Thursday, February 19, 2009

JE UNAUFAHAMU UMUHIMU AU FAIDA YA KUIMBA NYIMBO ZA ROHONI?


Bwana Yesu Kristo asifiwe!

“Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.”(1Kor1:4)

JE UNAUFAHAMU UMUHIMU AU FAIDA YA KUIMBA NYIMBO ZA ROHONI?

Bwana Yesu asifiwe tena! Ninamshukuru Mungu,Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa wema wake ulio mkuu sana kiasi kisichoweza kuelezeka kwa namna ya kibinadamu, kwa kunilinda mimi na wewe pia mpaka kufikia hapa, tunajua kuwa hii ni neema tunayotakiwa kumshukuru Mungu kwayo.

Ni muda mrefu umepita tangu nikuletee ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia hii(kwa wale waliokwishajiunga na huduma hii tayari), na kama wewe ndio umejiunga na huduma hii karibuni, basi karibu na ubarikiwe.

Leo ninakuletea kwa uwezo wa Roho Mtakatifu ujumbe huu unaosema “Je, unaufahamu umuhimu wa kuimba nyimbo za rohoni?”

Kuna faida kubwa sana tunayoipata pale tunapoimba nyimbo mbalimbali za rohoni katika Kristo Yesu. Ninaposema kuimba hapa, siyo lazima uwe umepewa huduma na karama ya uimbaji kama tunavyowaona waimbaji wengi wakiimba na kurekodi nyimbo zao, hapana. Kila mtu aliyeokoka amepewa ndani yake aina Fulani ya uimbaji, hata kama siyo karama yake, japokuwa unaweza kuimba kidogo tuu, lakini Baba Mungu ndiye ameweka hicho kitu ndani ya kila aliyeokoka. Kwanini Baba Mungu ametupa aina hii ya uimbaji hata kwa watu ambao huduma yao wanayomtumikia Mungu kwayo siyo ya uimbaji? Hii ina maana zipo faida za kipawa hiki Mungu alichoweka ndani yetu na inapaswa tukitambue na tukitumie vyema.

Kwanza hebu soma na UITAFAKARI mistari hii hapa chini:

“Je, pana mtu yeyote miongoni mwenu aliye na shida? Anapaswa kusali. Je, yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa”.(Yakobo 5:13)

“Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani.”-(Kolosai 3:16)

1Samweli 16:23 : “Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa na ile roho mbaya ikamwacha”


Bila shaka baada ya kuitafakari mistari hiyo hapa juu umeanza kupata picha kidogo juu ya jambo hili.
Mungu ametupa aina hii ya uimbaji ndani yetu kwa ajili ya kutusaidia katika maeneo mbalimbali tunayopitia hapa duniani.

Unaona katika mstari ule wa Yakobo 5:16, Roho Mtakatifu anasema kuwa kama mtu ana shida basi anapaswa kuomba, kisha akasema kuwa, kama mtu ana furaha basi anapaswa kuimba nyimbo za sifa. Bila shaka nyimbo hizi kwa ajili ya kumsifu na kumshukuru Mungu kwa jambo alilolifanya hata ukawa na furaha. Je, unafikiri Roho Mtakatifu ametoa agizo hili bure? La Hasha! Lazima jambo hili ni la muhimu sana ndio maana ametuagiza tufanye hivyo.
Naandika waraka huu wa leo kukuhimiza kuhusu kuimba nyimbo za rohoni kwa Bwana. Wakati wowote unapokuwa mahali na ukaona tuu kuwa ndani ya moyo wako unajisikia furaha, basi pata muda mahali wewe mwenyewe au na watu wengine na uimbe nyimbo zozote utakazokuwa nazo za kumsifu Baba Mungu na utaona matunda yake, Mungu atafurahi na ataendelea kukupa hiyo furaha zaidi.

Ukitazama ule mstari wa kwenye kitabu cha Samweli 16:23 unaona kuwa mfalme Sauli alijiwa na roho mbaya iliyomsumbua, na ukisoma mistari inayotangulia utaona kuwa, Sauli alipoona tatizo hili, hakumwita kuhani aje kumwombea, bali baada ya kushauriwa, aliagiza aletwe mtu wa kumpigia kinubi pale roho ile itakapomjia, na akaletwa Daudi. Na ikawa kuwa kila roho ile ilipomjia, Daudi alikipiga kinubi chake na roho mbaya ikamwacha Sauli. Hebu tazama tofauti ya jambo hili lililotokea hapa na lile liliagizwa katika mstari ule wa Yakobo! Kwa waraka wa Yakobo tunaagizwa kuomba pale tunapopatwa na jambo lisilo jema, lakini hapa kwa Samweli, Sauli ameshauriwa kupata mtu wa kumwimbia!

Ni wazi kuwa, kuna mahali Mungu Baba ataamua kukusaidia kwa kukuongoza kuomba, na mahali pengine Atakuongoza kuimba tuu nyimbo katika Roho. Unachotakiwa ni kusikiliza ndani ya moyo wako unasukumwa kufanya kipi.

Unapoimba nyimbo za kiroho mahali popote kuna mambo mazuri yanatokea. Nafsi yako inaponywa majeraha yoyote uliyoyapata, iwe ni kwa kuonewa, kutukanwa au majeraha yoyote yale ya kwenye nafsi. Pia unajazwa nguvu za Roho Mtakatifu ndani yako kwa namna ya ajabu.

Siku moja kuanzia mida ya mchana hivi, niliona kuwa kuna wimbo Fulani wa kwenye kitabu cha Tenzi za Rohoni unakuja sana moyoni mwangu bila hata kusikia mtu akiuimba popote japokuwa hata sifahamu beti zake vizuri. Hali hii iliendelea kwa siku nzima, wimbo huo ulikaa sana moyoni mwangu na kila mara nilipokuwa free nilijikuta tuu naanza kuuimba kidogo. Nikapanga kuwa baadaye nitauimba. Jioni niliporudi kupumzika, nilichukua kitabu changu cha Tenzi za Rohoni na nikaanza kuuimba huo wimbo. Nilipofika katikati ya ule wimbo, ghafla niliona nimeteremkiwa na kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu kwa namna niliyoishangaa sana, kwani hata sikuomba hata kidogo kabla ya tukio hili. Baada ya hapo ndio nikagundua ni nini maana yake mtu anapokuwa katika shughuli zake na ghafla anasikia ndani yake wimbo Fulani umekuja hata kama haufahamu wote. Kwa hiyo tangu hapo mimi huwa karibu na vitabu vyangu viwili vya nyimbo (Tenzi za Rohoni na Holiness Song Book) na kila nisikiapo Roho Mtakatifu ameweka wimbo Fulani ndani yangu, ninahakikisha kuwa nimepata muda mzuri wa kuuuimba mimi mwenyewe au na wenzangu, na mara kwa mara nipatapo nafasi hukaa na kuimba nyimbo kadhaa kwenye vitabu hivi. Kama naona sifahamu sauti ya wimbo Fulani basi huwa natafuta mtu anayeujua namwomba tuuimbe, au natafuta ala (Midi files) za huo wimbo na kuimba kwa kuzifuatia. Na baada ya kuuimba huwa ninajua kwa hakika kabisa kuwa kuna kitu Mungu amenifanyia wakati nikiuuimba. Yaweza kuwa ni moyo wangu umeponywa, maombi yangu yamejibiwa au imani yangu imeongezwa wakati nilipoimba ule wimbo. Sasa utaona ni kwa nini Biblia inatushauri tufarijiane kwa nyimbo hizi hata wakati wa maombolezo, mioyo yetu inaponywa na tunaongezewa imani.

Wakati mwingine unapomwomba Mungu Baba jambo, anakutaka uonyeshe imani kuwa unaamini kuwa kile ulichoomba ni chako tayari (kama Biblia isemavyo) na ili kukusaidia uonyeshe imani yako, anakuwekea ndani ya moyo wako wimbo wa kumshukuru Mungu Baba, hata kama wimbo wenyewe hujawahi kuuimba miaka kadhaa, na utajikuta tuu unataka kuiimba na utashangaa pia kuwa wala hakuna mtu yeyote aliyekutajia huo wimbo, na wala hujamsikia mtu akiuimba huo wimbo.


Je, na wewe umeshakutana na jambo kama hili? Ulichukua hatua gani? Watu wengi hujikuta wanapuuzia tuu na kusema “Ah! Huu wimbo umetoka wapi tena saa hizi na mimi nipo na kazi zangu?” Nimekuletea waraka huu kwa Roho Mtakatifu ili kukusaidia, kuanzia sasa unapoona hali ya namna hii, hakikisha kuwa unapata muda mzuri uliotulia na ukae na kuziimba nyimbo hizi, ni za muhimu sana. Ninakupa shauri sasa, nunua vitabu vyako vya nyimbo (kama Tenzi za Rohoni) ukae nacho pale ulipo, na unapopata muda, tafuta wimbo mmojawapo na uuimbe, baada ya muda mfupi utaona faida yake njema. Kama unafamilia yako, tengeni muda wa kuomba kila siku usiku (kwa mfano) kabla ya kulala, na kabla ya kuomba, changueni nyimbo chache za rohoni kutoka kwenye vitabu mlivyonavyo na mziimbe wote kwa pamoja. Baada ya muda mfupi mtagundua kuwa upendo na mshikamano ndani ya familia (au kundi lolote) unaongezeka kwa namna msiyoijua na Mungu anajibu maombi yetu kwa namna mnayofurahi zaidi.

Huu ndio ujumbe Bwana aliouweka moyoni mwangu siku hii ya leo kwa ajili yako na ninaamini kuwa utafanyika baraka kubwa sana kwako pale utakapouweka katika matendo, na hayo ndio maombi yangu kwa Baba Mungu.

“….Je yuko mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa”

Mungu Baba akubariki na tuzidi kuombeana daima.

Ni mimi katika Kristo,
FRANK LEMA.
www.lema.or.tz
Arusha Tanzania.


// Kupokea ujumbe huu kwa email jiunge na mailing lists kwa kutembelea www.lema.or.tz //

No comments: