KAKOBE AKUMBUKE ALIPOANGUKIA, ATUBU-MCHUNGAJI
SWALI: Katika mahojiano ambayo sehemu yake
imechapishwa katika gazeti la Nyakati la
Jumapili tarehe 14/7/2013 ulionesha kutokubaliana na hoja kwamba mwenendo wa
huduma ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary
Kakobe ni matokeo ya unabii uliotolewa na Mchungaji Antony Lusekelo wa Kanisa
la GRC Kibangu, Dar es Salaam. Kwanza hebu waambie wasomaji tangu mwaka gani
ulikuwa mchungaji katika kanisa la FGBF na uliondoka mwaka gani?
JIBU: Mimi niliwekewa mikono na Askofu Kakobe, na kuwa
mchungaji tangu tarehe 3-3-1996 na nimekuwa katika utumishi muda wote hadi
mnamo mwaka 2010.
SWALI: Ni muda wa
kutosha. Katika muda huo wote kihuduma ulikuwa karibu kiasi gani na Askofu
Kakobe?
JIBU: Ukaribu wangu na Askofu Kakobe ulikuwa katika huduma, na zaidi sana yeye ndiye
aliyekuwa mzazi na mlezi wangu kiroho, ndio ukaribu wangu na yeye kwa zaidi ya
miaka 19.
SWALI: Kwa
mtazamo wako kuna tofauti yoyote baina ya Kakobe wa wakati ule wewe ukiwa FGBF
na Kakobe wa sasa?
JIBU: Kama nimelielewa swali lako, nadhani unasema je, Kakaobe wa sasa na alivyo kuwa zamani, ukweli
ni kwamba, Askofu Kakobe alivyo sasa sivyo alivyokuwa miaka ya nyuma, zamani
alizingatia sana Neno la Mungu na kuishi katika mapenzi ya Mungu, na ndio
sababu Watanzania na Dunia kwa ujumla ilishuhudia uwepo wa Mungu juu yake, kama
vile ishara maajabu na miujiza, leo hii, neema hiyo kwake imepotea! Amepoteza
mwelekeo na kubaki na jina tu la uaskofu lakini kibali cha Mungu hakipo juu
yake. Na hii inatokana kupenda pesa zaidi na kupenda sifa au kutafuta utukufu.
SWALI: Turudi
kwenye msingi wa mahojiano haya. Unaamini kwamba huduma ya Askofu Kakobe
imeshuka? Unatumia vigezo gani kubaki na mtazamo huo?
JIBU: Ndio naamini kwamba huduma yake imeshuka,
kwanza kulikuwa hakuna huduma inayoleta watu wengi kwa Yesu kama huduma ya
Kakobe, leo hii imekuwa kinyume, watu wengi wanaondoka katika huduma yake na
kwenda duniani au kwenye mafundisho manyonge. Pia zamani ulikuwa ukipita
mitaani na sehemu mbalimbali hapa nchini, Kakobe alikuwa ni mtu wa kuheshimiwa,
leo ni mtu anayedharauliwa sana na watu, huko ni kushuka kwa huduma! Majuzi
hapa alikuwa amekwenda Canada, na siku anaondoka, alisema anakwenda kuwahubiri
maelfu ya watu, na akasema sababu mojawapo ya kuanza kwenda kuhubiri huko ni
kwavile watanzania wameikataa kweli na wazungu wanaitaka kweli inayo hubiriwa
na yeye. Ndugu mwandishi, ili ujue kwamba huduma yake inaelekea ukingoni,
fuatilia mkutano wake huko, hakupata matokeo aliyotarajia, na ameshindwa hata
kuonyesha picha za matukio ya mkutano wake kwenye ibada ya Jumapili iliyopita!
Mungu si wa mchezo anaweza kukupandisha na anaweza kukushusha!
SWALI: Hivi wewe
kama mchungaji huwezi kuamini kwamba pamoja na idadi ya watu au waumini kuzidi
kushuka FGBC Mwenge, mikutano yake (kama huo wa Toronto, Kanada) kutokuwa na
mahudhurio makubwa, lakini watu wengi wanaweza wakaendelea kuokoka na
kujikabidhi mikononi mwa Yesu Kristo kutokana na kusoma machapisho yake au
kutazama video za huduma yake zilizorekodiwa siku za nyuma? Ni lazima huduma ya
Kakobe ifanyiwe tathimini kupitia tu mikutano na mahudhurio ya watu kanisani?
JIBU: Ni
kweli kwamba Askofu Kakobe anayo machapisho ya mafundisho yake kwenye video na
kaseti za sauti na machapisho ya mafundisho kwa njia ya maandishi. Ndugu yangu,
mtu anapokosa kibali kwa Mungu, hata mafundisho yake mazuri yanakuwa kama si
kitu mbele za watu, mvuto na kiu ya yale mafundisho yake, ilitokana na kibali
alichokuwanacho kwa Mungu.
