Monday, December 22, 2008

Umejiandaaje kumalizia mwaka 2008 na kuanza mwaka mpya wa 2009?

Bwana Yesu asifiwe sana!
Ninamshukuru Mungu kwa Neema zake kuu na Upendo wake usio na kipimo kwa nafasi hii aliyotupa ya kujifunza Neno lake la Uzima kwa njia hii. Sifa ni kwake.
Ninamshukuru Mungu Baba kwa kutufikisha tena mwezi huu wa mwisho wa mwaka 2008. Naamini kuwa hata wewe mwenyewe unaona kuwa hii ni Neema kubwa sana. Neema ambayo hatukulipa chochote kupewa, ni zawadi kutoka kwa Baba Mungu kwa upendo wake. Ni wazi kuwa watu wengi sana walifikiri kuwa watafika siku kama hii ya leo lakini leo hawapo hai. Sisi tumefika hapa kwa sababu Baba Mungu ana kazi nasi tena, na ni kwa upendo wake tuu.
Tunapoelekea kuumaliza huu mwaka, ni vizuri tukitafakari pamoja mambo machache.Kwa wale walioweze kutembelea website yangu mwanzoni mwa mwaka huu, niliweka ujumbe maalumu wa "Salamu za mwaka mpya 2008" na nilizungumza kwa Roho Mtakatifu mambo muhimu sana kwa ajili ya mwaka 2008. Miongoni mwa mambo hayo, Roho Mtakatifu alitufundisha kuwa, Tuweke malengo kwa ajili ya mwaka mzima wa 2008, kisha tuweke mikakati ya namna ya kuyatimiza malengo hayo, tuyaombee malengo yetu kwa Mungu, n.k. Tena tuyaandike malengo yetu kwenye karatasi na kuyatunza. Je wewe ulifanya hivyo?
Kama uliweka malengo yako kwa mwaka 2008, sasa tumefikia mwisho wa mwaka, ni wakati sasa wa kukaa chini kwa utulivu na kuanza kuyapitia tena malengo yako, utathmini mafanikio yako.
Unapoyapitia malengo uliyojiwekea, tafakari ni kwa kiasi gani umefanikiwa kutimiza mipango uliyojiwekea ndani ya mwaka huu, ni kwa kiwango gani hujafanikiwa kuyatimiza malengo yako, na umwombe Mungu akuonyeshe ni sababu zipi zimekufanya usiweze kuyatimiza malengo yako. Hii ni muhimu kwani itakusaidia kujua ni mbinu gani uzitumie kufanikiwa mwaka ujao wa 2009.
Tafakari pia baraka na mambo yote mema ambayo Mungu amekukirimia kwa mwaka huu wa 2008. Kwa maneno mengine "HESABU BARAKA ZAKO" Angalia baraka Mungu alizokupa na maneno uliyokuwa unayakiri kuhusu mwaka 2008. Inawezekana umekuwa ukisema kuwa "Ah, mwaka huu siyo mzuri bwana!" Sasa je, ukiangalia Neema Mungu alizokupa, kauli hiyo ni sawa?? Mshukuru Mungu kwa baraka zake zote hizo, hata kama unaziona kuwa chache na ndogo, kumbuka ni Neema hiyo. Tenga muda maalumu kumshukuru Mungu kwa yote.
Tafakari pia mambo ambayo umeyaona kuwa ni mabaya kwa mwaka 2008. Pengine umemlaumu Mungu kwa kuyaacha mambo hayo kukutokea, lakini jiulize, Je, ni makosa ya nani? Wewe mwenyewe unajua kuwa Mungu huwa hafanyi makosa, kwa hiyo ni wazi kuwa inawezekana uzembe wako au kutokuwa makini kumechangia, pamoja na adui yetu shetani kutupinga. Hapo ndipo kunatokea umuhimu wa kutubu kwa kila mwezi wa mwaka 2008, mwombe Mungu akusamehe kwa uzembe wote ulioufanya, naye atakusamehe hakika.
Baada ya mambo hayo, sasa tumia siku zilizobakia kuanza kumwomba Mungu aanze kukuonyesha mambo ya 2009. Sasa anza kuweka tena malengo yako kwa ajili ya mwaka 2009. Panga mikakati ndani ya Kristo ambayo unataka kuitimiza mwaka 2009. Kumbuka namna unavyojiwekea malengo kuna athiri namna utakavyofanikiwa. Usipoweka malengo ni hatari, kwani ukiweka malengo na kuyaandika mahali, hayo malengo yatakuwa yanakuhimiza na kukumbusha kuongeza bidii ili kuyatimiza yote. Ni kama usemavyo msemo wa kiingereza "No man is greater than his vision" Hakikisha unaweka malengo kwa ajili ya mwaka ujao.
Hatua nyingine ni kuweka mikakati, yaani ni namna gani utakavyoweza kuyatimiza malengo hayo uliyojiwekea? Kwa mfano, kama wewe ni mzazi na unataka mwaka unaokuja uwe karibu zaidi na watoto wako ili kuzungumza nao na kuwafundisha mambo mbalimbali, hii ina maana kuwa unatakiwa uwe mwangalifu zaidi kutunza muda, ili upate muda wa kukaa na watoto wako. Weka mikakati.
Kumbuka kumwomba Mungu kwanza kabla ya kufanya tathmini yote hiyo.
Haya ndiyo mambo ambayo siku ya leo nimehimizwa nikushirikishe kwa kipindi hiki cha mwaka. Mungu akipenda hivyo, nitaendelea kukushirikisha zaidi na zaidi kupitia Huduma hii ya Mailing Lists. Kama una maswali au ushauri wowote tunavyoelekea mwisho wa mwaka, karibu.
Tuendelee kuombeana katika Jina la Yesu Kristo.
Ni mimi katika Utumishi,
Frank Lema.

No comments: