Wednesday, August 19, 2009

CCM yatoa tamko kuhusu Waraka wa Wakatoliki, Mahakama ya Kadhi

HALMASHAURI Kuu ya CCM imeiagiza serikali kukutana na viongozi wa dini ili kufanya mazungumzo yatakayosafisha hali ya hewa iliyochafuliwa na waraka wa Kanisa Katoliki (RC), kuhusu uchaguzi, huku ikiridhia kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nje ya mfumo wa dola.
Waraka wa Kanisa Katoliki umekuwa ni gumzo kubwa katika miezi ya karibuni kutokana na kuzungumzia jinsi ya kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, huku wanaoupinga wakidai kuwa, utawagawa wananchi katika misingi ya kidini.
Chiligati aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, Nec imeagiza viongozi wakuu wa nchi kukutana na viongozi wa dini ili kufanya mazungumzo kwa lengo la kusafisha hali ya hewa na kujenga umoja na utengamano katika jamii.
RC imekuwa ikiwataka wanaoupinga waraka huo kueleza udhaifu wake badala ya kutoa maoni ya kiujumla kuwa haufai, kama ambavyo mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru amekuwa akiupinga.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, CCM imesema inaunga mkono msimamo wa serikali kutaka suala hilo lianzishwe nje ya mfumo wa dola.
Katika ilani yake ya uchaguzi wa mwaka 2005, CCM iliahidi kulipatia ufumbuzi suala la Mahakama ya Kadhi, lakini katika miezi ya karibuni Waislamu wamekuwa wakishinikiza kutaka kuanzishwa kwa chombo hicho wakidai kuwa, CCM iliwahadaa kwa kuahidi kuwaundia chombo hicho.
“Halmashauri Kuu imesisitiza kuwa iwapo Waislamu wanaona haki zao hazikamiliki bila ya kuwa na chombo cha aina hiyo, wasizuiwe, alisema Chiligati.
“Waruhusiwe kuanzisha Mahakama ya Kadhi wao wenyewe na serikali isijihusishe kuiendesha mahakama hiyo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa imejiingiza katika shughuli za kidini.”
Kwa mujibu wa Chiligati, mahakama hiyo haitajihusisha na kesi za jinai wala madai badala yake itakuwa ikishughulikia masuala ya ndoa, talaka na mirathi.
Katika mkutano huo wa Nec, Jasson Rweikiza alichaguliwa kuziba nafasi ya ujumbe wa chombo hicho kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa.
Rweikiza alipata kura 88 na kumbwaga kwa tofauti ya kura tatu mpinzani wake wa karibu, Ramadhani Maneno ambaye alipata kura 85 huku mwanamke pekee katika kinyang'anyiro hicho, Sifa Swai akiambulia kura 46.
Jambo lingine lililojiri ndani ya kikao hicho kikubwa ni pamoja na uteuzi wa makatibu wa mikoa. Katika uteuzi huo, Sauda Mpembalyoto, ambaye alikuwa katibu wa wilaya ya Hai na kapteni mstaafu wa jeshi, Frarten Kiwango ambaye alikuwa katibu wa wilaya ya Kibaha Mjini, waliteuliwa kuwa makatibu lakini vituo watapangiwa baadaye.
Source: Mwananchi

No comments: