Thursday, August 20, 2009

Wapinga tamko la CCM kuhusu Mahakama ya Kadhi

Baadhi ya Waislamu jijini Dar es Salaam wamepinga kauli ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutaka Mahakama ya Kadhi ianzishwe nje ya mfumo wa serikali.
Aidha, hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuagiza Serikali kukutana na viongozi wa dini, kufanya mazungumzo ili kusafisha kile ilichodai hali ya hewa imeelezwa kutokana na chama hicho kukosa ujasiri na kukumbatia ufisadi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa kutetea haki za Waislamu Tanzania Issa Ponda alisema, kufanya hivyo ni kutaka kuwaundia Waislamu mahakama wasioiahidi tofauti na walivyoahidi kupitia ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2005.
"Kusema kwamba Mahakama ya Kadhi ianzishwe nje ya mfumo wa serikali ni kutaka kututengenezea mahakama ambayo hawakuiahidi, kwa sababu ilani ya CCM haukusema hivyo," alisema Ponda.
Ponda aliongeza kuwa, "Kabla ya Mahamakama ya Kadhi haijavunjwa nchini ilikuwa ikiendeshwa na serikali, na CCM walipotamka kuwa watairejesha walikusudia kuirejesha ile ya zamani, sasa kukiuka hayo ni usanii."
Ameitaka serikali iingize mahakama ya kadhi katika mamlaka yake ili itambulike kisheria na iiendeshe kama vile ilivyosaini mkataba wa kuyahudumia makanisa kupiia "Memorandum of Understand".
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema Dk, Willibrod Slaa alisema kuwa mbali na CCM kukosa ujasiri hatua hiyo ni sehemu ya rushwa. Alisema iwapo viongozi wa dini watakubali kukutana na kuongea kwa siri na serikali watakuwa wamenunuliwa.
"CCM kutaka serikali ikutane na viongozi wa dini kwa mazungumzo ya siri ni kitendo kisicho cha ujasiri, ni sehemu ya rushwa," alisema Dk. Slaa na kuongeza; Nitawashangaa viongozi wa dini watakaokubali kukaa na Waziri Mkuu kwa siri na kunywa naye chai kwa mazungumzo hayo."
Akizungumzia hatua ya CCM kupinga waraka uliotolewa na Kanisa Katoliki huku mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru akishika bendera, Dk Slaa alisema hatua hiyo haina tofauti na kuunga mkono ufisadi.
Alisema inashanga kuona watu wanapinga waraka ambao unaelekeza namna ya kupata kiongozi muadilifu, asiye fisadi, mla rushwa au mbinafsi anayeweza kupatikana katika imani yoyote ya dini.
"Yeyote anayetaka kupinga waraka wa Wakatoliki ni fisadi kwa sababu unazungumzia maadili mema ya kiongozi bila kuelekeza atoke dini gani: Kwenye wapagani kuna waadilifu, Uislamu kuna asiye fisadi hata dini nyingine wapo wasiokula rushwa. Yeyote anayekataa hilo sina jingine ni fisadi tu."
Kwa Kingunge sishangai, kupinga waraka ule kwani hata majina ya mafisadi pale Mwembe Yanga alikuwa wa kwanza kuyapinga akisema wapinzani ni waongo, sasa Kiko wapi?," alihoji Dk Slaa na kuongeza: Kama unamkataa asiye fisadi basi wewe ni fisadi, sisi tunawombea Mungu CCM waendelee kupingana na wapinga ufisadi." Alisema CCM imefika mwisho wake na haifai tena mbele ya jamii kwa kuwa inakumbatia ufisadi tena bila kificho.
Akizungumzia tamko la CCM kuitaka serikali ikutane na viongozi wa dini ili kusafisha hali ya hewa iliyochafuliwa na waraka wa Waraka wa Kanisa Katoliki , Ponda alisema njia itakayoweka hali hiyo kuwa nzuri ni Waislamu kuandaa waraka wao ambao alisema watautangaza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
"Hakuna njia itakayorejesha hali nzuri zaidi ya sisi nasi kutoa waraka wetu.Tuko katika hatua za mwisho kuukamilisha na ifikapo mwishini mwa mwezi huu(Agosti) tutautangaza"alitangaza Ponda.
Aidha Ponda alimshutumu Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi) John Chiligati kwa kuiamuria Kamati Kuu kwani kikao cha kujadili hayo hakijafanyika wala kutoa maamuzi juu ya hilo.
Chiligati juzi akiwa kwenye kikao cha NEC aliagiza serikali kukutana na viongozi wa dini ili kufanya mazungumzo ya kusafisha hali ya hewa iliyochafuliwa na waraka wa Wakatoliki na pia kuitaka serikali ianzishe mahakama ya kadhi nje ya mfumo wa dola.

Source: Mwananchi

No comments: