Monday, December 21, 2009

UMEJIANDAA KUINGIA MWAKA 2010?

Bwana Yesu asifiwe!
Ninamshukuru Mungu kwa kuwa kwetu sisi "Yeye ni mwema na fadhili zake zadumu hata milele (Zab 106:1). Tumeuanza mwaka 2009, wengine waliishia njiani lakini sisi tumefika hapa na kwa mapenzi yake tutasonga mbele. Tunajua wazi kuwa hakuna jema tulilofanya ambalo ndilo linampa Mungu sababu ya kuendelea kutuweka hai, NI NEEMA yake na MAKUSUDI yake kwetu, na tuseme wote "Asante Baba Mungu"
Katika ratiba ambayo niliitoa hapo awali (kwa waliokuwa wamejiunga hadi mwezi wa saba) ya kutuongoza kusoma Agano Jipya lote ndani ya 2009, ratiba yetu ilionesha kuwa tungemaliza kusoma tarehe 6 December. Na ratiba inaonesha kuwa sasa ni wakati wa kujiandaa kwenda mwaka 2010.
Sote tunafahamu kuwa ukiingia kwenye jambo wakati hujajiandaa kuingia katika jambo hilo, unaweza usifanye vyema katika jambo hili kama uwezo Mungu aliokupa nao, kwa sababu hakuna malengo uliyojiwekea, na Biblia imesema wazi kuwa "Pasipo maono(mipango,mikakati,malengo) watu huacha kujizuia. Mfano rahisi ni pale mtu atakapopata hela nyingi wakati hajajiandaa kuzitumia hizo pesa, atatumia hizo pesa kwa namna anavyofikiri ni vyema, lakini zikiisha ndiyo atagundua kuwa hakutoa hata fungu la kumi na hakufanya mambo mengi ambayo ni ya msingi kuliko aliyoyafanya. Nini tatizo? Hakuweka malengo kabla.
Tunapoelekea kuingia mwaka 2010 kwa neema za Mungu. Ni muhimu sana uanze kumwomba Mungu ("Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana akiomba kwa bidii") kwa ajili ya mwaka ujao. Mungu anakupenda sana, na ukimwomba ataweka moyoni mwako mambo mengi sana kuhusu mwaka ujao, hadi utashangaa.
Hatua ya kwanza, mshukuru Mungu kwa mwaka 2009, unajua mambo Mungu aliyokufanyia, hivyo mshukuru sana.
Ni mambo gani ulipanga kuyafanya 2009 na hukufanikiwa, au umefanikiwa kwa sehemu tuu? Tafakari kilichokufanya usifanikiwe kama ulivyotamani na ujifuze somo hapo kuhusu mipango ya mwaka ujao.
Weka Mipango yako:
Kisha anza kumwomba akupe mwongozo kuhusu mwaka 2010, muulize habari za huo mwaka. Muulize katika maombi, anataka ufanye kipi na vipi kwa mwaka huo? Kumbuka Mungu huwa anajibu maombi ya watu wake, ukiwemo wewe.
Kisha baada ya hapo, anza kusikiliza moyoni mwako Mungu amekuwekea mawazo gani kuhusu 2010. Kisha, soma Habakuki 2:2-3 "Iandike ndoto hiyo..."
Ili kurahisisha maendeleo yako ndani ya 2010, ni vyema ukajipangia mambo gani unayotaka kuyatimiza kwa mwaka huo mzima. Hii itakusaidia sana katika utekelezaji na pia namna ya kumwomba Mungu.
Chukua kalamu na karatasi (kama una familia ni vyema kushirikiana na mwenzi wako) na uanze kuandika mipango yako kwa mwaka mzima wa 2010, andika yote ambayo unaona Mungu ameweka moyoni mwako na unatamani kuyatimiza kwa kipindi cha 2010. Andika yote.
Kisha, muombe Mungu na ufikiri, mipango uliyojiwekea inahitaji ufanye nini ili kuifikia? (what strategies?) Mipango mingine inaweza ikakulazimu kubadilisha namna unavyoishi maisha yako (lifesyles), mingine inaweza ikakulazimu kubadilisha ratiba zako, mingina itakulazimu uanze kuweka akiba ya fedha ili kuitimiza. Kwa kila mpango ulioandika, andika utafanya nini ili kuutimiza.
