Wednesday, February 25, 2009

JE UNAFAHAMU FAIDA ILIYOPO KATIKA KUIMBA NYIMBO ZA ROHONI?--2

KUIMBA NA KUSIFU –SILAHA KUBWA KATIKA VITA.

Ndugu katika Kristo, Nakusalimu katika Jina lipitalo majina yote, Jina ambalo kwalo sisi wanadamu wote tunaokolewa kutoka dhambini, Jina linalotubariki, Jina linalotuweka huru, Jina zuri la Yesu Kristo. Nakutakia neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. (1Peter 1:2)

Wiki iliyopita kwa msaada wa Roho Mtakatifu tulijifunza sehemu ya kwanza ya somo hili, linalotuonesha umuhimu wa sisi tumwaminio Kristo kuimba nyimbo za rohoni. Ninaamini Roho Mtakatifu alikuwa juu yako kukufundisha na ukaelewa vizuri, ninanamshukuru Yeye hata kwa ajili ya wale walionitumia shuhuda zao. Kati ya hao, ndugu mmoja alinieleza kuwa kuna wakati alikuwa kiimba nyimbo za Tenzi za Rohoni akiwa anaishi katika nyumba za kupanga, na ikawa inatokea kuwa kuna wakati akiwa anaimba, mapepo yanawapagawa na kuwatoka baadhi ya wapangaji wengine, pamoja na kuwa alipewa notice kwenye nyumba hizo.

Leo tunaendelea na sehemu hii ya pili na ya mwisho ya somo hili, na leo tuangalia Faida za kuimba nyimbo za sifa&kushukuru mara tuwapo katika mapito magumu.

Leo tutazama vita ya ajabu kama ilivyorekodiwa katika kitabu cha 2 Mambo ya Nyakati sura ya 20. Ili kukusaidia wewe kuelewa vizuri zaidi habari hii ninakupa shauri, pata muda na usome vizuri sura nzima hii ya 20, mimi hapa nitataja mistari michache tuu.

Habari hii inaanza katika mstari wa kwanza kabisa, ambapo tunaona kuwa mataifa matatu yalitoka na kwenda kujipanga kuwavamia wana wa Israeli (kabila lile la Yuda) katika nchi yao waliyopewa kukaa na Mungu Baba. Ndipo mtu mmoja akatoka na kwenda kumpa mfalme wa Israel (Yehoshafati) habari hizi za uvamizi. Hizi zilikuwa ni habari za kusikitisha na kuogopesha sana, kwa ilikuwa ni mataifa matatu yaliyojiandaa yanawavamia wana wa Israeli, wale wa Yuda, taifa moja.

Biblia inatuambia wazi kabisa katika mstari wa tatu kuwa hata Yehoshafati mwenyewe aliogopa, lakini kulikuwa na jambo moja zuri katika kuogopa kwake- yeye alikwenda kumwomba Mungu Baba juu ya uvamizi huu na akatangaza kufunga katika nchi nzima (ingekuwa baraka namna gani kama leo Taifa zima la Tanzania, au angalau hata kanisa tuu tukapanga kufunga siku Fulani kwa ajli ya jambo Fulani katika nchi yetu?) na tunaona kuwa walitoka katika miji ya Yuda na wakakusanyika pamoja kumwomba Mungu Baba kwa ajili ya hili.

Tunaona kuwa baada ya kukutana mbele za mfalme, mfalme aliomba maombi ambayo yalifanya hata wana wa Israeli wakatiwa moyo. Kisha Roho Mtakatifu akashuka juu ya nabii mmoja naye akasimama na kuwaeleza watu wote kuwa wasiogope kwani Baba Mungu anasema kuwa vita sio vyao bali ni vya Bwana(mstari wa 15)-{Ni vyema na wewe ukajisemea na kuamini hili kila mara unapokutana na majaribu mbalimbali katika maisha yako}. Kwa maana nyingine, Mungu alikuwa amekuja kuwasaidia katika vita vile. Kisha yule nabii akaendelea kuwaambia kuwa hawatahitaji kupigana vile vita, bali wao wafike tuu katika uwanja ule wa mapambano na waoune wokovu wa Bwana. Wakamwabudu Bwana (inawezekana waliimba nyimbo za kuabudu) na wakalala usiku ule kwa amani.
Wakaamka asubuhi iliyofuata, ambayo ilikuwa ndiyo siku ya kwenda vitani, sasa kwa namna tuliyozoea sisi, tungejipanga kwa kila mtu kupewa silaha na kufundishwa namna ya kupigana-hata kama tumeshaambiwa kuwa vita ni vya Bwana na sio vyetu, lakini alichofanya mfalme Yehoshafati ni tofauti kabisa na ndio hasa ninataka ujifunze wiki hii nzima.

Biblia inatuambia kuanzia mstari wa 21 kuwa, mfalme aliamka asubuhi ili kuongea na watu juu ya vita vilivyo mbele yao, na badala ya kuwapanga namna ya kupigana, yeye aliwapanga watu kwa ajili ya kuimba nyimbo za kumsifu Bwana kwa uzuri wa utakatifu wake. Tena akawaambia watangulie mbele ya jeshi lao wakiimba na kusema “Msifuni Bwana kwa maana fadhili zake zadumu milele”

