Thursday, October 25, 2007

Waislamu wamjia juu Mchungaji Mtikila

Kamati ya Kuokoa Mali za Waislamu Tanzania, imetoa siku tano kwa Kiongozi wa Kanisa la Wokovu Kamili, Mchungaji Christopher Mtikila kuwaomba radhi Waislamu kwa kuidhalilisha, kuitusi na kuikejeli dini yao. Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa kamati hiyo, Sheikh Khalifa Khamis alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Sheikh Khalifa alisema iwapo Mchungaji Mtikila atashindwa kuwaomba radhi watajua nini cha kumfanyia. Aidha wamemtaka Mchungaji Mtikila kutamka hadharani kuwa Uislamu si dini ya kigaidi wala si ya kinyama, na badala yake ni dini ya amani na mapenzi kwa wanadamu wote. ``Tunamtaka Mchungaji Mtikila hadi kufikia Ijumaa ijayo, awe ametekeleza masharti yetu, asipofanya hivyo tutajua cha kumfanyia,`` alisema. Aliongeza kuwa, pamoja na hayo, kamati hiyo imeviomba vyombo vya dola kumchukulia hatua za kisheria Mchungaji Mtikila kwa matamshi yake ya kuudhalilisha Uislamu. Mchungaji Mtikila amefungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kupinga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi. Kwa mujibu wa kamati hiyo, sababu anazotoa Mchungaji Mtikila ni kuwa ameamua kufungua kesi hiyo ili kupinga ugaidi yaani Uislamu kwa kuwa Tanzania si nchi ya Kiislamu. Pia kuanzishwa kwa mahakama hiyo alisema kutaleta matabaka, kuchochea ugaidi, kuleta vurugu na kuharibu utawala wa kisheria au kuwagawa watu katika misingi ya kidini. ``Nchi yetu ni ya amani, tunaishi kwa kuheshimiana na kushirikiana katika shughuli zote za kijamii kama misiba, ndoa bila kubaguana,`` alisema. Aliongeza kuwa, endepo serikali itakaa kimya na kumwacha Mtikila kuendeleza matusi na kebehi dhidi ya Waislamu, serikali itabeba dhamana ya matokeo ya uchochezi huo. ``Tunayo mifano mingi ya Waislamu kubambikizwa kesi kuwa wamekashifu dini ya Kikristo, japo mashtaka wanayosomewa ni dhahiri yanatokana na misingi ya imani yao,`` alisema. Aliongeza kuwa, ili kulinda amani na utulivu ambao umedumu kwa muda mrefu, kamati hiyo haitaielewa Serikali endapo haitachukua hatua yo yote dhidi ya Mchungaji Mtikila. Sheikh Khalifa alisema Uislamu siyo dini ya kigaidi kama ambavyo Mchungaji Mtikila amedai katika kupinga kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi. ``Maaskofu wameshapinga kuanzishwa kwa kadhi lakini hawajatoa matamshi ya kashfa na kejeli kama ya Mtikila,`` alisema. Aliongeza ``Lakini tunashangaa kuona makanisa yanataka kujiweka katika nafasi ya kuamua hatma na maslahi ya umma wa Waislamu kana kwamba wao ndiyo raia bora wenye haki ya kutuamulia wengine kile kisichostahili.

No comments: