SERIKALI imetangaza kufuta leseni zote za waganga wa jadi kuanzia Ijumaa Jan. 23, 2009 ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya mauaji ya Albino na Vikongwe nchini.
Amri hiyo ilitangazwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga leo mwishoni mwa ziara yake ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhamasisha mapambano ya Serikali dhidi ya mauaji hayo.
Waziri Mkuu alisema kuwa aliwasiliana na Mwanasheria Mkuu kuhusu uamuzi wa kuchukua hatua hiyo ya kufuta leseni hizo na Mwanasheria Mkuu akasema jambo hilo linawezekana.
"Kuanzia leo leseni zote za waganga wa jadi futa… Mtu yeyote akiendelea na kazi hiyo mfuatilieni," aliwaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakuu wa Halmashauri zote za Jiji, Miji na Wilaya nchini.
Waganga wa jadi wamekuwa wakituhumiwa kuwa ndiyo chimbuko la mauaji hayo kwa vile wao ndiyo hupiga ramli za kuelekeza hivyo.
Katika mikutano na viongozi wa mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Tabora na Shinyanga, wachangiaji wengi waliitaka serikali kufuta leseni hizo. Hata baadhi ya waganga wa jadi waliochangia walikiri.
Waganga wa jadi husajiliwa na kupewa leseni za kufanya kazi zao na Halmashari kwa utaratibu wa kiutawala. Ipo sheria ya mwaka 2002 kuhusu Tiba Asilia na Tiba Mbadala (Traditional and Alterntive Medicine Act), lakini Kanuni za utekelezaji wake zilikuwa hazijatengenezwa.
Waziri Mkuu alisema mganga wa jadi ambaye anaweza kuruhusiwa baadaye ni yule ambaye dawa zake za mitishamba au za asili zitakuwa zimethibitishwa na Kitengo cha Uchunguzi wa Tiba Asili cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa kweli zinatibu. Mgonjwa naye atatakiwa awe na cheti kutoka hospitali kitakachothitisha maradhi yake na kuwa tiba yake hopitali imeshindikana. "Waganga hawa ni waongo wakubwa…Siyo lazima kuwa nao.
Wangekuwa waganga wa kweli magonjwa mengi yangepungua nchini, lakini magonjwa yapo na sasa wanapiga ramli na kuwa kichocheo cha mauaji. Mkoa wa Shinyanga unasemekana unaongoza kwa idadi ya waganga wa jadi waliosajiliwa na wako 1,104 na 94 ambao hawakusajiliwa.
Wilaya ya Kahama peke yake ina 763. Waziri Mkuu aliuambia umati uliofurika kwenye uwanja wa Chuo cha Biahshara cha Shinyanga (Shycom) huku akishangiliwa kuwa mapambano dhidi ya mauaji ya Abino ni vita na ndiyo maana anataka ulinzi wa jadi wa Sungusungu urejeshwe kusaidiana na vyombo vya dola kukabiliana na hali hiyo.
Aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa kufnya kazi zao kwa ufanisi zaidi na "kujipanga upya na kuteremka hadi ngazi ya chini" kusimamia mapambano dhidi ya mauaji ya Albino na Vikongwe.
"Inapotokea kuwa Albino au Kikongwe anauawa katika eneo fulani, mimi nitamshukia Mkuu wa Mkoa na kumuuliza kwa nini aliacha hali itokee hivyo. Mkuu wa Mkoa naye atamshukia Mkuu wa Wilaya na vivyo hivyo," alisema.
Aliongeza: "Tukijumuika wote kwa pamoja tutashinda vita hii kama tulivyoshinda vita dhidi ya nduli Idi Amin wa Uganda". Waziri Mkuu pia alisema atamwomba Jaji Mkuu kuwa zile kesi za mauaji ya Albino ambazo ziko tayari zinapangiwa majaji maalum ili zikamilike na hatima yake ijulikane haraka.
Tangu Juni mwaka 2007 mpaka Novemba mwaka 2008 jumla ya Albino 34 wameuawa nchini kwa imani za ushirikina kuwa eti viungo vyao vinasaidia kupata utajiri.
Idadi yao kimkoa kwenye mabano ni Mwanza (19) Mara (4) Kigoma (3) Shinyanga (4), Kagera (3) na Mbeya (1). Mwaka huu tayari wameuawa watatu.
Jumla ya vikongwe waliouawa nao kwa kushukiwa wachawi ni 2583 ambapo idadi yao kimkoa kwenye mabano ni Mwanza (696), Shinaynga (522), Tabora (508), Iringa (256), Mbeya (192) Kagera (186), Singida (120) na Rukwa (103).
Ziara ya Waziri Mkuu Pinda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa inamalizika leo kwa majumuisho yatakayowahusisha viongozi wa mikoa hiyo. Alianzia Kagera na badaye kutembelea mikoa ya Mwanza, Tabora na Shinyanga.
Mkoa wa Mara ulijumuishwa kwa viongozi wake kuhudhuria mkutano wa viongozi Mwanza.
1 comment:
I will like to slide my pages up and down because its easier for me when I am holding my iphone with one hand. I have cydia. If you know a way please let me know. Thanks
[url=http://unlockiphone22.com]unlock iphone[/url]
Post a Comment