SWALI: Wanadamu
wanasema huduma ya Askofu Kakobe imeshuka, wengine wanaongeza wanasema imeshuka sana. Haohao wanadamu
wengine wanadai ni unabii wa akina Lusekelo waliomtabiria kuwa atadondoka
alipowashambulia kwa kuruhusu waumini wanawake kuvaa suruali zenye kubana
matako na nywele za bandia, maarufu kama ‘mawigi’ makanisani. Wewe umesema huna
imani na unabii huo, badala yake unasema kuna mambo ambayo Kakobe ameyafanya,
Mungu amemkasirikia na anapaswa afanye toba. Ni mambo gani hayo?
JIBU: Jambo ambalo naweza kusema hapa ni kwamba,
Kakobe kilicho mfikisha hapo, ni kiburi, Biblia inasema, kijapo kiburi ndipo
ijapo aibu, Kakobe amekuwa na kiburi cha juu sana, kwa mfano yeye h ujiona kuwa
ndiye mwalimu na mtumishi mwenye mafundisho mazuri kuliko wengine wote, pili
kuna wakati alisema yeye amefanya kazi kubwa kuliko Askofu Kulola, na hii
aliisema sio kwetu tu wachungaji wake au kanisani, aliyanena hayo kwenye vyombo
vya habari (tv) wakati ule alipomaliza kuyatembelea makanisa ya FGBF kote
nchini. Huoni kama hicho ni kiburi cha hali ya juu sana!! Tatu hivi karibuni
kuna wachungaji wamemshitaki Kakobe mahakamani, lakini watumishi mbalimbali wa
Mungu (maaskofu) waliposikia wakamwendea na kumwambia sio vema kwenda
kumalizana mahakamani na wachungaji wako, tunaomba tukae na wewe na wachungaji
wako tutafute ufumbuzi ( tuwapatanishe), Kakobe alikataa kabisa, je huoni kuwa
hicho ni kiburi? Na sio tu kiburi kwa wale watumishi waliomwendea, ni kiburi
hata kwa Mungu aliyeagiza na anayemtaka kila mtu kupatana na mwenzake! Pia
mambo mengine tunayoweza kusema kuwa ni chanzo cha Kakobe kuwa hivi ni kwamba,
Kakobe amewaumiza watu wengi sana katika maisha yao kiroho na kimwili, leo kuna
watu wameacha wokovu kwasababu ya Kakobe, leo kuna watu wanaishi maisha ya
shida na kutokuwa na chochote
kwasababu ya Kakobe! Leo kuna wachungaji na
waumini wa FGBF wanakosa hata nauli au chakula kwasababu ya Kakobe, leo kuna
watoto wa washirika na wachungaji, wameshindwa kusoma kwasababu ya Kakobe!
Majuzi majuzi hapa nimesikia kutoka kwa mmoja wa watoto wa Kakobe, kuwa baba
yake (Kakobe) kuwa hakwenda kwenye mazishi ya mama yake mzazi huko Kigoma
kijiji cha Kakonko, ndugu mwandishi, je unadhani hayo ni madogo mbele za Mungu?
SWALI: Pengine
wakati msiba unatokea alikuwa kwenye huduma na ataenda kumzika mama yake kama
hilo ni kweli. Sasa hebu waambie wasomaji wa mtandao huu, umekuwa mchungaji
katika huduma ya FGBF kwa miaka yote hiyo, leo ungepata nafasi ya kukutana na
Askofu Kakobe na akawa tayari kukusikiliza kama mtumishi wa Mungu nini
ungemwambia?
JIBU: Mimi
ningemwambia jambo moja muhimu ambalo ni sawa na maandiko, kumbuka ni wapi
ulipoanguka na ukatubu, najua Kakobe anakumbuka mahali alipoanguka, pia
ningemwambia, neno la Mungu linasema, nabii atakapotoa unabii na usitimie, atadharauriwa na watu
wote, alitoa unabii kuwa Mrema atakuwa Rais wa Tanzania mwaka 1995, na haikuwa
hivyo. Awaombe msamaha aliowambia uongo na Mungu atamsamehe na kumpa heshima
kubwa zaidi.
Source: http://www.fungukasasa.blogspot.com/2013/07/kakobe-akumbuke-alipoangukia-atubu.html
1 comment:
Huyu mtoa habari kavamiwa na shetani mzima-mzima, aache kudanganya watu, Kakobe ndo kwanza anazidi kuinuliwa na huduma inazidi kutambulika na kuhitajika Duniani kote
Post a Comment