Friday, September 4, 2009

Bifu mpya ya Kakobe vs Pengo

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe, amewacharukia viongozi wenzake wa dini akipinga uamuzi wao wa kuandika nyaraka, ilani na mwongozo. Ameiomba pia serikali iitishe mkutano wa pamoja na viongozi wote wa dini nchini, kujadili hatima ya nyaraka na miongozo waliyoitoa na kuwakemea.
Akinukuu maneno ya Biblia ya 2Timotheo 2:1-3 unaotaka watu watii mamlaka ya nchi kwa kuwa yanatoka kwa Mungu, amesema baadhi ya viongozi wa dini ni wababe hasa kutokana na kitendo cha hivi karibuni cha kiongozi mwenye cheo na dhamana kubwa nchini, kuisema vibaya serikali mbele ya Rais, jambo linaloashiria utovu wa nidhamu, ubabe na kujiamini.
Ingawa hakumtaja jina, lakini hivi karibuni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo mbele ya Rais Jakaya Kikwete, katika maziko ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayala, alisema serikali inaelekea kubaya kwa kuzitaka taasisi za dini kupeleka nyaraka zake kuchunguzwa, kabla ya kuwafikia waumini na kusema Kanisa haliko tayari kulitekeleza hilo, kwani kufanya hivyo ni kuingilia kazi za kichungaji.
Kakobe alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, kuhusu Waraka na Ilani ya Kanisa Katoliki pamoja na Mwongozo wa Shura ya Maimamu wa Kiislamu, vilivyotolewa hivi karibuni na kuzua mijadala katika jamii. Askofu huyo ambaye mwaka 2000 alijiingiza katika siasa kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea wa TLP, Augustine Mrema na jana kukiri kuwa ‘alichemka’ kufanya hivyo, alisema si kazi ya viongozi wa dini kutoa nyaraka na miongozo yenye mwelekeo wa kisiasa.
Alisema kufanya hivyo ni kudhihirisha udhaifu wa wazi kuwa wameshindwa kuhubiri kulingana na imani zao, ili mafisadi wabadilike, maana wapo katika makanisa na misikiti yao pia. “Viongozi wa dini (yeye akijitoa katika hilo) ndiyo chanzo kikuu cha ufisadi katika nchi hii, wanaotajwa katika ufisadi ni waumini wao, wajiulize wamefanya nini kukemea na kufanya waumini wao wasiwe mafisadi,” alisema Kakobe ambaye alilisifu kanisa lake kuwa halina mafisadi na wakiingia katika kanisa hilo basi watakiona cha moto.
Alisema serikali inapaswa kukemea vikali nyaraka hizo, tena bila kuchelewa, kwa kuwa wasiwasi wake ni kwamba bila kujua, viongozi hao wanaweza kuwa wanatumiwa na mataifa tajiri yenye kutengeneza silaha, kuibua vurugu zitakazosababisha vita ili wauze silaha na hatua hiyo inachochewa na wanasiasa wanaoshabikia nyaraka hizo.
Kakobe ambaye alimsifu Rais Jakaya Kikwete kuwa ni mpole, alisema upole huo umekithiri na haupaswi kuwa katika suala lolote lenye kuhatarisha amani ya nchi kama hilo na kumtaka yeye (Kikwete) na marais wastaafu waliopita, kutoa kauli kuhusu suala hilo na waepuke kufanya kazi kwa kumfurahisha kila mtu. “Waasisi wetu (akimtaja Nyerere) walitutengenezea mazingira mazuri sana hadi kuitwa kisiwa cha amani, kuna watu wanataka kuliharibu hilo, hivi sasa nchi majirani zetu zilizokuwa na vita, zinaanza kurejesha amani, sisi hatujui vita, ndiyo maana wanataka tuanze kupigana, tukiruhusu vita, Watanzania tutakufa kama panzi,” alisema.

Source: Habarileo

No comments: