Friday, January 30, 2009

Waziri mkuu aangua kilio bungeni

Hoja ya wapinzani kumtaka ajiuzulu yayeyuka

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameangua kilio bungeni kuonyesha uchungu alio nao dhidi ya vitendo vya mauaji ya kikatili ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), hivyo kuyeyusha hoja ya wabunge wa upinzani waliokuwa wamepania kumbana, ili ajiuzulu kwa madai kwamba, alitoa amri ya kuua wauaji ambayo ni kinyume na katiba ya nchi.
Hali hiyo ilitokea jana bungeni, wakati Pinda akielezea yaliyomfanya atoe kauli hiyo tata kikatiba na misingi ya haki za binadamu.
Pinda alisema alipokuwa katika ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, alipata taarifa za kusikitisha kuhusu mauji ya albino na mara kesho yake habari zikatoka kwenye vyombo vya habari kwamba, albino mwinge kauawa.
"Jamani jamani taarifa za matukio hayo kibinadamu zinatia uchungu sana na kumfanya mtu ashindwe kujizuia….," mara akaanza kutokwa machozi na kukatisha maelezo yake akatoa miwani na kujifuta huku wabunge wakiwa kimya.
Waziri Mkuu alisema hayo baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed, kumtaka atoe ufafanuzi kuhusu kauli aliyoitoa hivi karibuni akiwa katika ziara Kanda ya Ziwa, kuwaruhusu wananchi kuwaua watu watakaokutwa wakimchinja albino.
Hamadi alisema katiba ya nchi inamlinda mtu kupewa nafasi ya kujitetea, hivyo akamtaka waziri afafanue maana ya kauli yake, kwa kuwa ni kinyume na taratibu ambazo nchi imejiwekea katika kuhakikisha haki inapatikana.
Pinda alisema mtu anaposikia au kusoma taarifa za mauaji ya albino, hawezi kupata hisia juu ya mateso wanayoyapata, sawa na anayewasikiliza watu walionusurika kufa au walioshuhudia vitendo hivyo vikitendeka.
“Mimi walinihadithia, aah! Samahani," alisema kwa masikitiko Pinda huku akiwataka radhi wabunge kwa kushindwa kuendelea kueleza kwa jinsi alivyoguswa na matukio hayo. Mara akaanza kububujikwa na machozi na baada ya sekunde kama 15, alichukua kitambaa chake akajifuta.
Aliendelea kuelezea jinsi maalbino wanavyouawa kikatili, akisema wengi walikufa kwa kushindwa kupata huduma mapema ya kuzuia damu baada ya ama kukatwa mikono ama miguu na majitu hayo katili yenye imani potofu kwamba, viungo hivyo vinaweza kumpatia mtu utajiri.
Alisema alielezwa kuwa, wauaji wanachokifanya ni kumshambulia albino na kumkata kiungo wanachokitaka kwa kutojali hali wanayomuacha nayo kama ni mateso, kufa au kupona hivyo alipatwa na uchungu kiasi cha kujikuta anatamka kuwa, watu wanaokutwa wakitenda hayo nao wanapaswa kuadhibiwa papo hapo.
Alifafanua kuwa wakati akiwa kwenye ziara hiyo iliyokuwa maalumu kwa ajili ya kukemea na kupanga mikakati ya kukabaliana na vitendo hivyo, idadi ya maalbino waliouawa walikuwa 30 na baada ya kukemea vitendo hivyo, ghafla akapewa ripoti ya kuuawa wengine wawili, jambo ambalo lilizidi kumuudhi na kumchanganya.
Waziri Pinda aliwaomba radhi watu walioudhika kutokana na matamshi na pia akimuomba Mungu amsamehe iwapo amewakosea.
"Kama mnaona kile nilichofanya ni makosa naomba mnivumilie. Naomba Mungu anisamehe kama nimewakosea," aliomba Waziri Mkuu na kuongeza kuwa serikali imechukizwa sana na mauaji hayo ya kikatili.
Alisema Tanzania imekuwa ikiheshimika sana katika jumuiya ya kimataifa, lakini mauaji ya albino na ya vikongwe katika eneo hilo yameitia doa.
Alielezea pia kuhuzunishwa zaidi na tamko la Bunge la Jumuiya ya Ulaya (EU) la kulaani mauaji hayo, kana kwamba wao wanaguswa sana na suala hilo kuliko Serikali ya Tanzania.
Hata hivyo, alisema kuwa katika ziara hiyo, ambayo iliwahusisha pia baadhi ya mawaziri, wabunge, viongozi wa polisi, viongozi wa dini na kisiasa, waliahidi kushirikiana kuhakikisha kuwa wanakabiliana na kulimaliza tatizo.
Isitoshe alisema aliwataka viongozi wa vijiji kurejesha ulinzi wa jadi, maarufu kama sungusungu ili kukabiliana na wauaji.
