Mchungaji wa Kanisa la Gospel Revival Assemblies of God, lililopo Kiluvya Madukani, Jijini Dar es Salaam, Yusuph Abdalah, anasakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumpachika mimba mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Kiluvya.
Akizungumza na Mwandishi wetu hivi karibuni, mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Mary Mdoe alisema kuwa, yeye pamoja na familia yake, wote walikuwa wakiabudu kwa mchungaji Yusuph na alikuwa mmoja wa wazee wa kanisa hilo.
Kufuatia familia hiyo kuabudu kanisani hapo, mchungaji huyo alianza kufanya mazoea ya kutembelea familia hiyo ambapo hakuna aliyewahi kumtilia shaka kama anaweza ‘kutafuna kondoo’ anaowachunga.
Mama wa mtoto huyo alidai kuwa siku za hivi karibu alimshtukia binti yake akiwa katika hali iliyomtia wasiwasi hivyo ilimbidi akanunue kipimo maalum cha ujauzito.
“Baada ya kumpima nilibaini kuwa mwanangu ni mjamzito, nikampeleka tena kupimwa kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Tumbi Kibaha, Pwani ambapo alithibitika kuwa na ujauzito ndipo nilipombana amtaje aliyembaka na kumpachika mimba aliyempachika,” alisema mama huyo.
Bi. Mdoe alisema alipigwa na butwaa baada ya binti yake kumtaja Mchungaji Yusuph ambaye ni kiongozi katika kanisa lao.
Kufuatia taarifa hizo, Bi. Mdoe na mumewe Oswald Mdoe walikimbilia Kituo cha Polisi cha Kibaha Maili Moja kutoa taarifa ambapo polisi wa kituo hicho walimfuata mchungaji huyo na ‘difenda’ lakini walikuta tayari ameshauza mabenchi ya kanisa hilo na kutorokea kusikojulikana.
“Baada ya kukuta mchungaji ametoroka, polisi hao walimkamata mkewe Grace Yusuph, na kumtia kwenye difenda kisha kumpeleka Kituo cha Polisi cha Tumbi kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo,” alidai mama huyo.
Aliongeza kuwa, polisi baada ya kumfanyia mahojiano mke wa mchungaji huyo, walifungua kesi kituoni hapo kwa jalada namba AMM/RB/2152/2010.
Mama mzazi wa mtoto huyo alidai kuwa, alimpigia simu mchungaji huyo na kumlaumu kwa jambo alilofanya lakini aliomba msamaha kwa yaliyotokea na kudai ni ibilisi alimpitia na haikuwa nia yake.
Hata hivyo habari zimasema kuwa waumini wa kanisa hilo walisikitishwa sana na kitendo hicho na wengine kuangua vilio.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Absalom Mwakyoma, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema analivalia njuga ili sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment