Wednesday, February 18, 2009

Mchungaji Auwawa kwa baada ya kufumaniwa

MCHUNGAJI wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Manundu mjini hapa, Bw. Ernest Mngazija (52) ameuawa kwa kuchomwa kisu baada ya kufumaniwa na mke wa mtu akifanya naye mapenzi ndani ya nyumba yao. Tukio hilo lilitokea juzi saa 2. 30 usiku baada ya Mchungaji huyo kukutwa katika nyumba yenye namba HMK/MT/86 iliyopo mtaa wa Mtonga nje kidogo ya mji wa Korogwe. Mchungaji huyo aliyeacha mke na watoto zaidi ya watano, alikutwa na Bi. Happy Temu (19) ambaye ni mke wa Bw. Mandia. Mwandishi wa habari hizi alipofika katika eneo la tukio jana alishuhudia michirizi ya damu kutoka nyumba aliyofumaniwa mchungaji huyo hadi sehemu aliyoangukia kiasi cha mita 100 baada ya kukosa nguvu kutokana na damu kumtoka nyingi. Akizungumzia tukio hilo, Bw. Herman Kiluu ambaye ni Balozi wa mtaa wa Mtonga Juu (Meco) alisema, Mchungaji huyo alikutwa akifanya mapenzi na mke huyo nyakati za usiku. Alisema baada ya kijana huyo kumkuta mchungaji alikwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bw.Hassan Mndolwa 'Segere Kuu'ambaye naye alifika nyumbani kwake ambapo walivunja mlango wa nyumba hiyo baada ya mke kukataa kufungua na hivyo kuingia ndani kujua kulikoni. "Mchungaji alipotoka alikatwa kisu cha shingo na Mandia, akakatwa tena huku akitafuta njia za kukimbia na vijana walikuwa wakipiga kelele za mwizi," alisema Bw. Kiluu. Alisema hata hivyo, baada ya Mchungaji kukatwa visu vingi alikosa nguvu na kuanguka jirani na nyumba yake ambapo walimpeleka Hospitali ya Magunga kupitia Polisi lakini alifariki akiwa njiani kabla ya kufikishwa hospitali kutibiwa. Tukio hilo limeibua maswali mengi kwani wiki iliyopita, Mchungaji huyo aliongoza misa ya marehemu Salmin Karata ambaye alikuwa dereva wa World Vision aliyekufa kwa ajali ambapokatika mahubiri yake alisema watu wajiandae na kifo. "Leo hii Salmin kesho mimi au wewe," alikaririwa akisema. Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Bw. Sirro Nyakoro alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema mtuhumiwa anasakwa na Polisi kwani alikimbia baada ya mauaji hayo. Alisema Happy alihojiwa na Polisi na kuachiwa na atakuwa shahidi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa. Shahidi mwingine atakuwa Balozi aliyeitwa na mtuhumiwa kushuhudia ugoni. Kamanda alisema, marehemu alichomwa visu mara nne katika sehemu mbalimbali za mwili na kutokwa damu nyingi na alikutwa uchi wa mnyama akivaa chupi mlango ulipovunjwa. Alipoulizwa walijiridhishaje Mchungaji alikuwa amefanya mapenzi na Bi. Happy Kamanda alisema 'mtu amekutwa uchi wa mnyama anavaa chupi maana yake alikuwa anafanya nini".

No comments: