Thursday, August 27, 2009

Waislamu kuzindua mwongozo wa uchaguzi Alhamisi

SHURA ya Maimamu wa Tanzania, kesho inatarajia kuzindua rasmi mwongozo kwa Waislamu kuhusu uchaguzi mkuu wa 2010 na moto wa siasa za ukombozi.
Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 8:00 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari Kinondoni jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa kamati kuu ya siasa ya taasisi hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema uzinduzi huo utahudhuriwa na zaidi ya masheikh 100 kutoka katika mikoa 22 ya Tanzania Bara.
Alisema mwongozo huo utagusia masuala mbalimbali ya kitaifa yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“Mwongozo unahusisha masuala ya elimu, afya, uchumi, demokrasia, siasa na kilimo. Mambo mengi zaidi tutayaeleza katika uzinduzi ,” alisema Sheikh Ponda.
Alisema kila mkoa utatoa masheikh watano ambao watawawakilisha Waislamu wa mikoa yao na baadaye kuwarejeshea salamu za pamoja za Waislaam kwa serikali ya CCM.
Alisema mWongozo huo utakuwa na salamu na ujumbe maalum kwa serikali kufuatia kitendo chake cha kukaa kimya wakati Kanisa Katoliki, lilipotoa waraka ambao kimsingi unahatarisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.
“Ndani ya mwongozo wetu kuna ujumbe maalum kwa serikali ya CCM kwa kule kakaa kimya kwake kimya baada ya Kanisa Katoliki kutoa waraka ambao kimsingi jamii na serikali zinajua kabisa kwamba unahatarisha umoja wa kitaifa,” alisema Sheikh
Ponda.
Alisema huko nyuma, viongozi wa madhehebu ya Kiislamu walijaribu kutoa elimu ya uraia, lakini serikali iliwakamata na kuwawe ndani kwa madai ya uchochezi.
"Je waraka na ilani ya Wakatoliki hazileti uchochezi,” alihoji Ponda.
Alisema mwongozo huo utaweka mwelekeo na msimamo wa pamoja wa Waislamu kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu na uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani utakaofanyika mwakani

Source: Mwananchi

No comments: