Friday, February 19, 2010

Waumini wa Kakobe wacharuka

WAUMINI wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) jana waliwazuia watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuweka nguzo zenye msongo mkubwa wa kilovolti 132 karibu na kanisa hilo tukio ambalo nusura lizue vurugu, lakini Polisi wakawahi eneo hilo na kutuliza hali hiyo.
Tukio hilo lilitokea saa tano asubuhi baada ya wafanyakazi wanaosadikiwa kuwa ni watumishi wa Tanesco kwenda eneo hilo na gari lenye namba za usajili T346 ARR kwa lengo la kusimika nguzo hizo, lakini hata hivyo walikutana na upinzani mkubwa kutoka kwa waumini hao.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema walivyofika walisimamisha gari eneo hilo tayari kuanza kazi, lakini hata hivyo waumini wa kanisa hilo ambao wanapeana zamu za kulinda kanisa hilo, waliwazuia wasifanye lolote. Jana kulikuwa na waumini takribani 200 ambao walikuwa zamu ya asubuhi.
Kiongozi wa kanisa hilo, Askofu Zacharia Kakobe alikiri waumini wake kuwazuia wafanyakazi wa Tanesco kusimika nguzo hizo kwa maelezo kuwa bado mazungumzo kati yake na wadau wengine ikiwemo serikali yanaendelea hivyo haoni haja kwa nini zitumike nguvu kuweka nguzo hizo. “Nimeambiwa na wizara nipeleke maoni yangu na mwisho ilikuwa jana, iweje hawa leo waje kuweka nguzo wakati hakuna tangazo lolote la serikali? Alihoji Kakobe na kueleza kuwa yawezekana kuna watu ambao wanania ya kuchochea vurugu kwa lengo la kuipaka matope serikali. Askofu huyo alisema baada ya vuta nikuvute baina ya watumishi hao na Tanesco, polisi walifika wakiwa kwenye magari tayari kwa ajili ya kutuliza ghasia, lakini gari hilo la Tanesco liliondolewa na watumishi hao. Polisi walifika eneo hilo wakiwa kwenye magari matatu tayari kutuliza ghasia hizo kutokana na waumini wa kanisa hilo kuapa kwamba nguzo hizo haziwezi kuwekwa hapo kwa sababu ya zina madhara kwa afya zao na kwa vyombo vya mawasiliano vya kanisa hilo ikiwemo kituo cha televisheni ambacho wako mbioni kukianzisha. Polisi walipofika eneo hilo na mafundi hao kuondoa gari kwa kasi na kuondoka, kiongozi wao ambaye jina lake halikupatikana alisema angefuatilia kuona sababu ya mafundi hao wa Tanesco kuondoka eneo hilo.
Meneja Mawasiliano wa Tanesco Badra Masoud, alikiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini akasema waliozuiwa kufanya kazi ni kampuni iliyoajiriwa na Tanesco kusimika nguzo hizo ijuliakanyo kama Takawoka. “Wale waliozuiwa sio Tanesco ni kampuni tuliyoiajiri kusaidiana na sisi kuweka nguzo zile, pale walienda kwa ajili ya kusafisha na kufanya maandalizi ya kuweka nguzo,” alisema Masoud na kukanusha kuwa watu hao walienda hapo kuweka nguvu. “Lile eneo mimi silizungumziii kabisa kwa sasa, lakini kazi yetu ya kuweka nguzo inaendelea huku Kijitonyama kwani hakuna malalamiko kama pale, lakini pia nikuhakikishie kuwa uwekaji wa nguzo uko maeneo mengine na sio pale,” alisema Badra.
Source: habari leo

2 comments:

Unknown said...

Askofu kakobe,ilitakiwa uongoze kanisa kufunga na kuomba juu ya suala la tanesco na serikali,Mungu wetu tunae mwabudu anajibu.Na sio kupigana kwa nyama

Unknown said...

Askofu kakobe,ilitakiwa uongoze kanisa kufunga na kuomba juu ya suala la tanesco na serikali,Mungu wetu tunae mwabudu anajibu.Na sio kupigana kwa nyama