Pinda alisema kuwa serikali ipo tayari kupokea maoni kutoka kwa watu mbalimbali, yanayoweza kusaidia kupata mbinu ya kukomesha kabisa mauaji hayo, ili kuiokoa jamii hiyo ya albino.
Alisema katika kumbukumbu za serikali, hadi mwishoni mwa mwaka jana vikongwe 2,866 walikuwa wameuawa kwa imani potofu kuwa ni wachawi.
Alisema serikali imeliagiza jeshi la polisi kutumia maarifa yake, hata kama itabidi kutumia gharama kubwa, ili kuwatia mbaroni watu wote wanaojihusisha na mauaji hayo.
Wapinzani pia walimtaka Pinda atoe maelezo yanayodaiwa kuwa yalitolewa na Rais Jakaya Kikwete kisiwani Pemba kwamba, aliwashangaa wakazi wa eneo hilo kuwachagua watu ambao hawawezi kuunda serikali na ambao watachukua muda mrefu kupata nafasi hiyo.
Pinda alisema anapata taabu kujibu swali hilo, kwa sababu hawezi kuyatolea maelezo mambo yaliyozungumzwa na bosi wake na wala hajui kama ni kweli rais alisema kama vyombo vya habari vilivyoripoti.
Mbunge wa Konde, Dk Ali Tarab Ali (CUF) alimtaka Pinda aeleze kama kitendo cha Rais Kikwete kutumia magari ya serikali kisiwani Pemba na kuonekana akifanya shughuli za chama ni matumizi mabaya ya fedha za serikali.
Pinda alimjibu akisema kuwa, ni vigumu rais kutofautisha vyombo vya usafiri anavyovitumia wakati akifanya ziara za kisiasa ama za kiserikali na kutoa mfano kwamba, hata rais wa Marekani hutumia ndege aina ya Air Force one bila kuchagua kuwa ni shughuli ya kisiasa au kiserikali.
Wakati hayo yakitokea bungeni, baadhi ya viongozi wa dini nchini, wamemtaka Waziri Pinda kukiri kosa, kufuta kauli yake na kuomba radhi kwa mamlaka za kisheria, Bunge na Wananchi.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislaam, Sheikh Ramadhan Sanze alisema Pinda alifanya kosa la kiufundi kwa kuwa yeye ni mtendaji mkuu wa serikali, hivyo hakupaswa kusema jambo linalopingana na msimamo wa serikali, sheria na katiba ya nchi.
"Kwa vile kauli hiyo haijaleta madhara mpaka sasa Waziri Mkuu ana uchochoro wa kupita ili kujisafisha. Cha msingi ni kukiri kosa, kufuta kauli yake na kuomba radhi kwa mamlaka za kisheria, Bunge na Wananchi" alishauri Sheikh Sanze.
Alisema, hajafuatilia vizuri kuhusu hoja za kambi ya upinzani bungeni na kwamba, kujiuzulu inaweza isiwe suluhisho la tatizo hilo kwa kuwa, hata kama atajiuzulu kauli haitafutika na tatizo litabaki palepale.
"Nchi hii haina dini na kwa hiyo haingozwi na sheria za dini bali inaongozwa na sheria za nchi, kwa hiyo Pinda alipaswa kuangalia sheria ya nchi kwanza kabla ya kutoa agizo lake," alisema Sheikh Sanze.
Alifafanua kuwa, Waziri Pinda ametengeneza mazingira ya uchafuzi na uchochezi, kutokana na kauli yake hiyo kwani baadhi ya watu wanaweza kuitumia vibaya kwa kumuua mtu kwa sababu ya chuki tu baina yao.
Alisema, athari ya kauli kama hizo zinaweza kusababisha migogoro kati ya dini na dini nyingine, kabila moja na jingine au dhehebu moja na jingine kama wananchi watautumia wito huo.
Alisema vita dhidi ya mauaji ya albino imekuwa ikitumika kisiasa zaidi kuliko kitaalamu na kuongeza kuwa, mamlaka husika ziliangalie tatizo hilo kitaalamu badala ya kuliacha likitumika kisiasa.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Valentino Mokiwa alisema kauli ya Pinda ya kutaka aliyeua albino auawe si sahihi kwa sababu mtu akimuua aliyeua ni muuaji na ana kosa kisheria.
Mauaji ya albino yamekuwa yakitikisa nchi na hasa katika eneo la Kanda ya Ziwa, licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na serikali kupitia jeshi la polisi, mashirika ya kutetea haki za binadamu, vyama vya walemavu na watu binafsi.
Source:Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Sijuwi hapa mwelekeo ni upi. Mwizi akikutwa anaiba huwa anaadhibiwa na wengi tunashuhudia wakifa papo hapo. Hili lilishapitishwa na katiba? Sasa kama halipo kwenye katiba lakini linafanyika; Je, Katiba ni Ipi - YANAYOFANYIKA? au YALIYOANDIKWA KWENYE MAKARATASI?