Mstari wa 22 unasema “ Na walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao kinyume cha wana wa Amoni,Moabu na mlima Seiri waliokuja kupigana kinyume cha Yuda; nao wakauawa” Biblia haiweki wazi kuwa hawa “waviziao” ni kina nani lakini inavyoonesha, hawa ni malaika ambao Bwana aliwateremsha kuja kuwasaidia Yuda. Na kilichotokea ni wale wa mataifa waliokuja kuwashambulia wana wa Yuda walianza kupigana wao kwa wao hadi wakamalizana. Wana wa Yuda walipofika hapo walipo, walikuta maiti zao tuu, maadui zao wote walikufa! Huu ni ushindi mkubwa sana ambao Bwana aliwapatia bila nguvu zao hata kidogo na tunaambiwa kuwa wana wa Yuda walitumia siku tatu kukusanya nyara (mali) walizokuwa nazo wale maadui zao na kisha wakamshukuru Bwana.
Hebu utazame tena huo mstari wa 22. Utaona kuwa umeanza na maneno “na walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao………..” Maana ya haya maneno ni nini katika mstari huu?
Maana yake ni kwamba, Bwana hakuanza kuwapigania wao ila mpaka pale walipanza kuimba na kusifu. Yaani muda wote Bwana alikuwa kimya anawatazama watafanyaje, walipoanza kuimba na kusifu ndio akawapigania. Tupo pamoja?

Je unajifunza nini hapa? Hii ina maana kuwa wasingeanza kuimba na kusifu, Bwana angekaa kimya kabisa, nap engine wangeamua kupigana vita vile kwa nguvu za jeshi lao na wangeshindwa kwa sababu huo ulikuwa siyo mpango wa Mungu Baba kuwasaidia (sio kila mpango ni mpango wa Bwana kukusaidia pale upatapo shida). Hivyo Bwana alikaa kimya hadi pale walipoanza kuimba na kusifu.

Sasa nataka ujiulize, ni kwa nini Bwana awasubiri hadi waimbe na kusifu? Kwa nini sio hadi waombe na kufunga siku kadhaa? Kwanini kuimba?
Ukijiuliza swali hili utaona tena faida nyingine ya kumsifu Bwana pale unapopita katika magumu ya ulimwengu huu.

Sababu iliyopo ni kwa kuwa “Uimbaji ni sauti ya Imani” (“Praise is the voice of faith”). Yaani, unapoimba wimbo Fulani katika Roho, kwa kumaanisha, unaonesha imani iliyo ndani ya moyo wako kwa Bwana. Baada ya kumwomba Baba Mungu juu ya jambo fualani, je unaamini kuwa atakufanyia kama ulivyomwomba? Je, unaioneshaje imani yako? Njia mojawapo ya kuonesha imani ya mtu anapopita katika hali Fulani ngumu ni kwa kusikiliza maneno anayosema juu ya hali ile ngumu. Ukimsikia anasema maneno ya kukata tamaa, kuwa haamini kuwa Bwana atamsaidia hapo, basi ujue imani yake imekufa (na hiyo ni hali ya hatari) lakini ukimsikia anakiri ushindi kutoka kwa Bwana hata kama hali ni mbaya kiasi gani, basi mtu huyu anayo imani iliyo hai na Bwana atamsaidia mara moja.

Kwahiyo unapopita katika majaribu au hali yoyote ngumu usiyoipenda, ni vyema kumwomba Bwana kwa Jina la Yesu, na baada ya kumwomba, Atataka kuona imani yako, kwa hiyo anza kuimba nyimbo kadha wa kadha za kumsifu Bwana, uziimbe kwa kumaanisha na moyoni mwako ukimsifu Bwana kwa kukusaidia katika hali ngumu unayopitia, maana hiyo ndiyo imani yako. Ukifanya hivyo, wewe utakuwa ni sawa na wale wana wa Yuda walipoanza kuimba na kusifu, na Bwana akaja na kuwasaidia. Bwana atakusaidia na wewe. Na hilo ndilo kusudi la Roho Mtakatifu kukuletea ndani ya moyo wako nyimbo za kusifu kama tulivyoona kwenye sehemu ya kwanza ya somo hili.

Ninaamini kuwa umeona faida nzuri zilizo katika kumwimbia Bwana nyimbo katika Roho, kwa kumaanisha. Ukijisomea Biblia zaidi pia unaweza ukaona namna huduma ya uimbaji ilivyo ya muhimu sana katika kuujenga mwili wa Kristo. Na ninaamini kuwa utabarikiwa sana ukiyaweka haya katika matendo.
Watu wote tumshukuru na kumsifu Mungu Baba kwa kutuletea somo hili kwa wakati huu, na hapa ikiwa ni mwisho wa somo hili, Amen.
********************

SEMINA YA MWAKASEGE ARUSHA
Tangazo: Kwa wale wakazi wa jiji la Arusha, tunamshukuru Mungu kwa kuwa semina ya Neno la Mungu ya Mwalimu Christopher Mwakasege imeanza hapa Arusha tarehe 22 mwezi huu na itamalizika tarehe 1 mwezi wa tatu. Kwa wale wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani, huu ni wakati wa kwenda kupata maarifa ya Neno la Mungu pale. Lakini pia kwa wale waishio nje ya Arusha na wangependa kupata mafundisho ya semina hii yake katika kanda za redio, kanda za video(VHS), Audio CDs, au DVD basi wawasiliane nami ( savedlema2 at yahoo dot com) ili nione namna naweza kuwasaidia kwa kuwatumia.

****************
Je una ushuhuda wowote wa matendo ambayo Bwana amekufanyia katika maisha yako au familia yako na ungependa watu wengine wauosome na imani yao kwa Bwana iongezeke? Kama ndivyo basi ingia katika website yangu
www.lema.or.tz na kisha click ukurasa wa “Shuhuda” na uandike ushuhuda wako hapo.

********************
Tuzidi kuombeana tafadhali,
Frank Lema
www.lema.or.tz
Arusha.

No comments: