MAMIMIA ya wananchi wamekimbia nyumba zao maeneo ya Mbagala Kuu kwa miguu hadi Tuangoma Kongowe umbali wa kilomita tatu na nusu katika Manispaa ya Temeke, kufuatia milipuko ya mabomu iliyotokea jana katika kambi ya JWTZ, iliyo Mbagala.
Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa wananchi hao, Mohamed Said alisema hali ni mbaya watu wamefadhaika na nyumba kadhaa zimeharibiwa na wengi wao wapotezana na familia zao.
“Mimi nimepotezana na watoto wangu na baadhi ya ndugu zangu sijui waliko,” alisema.
Walipoulizwa kwamba sasa wanaelekea wapi, walisema wanakwenda kujihifadhi kwa ndugu zao wanaoishi maeneo ya Tuangoma.
Wakati huhuo, moja ya bomu lililoruka kutoka katika kambi hiyo liliangukia eneo hilo la Tuangoma na kuleta taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.
Baadhi ya watu kutoka Mbagala na maeneo mengine, walionekana wakimbilia Kitunda, Gongo la Mboto, Chanika na Mkuranga kwenda kujihifadhi wa ndugu zao na wote walikuwa wakitembea kwa miguu ili kuokoa maisha yao.
Athari za mabomu pia zililikumba eneo la Tandika Mikoroshini ambako baadhi ya vipande vya mabomu viliangukia katikati ya makazi ya watu.
Wakizungumza na Mwananchi wakazi wa maeneo hayo wanasema vipande vya bomu hilo vilidondoka eneo hilo kwa kishindo kikubwa na kufuatiwa na moto ambao hata hivyo haukuzifikia nyumba zao.
Mkazi mmoja wa Tandika, Asha Jumanne alisema kabla bomu hilo kutua mahali hapo, alilishuhudia likipita angani wakati akianika nguo za mwanae, hivyo kumfanya aache shughuli zake na kukimbia ili kuokoa maisha yake na kuwaacha watoto wake waliokuwa wamelala ndani.
Katika maeneo ya Kiwalani hali ilikuwa mbaya, baada ya mtikisiko wa bomu ulipofumua paa la kibanda ambamo vijana kadhaa walikuwa wanaangalia filamu ya kutisha ya ‘Predator’ ya Arnord Schwarzenegar.
No comments:
Post a Comment