Kama mwizi wa simu akikamatwa anapigwa hadi anakufa hapo hapo, Iweje leo MUUAJI WABINAADAMU eti katiba inamlinda? IMEKUWAJE WATANZANIA WOTE WANAKAA UPANDE WA WAHALIFU.....NI KWELI WATZ WAMEAMUWA KUTETEA WAHALIFU KULIKO WATU WEMA?

AMANI HUWAENDEA WATENDAO AMANI, IWEJE WAUAJI WAPEWE AMANI? Je, NI haki gani wanatendewa wanaouawa kitakitili namna hii?
Au ni kwa kudanganyana kwamba Marehemu hana Haki?

Sheria Mbovu haziwezi kumaliza uhalifu. Nchi inahitaji sheria na amri zenye kuleta adhabu kwa wakosaji. Hivi ndivyo uovu utakavyoondoka nchini. Ni kweli Injili itaondoa uovu. LAKINI KAMA WATU HAWATAKI KUOKOKA MTAWALAZIMISHA?

HIYO KATIBA WANAYOITETEA WABUNGE INASEMAJE MTU AKIUWA AFANYWEJE?

HAO WANALIOKAMATWA NA KUKIRI KWAMBA WAMEUWA WAMECHUKULIWA HATUA HIYO YA KATIBA?.....AU UCHUNGUZI UNAENDELEA? Huu uchunguzi wa kuchunguza wakati mtuhumiwa ameshakiri kutenda kosa, nini kinachunguzwa tena?

Hivi ni kweli Tanzania inachukia uovu?

Au kwa sababu Hakuna aliye MSAFI ili aanze kumpiga mawe muuaji wa albino?

Ooh! Tanzania.......

Anonymous said...

Hakika ni jambo la kusikitisha sana ndugu zetu wanakufa kikatili sana,Bwana yesu tunaomba msaada wako,hata waziri wetu analia kwa sababu ya ndugu wanaokufa kikatili.hakika yesu tunahitaji msaada wako bila wewe uovu utazidi,tuma watenda kazi wengine.