Thursday, August 20, 2009

Ukizaliwa mara moja utakufa mara mbili, ukizaliwa mara mbili utakufa mara moja tuu!

Ukizaliwa mara moja utakufa mara mbili, ukizaliwa mara mbili utakufa mara moja tuu!

Bwana Yesu Asifiwe!

Daima namshukuru Mungu kwa neema zake na upendo wake mkuu kwetu sote (ni vyema kumshukuru Mungu kwa baraka zake kwetu, tunazoziona na tusizoziona) ile tuu kuweza kusoma ujumbe huu ni neema yake.

Karibu tena tushirikiane Neno la Mungu litakalotuongoza katika maisha yetu yote. Leo tutatafakari ujumbe huu unaosema “Kama umezaliwa mara moja tuu utakufa mara mbili, na kama umezaliwa mara mbili, utakufa mara moja”.Ndiyo, hii ina maana kuwa kuna kuzaliwa mara mbili na pia kuna kufa mara mbili.

Hebu tafakari mstari huu wa Yohana 3:3 “Yesu akamwambia, "Amen nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu." Maneno haya Bwana Yesu alikuwa akimwambia kiongozi wa kikundi cha Mafarisayo aitwaye Nikodemo. Nikodemo alikuwa hajafahamu bado ni nini maana yake kuzaliwa mara ya pili, na ndipo Bwana Yesu akamfunulia zaidi: “Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.” [Yohana 3:5]. Na pia “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili, na kilichozaliwa kwa Roho ni Roho. Usishangae basi ninapokwambia, ni lazima uzaliwe mara ya pili” [Yohana 3:6-7]
Bwana Yesu hapo kwenye mistari hiyo anaonesha kuwa kuna kuzaliwa mara ya kwanza na kuna kuzaliwa mara ya pili pia. Na anaendelea kwa kuweka wazi kuwa kuzaliwa mara ya kwanza hakutufanyi sisi tuoone ufalme wa Mungu (ndio maana kuna waliobatizwa wengi hawataingia mbinguni kwa sababu hawajaokoka), bali ni kuzaliwa mara ya pili (kuookoka) ndiyo kunatupa sisi neema ya kuuona ufalme wa Mungu [Yohana3:3].

Ni vyema kujiuliza, kuzaliwa mara ya kwanza na kuzaliwa mara ya pili ni kupi? Yule ndugu aitwaye Nikodomo aliposikia kuhusu kuzaliwa mara ya pili, lilikuwa ni jambo jipya kwake, hivyo akamuuliza Bwana Yesu:
“Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili! "[Yohana 3:4] ni wazi kuwa Nikodemo hakuwa amemwelewa Bwana Yesu, ndipo Bwana Yesu akamjibu katika mstari huo hapo juu akimwambia, “Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho {Roho Mtakatifu} hawezi kamwe kuuona ufalme wa Mungu.” Hapa sasa tunaelewa kuwa ‘kuzaliwa mara ya kwanza’ kunamaanisha ubatizo wa maji, na ‘kuzaliwa mara ya pili’ kuna maanisha kuzaliwa kwa Roho Mtakatifu, yaani kuokoka.

Kwa hiyo sasa tunaona kuwa ni kwa lugha ya sasa hivi mstari ule wa Yohana 3:3 tunaweza tukautafsiri hivi “Yesu akamwambia, "Amen nakwambia, mtu asipookoka hataweza kuuona ufalme wa Mungu.” Ndiyo ujumbe wetu wa leo, mtu asipookoka hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.

Je, ni nini kitatokea kwa waliokokoka na wale wasiokokoka?

Ninaamini unafahamu vyema kuwa ile siku ya mwisho, siku ya hukumu itakapofika, kama Biblia inavyosema, watu wote wa nyakati zote watakusanyika mbele za Mungu na hapo hukumu itatolewa. Kila mtu anapookoka, jina lake linaandikwa kwenye kitabu kule mbinguni sekunde ile ile anapoisema sala ya kuokoka. Kwa hiyo, itakapofika ile siku ya mwisho, watu wote waliokuwa wameokoka wakiwa hapa duniani majina yao yatakuwa kwenye kile Kitabu. Hivyo majina yatasomwa, na wale ambao majina yao yameandikwa humo wataingia katika ule mji wa Yerusalem mpya ulio tayari hata sasa. Wale ambao majina yao hayaandikwa kwenye kile Kitabu hao watatupwa katika lile ziwa la moto, liitwalo jehanamu pamoja na ibilisi na malaika zake waovu. Ni vyema kuyafahamu mambo haya kama yalivyoandikwa kwenye Biblia katika mistari ifuatayo:

Ufunuo 20:13-15: “Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; kifo na kuzimu vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana na matendo yake.Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili.Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.”

Ufunuo 21:27: “Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo ndio watakaoingia ndani.”

Tumeshaona ni nini maana ya kuzaliwa mara mbili, sasa tuone ni nini maana ya kufa mara mbili?. Kufa kwa mara ya kwanza ni kifo kile tutakachokufa hapa duniani wakati wa Bwana unapofika, yaani kifo cha mwili huu wa nje tunaotembea ndani yake. Kifo cha pili ni kile kilichoelezwa katika Biblia, Ufunuo 20:14 “Kisha mauti na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili.” Naam, Biblia inasema kuwa, kutupwa katika ziwa lile la moto ndiyo kufa mara ya pili. Kwa hiyo wale wote ambao watakuwa hawajaokoka [yaani walizaliwa mara moja tuu kwa kubatizwa], watakufa hapa duniani na pia siku ya hukumu watahukumiwa kifo cha pili {yaani ziwa la moto}, kwa hiyo hawa watakufa mara mbili. Lakini wale wote watakaokuwa wamekubali kuokoka [yaani kuzaliwa mara mbili, kubatizwa na kuokoka], watakufa hapa duniani lakini baada ya hapo hawatakufa tena, bali tutaishi milele, kwahiyo, waliookoka wote watakufa mara moja tuu. Na hiyo ndiyo maana ya ujumbe wetu wa leo, “Ukizaliwa mara moja utakufa mara mbili na ukizaliwa mara mbili utakufa mara moja tuu”

Je, wewe umeokoka?

Ni swali lako binafsi. Je, wewe umeokoka (kuzaliwa mara ya pili)? Kuokoka siyo dini wala dhehebu jipya. Ni wazi kuwa hatujamsikia Bwana Yesu katika Biblia akiwaambia watu waingie dhehebu fulani ili wauone ufalme wa Mungu, Yeye alisema tuu ni lazima kuzaliwa mara ya pili, yaani kuokoka. Kuokoka ni uhusiano wako binafsi na Bwana Yesu Kristo.

Kama umeokoka, basi huu ni ujumbe wa kukutia moyo, songa mbele katika wokovu maisha yako yote. Kama hujaokoka na umeupata ujumbe huu, basi ninakupa shauri ufanye kama Bwana Yesu alivyoagiza, yaani uokoke. Ukiokoka Bwana Yesu atakusamehe dhambi zako zote kama ilivyoandikwa 1Yohana 1:7 “Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na Damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote.”

Kama unataka kuokoka sasa
bonyeza hapa.

Ubarikiwe na Mungu aliye juu mbinguni, tuzidi kuombeana.

Katika utumishi Wake,

Frank Lema
www.lema.or.tz
savedlema2@yahoo.com

Arusha, Tanzania.
Aug 13th, 2009.

1 comment:

Mary Damian said...

Mungu akubariki sana kwa Neno.