Friday, February 19, 2010

Waumini wa Kakobe watimua wahandisi wa Tanesco

Mgogoro kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na waumini wa Kanisa la Full Gospel Fellowship kuhusu kupitisha njia ya umeme wa msongo wa Kilovoti 132 mbele ya kanisa hilo, umechukua sura mpya, baada ya waumini hao kuwatimua wahandisi wa shirika hilo waliokwenda kufanya tafiti.
Tukio hilo lilitokea jana saa 6:30 mchana, baada ya wahandisi hao wakifuatana na polisi kufika eneo la kanisa hilo lililopo Mwenge kwa ajili ya kuanza utafiti kuhusu athari zitakazotokea umeme huo utakapopitishwa.
Mratibu wa Mgogoro huo kwa upande wa kanisa hilo, Emmanuel John, alisema watu hao ambao walijitambulisha kuwa wanatoka Kampuni ya Dico na Tanesco walifika eneo hilo na kueleza kuwa walikwenda kwa ajili ya kufanya utafiti wa athari zitakazopatikana kwa binadamu, jengo na vifaa vya kanisa hilo.
Alisema, kabla ya tukio hilo, juzi walipokea fax kutoka Wizara ya Nishati na Madini ikiwataarifu kuwa itatuma jopo la wahandisi kwenda kufanya utafiti, lakini haikueleza siku na saa ambayo watu hao watafika.
Alisema mtafaruku uliibuka baada ya waumini kuwaarifu wahandisi hao kwamba hawawezi kuwaruhusu kufanya kazi hiyo bila kuwepo kwa Askofu Kakobe, kwani muda huo hakuwepo.
"Waumini walipinga kufanya kazi hiyo ikiwa Askofu Mkuu hayupo, lakini wenzetu walikuwa wabishi wakataka kuenndelea na kazi zao kitu ambacho kilileta mvutano mkali," alisema.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, waliamua kumpigia simu Askofu Kakobe ili wajadiliane na watu hao, ambapo baada ya majadiliano hayo iliamuriwa wahandisi hao warudi walipotoka na kazi hiyo ifanyike leo wakati askofu huyo akiwepo.
Mgogoro huo unaodumu kwa miezi miwili sasa umesababisha waumini wa kanisa hilo kuanzisha ulinzi nje ya kanisa kupinga hatua yoyote ya Tanesco kutekeleza mradi huo.
Source: Nipashe

No comments: