hata tone la maji, na alijua wazi kuwa kwa mazingira ya vita,baadhi ya wale askari waliotaka kubatizwa anaweza asiwaone tena baada ya pale kwani wanaweza kufa vitani, hivyo hawezi kuwaambia "Njooni baadaye",ungekuwa wewe ungefanyaje? Anasema yule mchungaji katika hali ile (kwa alivyoamini) aliamua kutumia mate yake kuwabatiza, na akawabatiza!
Ninafikiri kinachotokea katika mwili wa Kristo sasa hata watumishi wa Mungu hawashirikiani katika kuujenga mwili wa Kristo ni mbinu tuu za shetani za kutaka kututenganisha ili tusiwe na umoja Bwana aliotuombea katika Yohana 17.Nafikiri unaweza ukawa umeona namna madhehebu yalivyojitenga, kila mmoja akieleza ubaya wa dhehebu lingine badala ya kueleza ubaya wa shetani. Shetani anataka kumfanya kila Mkristo ajione kuwa bora kuliko mwenzake na tusiweze kuungana katika kumpinga ibilisi.
Kuhusu kiasi cha maji ya kubatizia kiasi chochote kinafaa, kila mtu na afanye kama apendavyo,mradi tuu maji yatumike.
Kuhusu ubatizo wa watoto au watoto wazima, ninaona pia kuwa kila watu na wafanye wapendavyo wenyewe. Wapo wanaoamini kuwa mtoto hawezi kubatizwa,na kwamba lazima mtu aokoke kwanza ndio kisha abatizwe (kwa sababu Biblia imesema kuwa "Aaminiye na kubatizwa ataokoka"), na wapo wanaoamini mtoto mchanga anaweza kubatizwa (“Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.” [Yohana 3:5] -ameanza kwa maji, yaani kubatizwa na kisha kwa Roho(kuokoka)) hivyo hawa huanza kubatiza kwanza na kisha wokovu, ingawa akitokea mtu mzima katika madhehebu hayo hajabatizwa (kwa mfano mshirika mpya) hubatizwa pia.
Siyo lazima mtu awe mdogo au awe mkubwa ili abatizwe,ubatizo ni kwa yeyote yule. Ndiyo maana kuna baadhi ya watu walipata neema ya kuokoka wakiwa bado watoto wadogo sana, hadi miaka sita,je hawa wakiokoka tuwazuie kubatizwa kwa sababu ni wadogo? Hebu soma kilichotokea kwa Mtume Petro katika Matendo 10:44-48.
Ushauri wangu mimi, Ubatizo wa maji mengi ni sawa na wa maji kidogo ni sawa, mradi maji yanatumika hakuna ulio bora kuliko mwingine, pia, kubatiza watoto wadogo ni sawa, kubatiza wakubwa ni sawa,hakuna ulio bora kuliko mwingine, nami ninaamini kuwa nina Roho Mtakatifu.
Tusikubali tena shetani aendelee kututenga sisi tulio viungo katika mwili mmoja wa Kristo, ndiyo kusema, Tujenge madaraja (ya kutuunganisha) na siyo kuta (za kututenga). Na tukumbuke, siku ya mwisho watakaoingia mbinguni ni wale ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima, yaani waliookoka,na siyo waliobatizwa. Wapo waliobatizwa ambao hawataingia mbinguni kwa sababu hawajaokoka.(Kwa hivyo unajua ni wapi pa kuweka bidii kubwa)
"Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.”-Ufunuo wa Yohana 20:15.
Kwa utukufu wa Mungu,
Frank Lema
www.lema.or.tz
savedlema2@yahoo.com

1 comment:

Anonymous said...

Wewe ni mwongo sana, Ubatizo ni neno lenye asili ya kiyunani baptizo lenye maana ya kuzamishwa kabisa, biblia haituoneshi ubtizo wa maji kidogo, filipo alimbatiza mkushi sehemu yenye maji mengi, kadhalika Yesu alibatizwa kwa maji mengi. Maana ya kubatizwa ni kuzika dhambi zetu na kuzaliwa upya ndani ya Yesu, sasa huwezi kuzikwa nusu (kunyunyiziwa maji kidogo), huu ni ubatizo wa kishetani ambao ulianza enzi za mfalme kostantino kipindi cha utawala wa rumi. Soma biblia upate maarifa