Omba Neno la kukuongoza 2010
Hili ni eneo lingine ambalo nakusihi usipuuzie kabisa. Biblia inasema "Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia zangu"- Zaburi 119:105. Ni muhimu sana, mwombe Mungu pia akupe mstari wa Biblia wa kukuongoza kwa mwaka mzima wa 2010. Ninamshukuru Mungu kuna ndugu mmoja ameniandikia na kunieleza kuwa ameshamwomba Mungu na Mungu ameshampa mstari wa kumwongoza yeye na familia yake kwa mwaka mzima wa 2010. Mwombe Mungu akupe Neno hilo, na utakapokaa na kutafakari, Roho Mtakatifu atauleta huo mstari ndani ya moyo wako, inawezekana ni mstari ambao unaufahamu lakini utaona tuu kuwa huo mstari fulani unakujiajia sana mawazoni mwako, huyo ni Roho Mtakatifu anakuletea hilo Neno (na siyo mawazo yako tuu!). Ukishapewa mstari huo, utafakari kwa kina na utakusaidia kujua Mungu anataka uishi vipi na ufanye nini kwa mwaka ujao, sawa?
Siku ya Kuaga na kupokea mwaka.
Hii ni siku maalumu kwako. Tumia siku hizi kumshukuru Mungu na kumwomba Mungu kuhusu 2010. Mweleze Yeye mikakati yako yote uliyoipanga na umwombe akufanikishe katika hiyo. Omba kama Mungu atakavyokuongoza. Katika mkesha wa mwaka mpya nia muhimu ukitumia wakati huo kumweleza Mungu mambo hayo yote,(pamoja na familia yako kama unayo), imba nyimbo za sifa, tenzi za rohoni na mwombe Mungu.
Toa Sadaka yako
Unapomweleza Mungu haja yako kwa mwaka 2010, ni vyema kuambatanisha sadaka na maombi yako hayo. Andaa sadaka yako kuanzia sasa, kiasi chochote Roho wa Mungu atakachokuongoza, iweke kwenye bahasha na kuanzia sasa, kila umwombapo Mungu kuhusu 2010 uwe na sadaka yako mkononi, fanya hivyo hadi ile siku ya mwaka mpya, na kisha ipeleke hiyo sadaka yako mahali popote Roho Mtakatifu atakapokuongoza, kwa mfano kanisani kwako.
Ni matumaini yangu kuwa mipango yako itakuwa sawasawa na Neno la Mungu na kwamba itamweka Mungu mbele daima.
"Ninakutakia baraka tele za Mungu, furaha, raha, mafanikio na afya njema katika mwaka 2010. Mungu akubariki na kukutunza, akuangazie nuru ya uso wake na akupe neema yake na kukupa amani kwa mwaka mzima wa 2010, Amen"
Tuombe...
"Mungu Baba, ninakuja mbele zako saa hii kwa Damu ya Yesu Kristo. Ninakiri kuwa mimi ni mkosaji na ninaomba unisamehe na kunitakasa nafsi,mwili na roho yangu kwa Damu ya Mwana wako mpendwa, Yesu Kristo. Mungu ninakushukuru kwa kuwa nami na kunilinda kwa mwaka mzima wa 2009. Asante kwa kuniepusha na mambo mabaya na kunipatia mema tele. Baba ninakuomba uniongoze ninapoingia mwaka 2010, ninaomba unipe Neno la kuniongoza kwa mwaka mzima. Ninaomba uniambie ni mambo gani unataka niyafanye kwa mwaka 2010 na unipe mikakati ya kuyatimiza yote kwa wakati. Ninaomba uibariki huduma hii ya Neno lako, na mtumishi wako, umbariki na kumpa afya njema, hekima, maarifa na bidii nyingi, ili kwa mwaka ujao, mapenzi yako yatimizwe zaidi na zaidi. Nimeomba haya yote na kuamini kwa Jina la Yesu Kristo, Amen."
Katika mwaka 2010,"Utafute kwanza Ufalme wake, na haki yake na hayo (mambo mengine) yote utazidishiwa" Mathayo 6:33.
Happy and Blessed New 2010 Year!
Ili Kristo apendwe;Frank Lemasavedlema2@yahoo.comwww.lema.or.tzDecember 18th, 2009.

No comments: