Thursday, March 19, 2009

Wanafunzi Tegeta wateswa na mapepo

ZAIDI ya wanafunzi 20 wa kike wa Shule Sekondari ya Tegeta jijini Dar es Salaam, wamekumbwa na ugonjwa wa kuanguka na kupoteza fahamu.
Wakizungumza na Mwananchi, jana baadhi ya wanafunzi walisema ugonjwa huo ulianza jana saa 5.30 asubuhi baada ya mmoja wao wa kidato cha pili, kuanza kupiga kelele kuwa watu waliokuwa na mapanga, walikuwa wakimfuata.
Walisema mwanafunzi huyo alikumbwa na hali hiyo wakati mwalimu anafundisha.Kwa mujibu wa maelezo yao, mgonjwa huyo alianza kupiga kelele hafla na kuchukua biblia aliyokuwa ameiweka mfukoni na kuanza kukemea mithili ya walokole, katika kufukuza mashetani.
"Tulishangaa mwenzetu alipoanza kukemea na kudai kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanamwendea ili kumkatakata kwa mapanga. Baadhi walimcheka lakini baadaye, wale waliomcheka nao wakaanza kuanguka na kupoteza fahamamu," alisema mmoja wa wanafunzi hao, kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Alisema hali hiyo iliwafanya wanafunzi kuingiwa na hofu hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huo ulikuwa unaendelea kusambaa kwa wengine waliokuwa karibu na mgonjwa wa kwanza na hatimaye kwa wanafunzi wengine waliokuwa madarasani.
Alisema hata hivyo ni jambo la kushangaza kuwa ugonjwa huo, uliwakumba wanafunzi wa kike tu.
Mwanafunzi huyo alisema hofu ilizidi pale wanafunzi walioanguka, walipokuwa wakihema kwa kasi kubwa na kukosa nguvu baada ya kuzinduka.
Mkuu wa shule hiyo, Tailes Ngela alithibitisha habari kuhusu tukio hilo na kwamba wanafunzi waliopoteza fahamu ni wanne na wengine walifadhaika kutokana na mshutuko wa kuona wenzao wakihangaika.
Alisema kufuatia hali hiyo, uongozi wa shule uliamua kusitisha masomo, na kuwaruhusu wanafunzi kurudi nyumbani, ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kiini cha ugonjwa huo.
"Aliyeanza kupatwa na ugonjwa huu ni binti ambaye amehamia shuleni kwetu, historia yake inaonekana huwa anakumbwa na matatizo haya mara kwa mara. Tunafanya mawasiliano na uongozi wa juu kujua tufanye nini kudhibiti tatizo hili," alisema Mkuu wa shule.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch, aliishauri serikali kufanya utafiti na kutafuta ufumbuzi juu ya tatizo hilo ambalo bado chanzo chake hakijajulikana.
Source: mwananchi

Wednesday, March 18, 2009

Maendeleo ya Wasabato Masalia Dar

Kundi la watu wanaojiita wa madhehebu ya Wasabato Masalia waliopiga kambi Dar es Salaam, wameendelea kuishi katika mazingira magumu hali iliyosababisha mmojawao kupoteza maisha.
Sambamba na kuishi katika mazingira magumu na machafu, Wasabato Masalia hao wapatao 30 walio katika kambi ya Tabata Sanene, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wamesema licha ya kufukuzwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bado wana mpango wa kwenda tena kwa lengo la kusafiri nje ya nchi kuhubiri Neno la Mungu. Wakielezea maisha wanayoishi, majirani wa eneo hilo walisema wiki tatu zilizopita, walishuhudia mwanaume wa kundi hilo aliyeumwa na nyoka katika kichaka wanamoishi na majirani wakataka kutoa msaada wa kwenda kumtibu, lakini wenzake wanaojiita Wainjilisti walikataa wakidai angetibiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. “Yule kijana aliumwa na nyoka na akabadilika rangi mwishowe akafariki dunia na wenzake (Wasabato Masalia) wakamzika kwenye mwembe jirani na walipo na sasa hivi kuna mwanamke anaumwa amevimba sana miguu na tunamsikia analia sana, lakini wenzake hawataki apelekwe hospitalini wanamficha,” alisema Paulina Maro anayeishi jirani na kambi hiyo.
Hata hivyo, mmoja wa waumini hao, Fanuel Saasita, aliliambia gazeti hili kuwa hakuna mtu aliyefariki dunia eneo hilo na wao hawatakufa kwani Mungu anawalinda na kuongeza: “Aliyekufa ni kijana wa miaka 30 ambaye alifia katika gereza la Keko na walimzika huko huko, na hapa hakuna aliyekufa”. Mbali na hilo, Saasita alidai kuwa Mungu ameshawaeleza waendelee na mpango wao wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius kupanda ndege bila hati za kusafiria wala tikiti na kwenda nchi mbalimbali kutangaza onyo maalumu kutoka kwa Mungu. “Tunachosubiri sasa ni amri kutoka kwa Mungu kutuambia leo nendeni na ndipo tutakapokwenda huko, Mungu hutuambia kwa njia ya njozi nasi tutatekeleza, tunakwenda kuieleza Dunia, kuwa utawala wa serikali unapaswa kushirikiana na utawala wa dini kukuza uchumi wa Dunia na Jumapili ni siku ya mapumziko na si kuchanganya na kazi,” alisema.
Majirani wa eneo hilo walisema watu hao hawana usumbufu isipokuwa wanawakera kwa kujisaidia hovyo katika maeneo yao, hasa katika bustani za mchicha na kusababisha watu wengi kuacha kununua mboga hiyo katika eneo hilo. Gazeti hili liliwashuhudia zaidi ya Wasabato Masalia 15 waliokuwa eneo hilo huku wengi wao wakiwa na ugonjwa wa ngozi, wakati wenzao wengine wakiwa wamekwenda kutafuta chakula na fedha na kuwaona wakipika chakula, wakichota maji ya kunywa na kwa matumizi yao kutoka kwenye dimbwi la maji yasiyo salama. Katika eneo hilo walilopo kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, wameweka karatasi ndogo ya nailoni wanakohifadhi vyakula huku wenyewe wakilala ardhini, hali wanayoieleza kuwa wamepangiwa na Mungu na kuridhika nayo na kuongeza kuwa wakati wowote watahamia eneo lingine watakaloelekezwa pia na Mungu. Ingawa wenyewe walidai kuwa fedha na chakula wanapelekewa na Mungu, majirani walisema mara kwa mara wamekuwa wakienda katika maduka barabarani kuomba msaada wa fedha na chakula. Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema kwa sasa hawezi kuwakamata kwa sababu hawajafanya kosa la jinai na kuahidi suala lao kuliwasilisha katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilala, ili watu wa Ustawi wa Jamii waweze kuwapa elimu na kuwarejesha maeneo walikotoka. Wengi wao wanatokea Kyela, Mbeya na Musoma, Mara. Hata hivyo, alisema watakapokwenda kuweka kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, atawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Wasabato Masalia walianza kuweka kambi katika maeneo manne tofauti, matatu eneo la Tabata Sanene na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere tangu mwaka jana. Waliwahi kukamatwa na kuwekwa rumande kwa siku 40 kwa tuhuma za kuvamia eneo la mtu. Hata hivyo, waliachiwa baada ya aliyewashitaki kuwasamehe. Wamekuwa wakihama maeneo kutokana na kupigwa na wananchi wa maeneo husika kwa uchafuzi wa mazingira.

Tuesday, March 3, 2009

Smart Card ,Namba 666 na Mfumo wa Computer

Kama ilivyo ada , wataalamu wa kampuni inayokuwa kwa kasi hivi sasa hapa nchini Tanzania ya DigitalBrain jana walikuwa na mtumishi wa Mungu,mwalimu na mwinjilisti Isaya Mzolo ndani ya radio WAPO FM.Mwalimu Isaya Mzolo ambaye pia ni mtaalamu aliyebobea katika masuala ya computer aliyelezea kwa kina na kufafanua masuala hayo jinsi ambavyo mfumo wa computer na biochips mbali mbali zinavyoweza kupandikizwa kwenye mwili wa binadamu hasa kwenye paji la uso na kwenye mkono.



Soma hapa kwanza:



Ufunuo wa Yohana 13:16-18 "16Pia aliwalazimisha watu wote, wakubwa kwa wadogo, matajiri na mas kini, watu huru na watumwa, watiwe alama kwenye mikono yao ya kulia au kwenye vipaji vya nyuso zao. 17Hakuna mtu ye yote ambaye angeweza kununua au kuuza kitu kama hana alama ile, yaani jina la huyo mnyama au namba ya jina lake.
18Jambo hili linahitaji hekima. Mwenye akili ya kutambua apige hesabu ya mnyama huyo kwa sababu ni namba ya mtu. Namba yake ni mia sita sitini na sita. "



Ufunuo wa Yohana 14:9 "9Malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kuu, ``Kama mtu ye yote anamwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa alama yake kwenye kipaji cha uso wake au kwenye mkono wake, 10yeye naye atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu ambayo imemiminiwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchan ganywa na maji. Naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya mal aika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo. 11Moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele; wala hakuna nafuu, mchana au usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake au kwa ye yote anayepokea alama ya jina lake.'' 12Jambo hili linahitaji watu wa Mungu, wale ambao wanazishika amri zake, wawe wavumilivu na kumwamini Yesu"

Waweza kusikiliza kwa undani mafundisho haya kutoka kwa mwalimu Isaya Mzolo kupitia hata http://www.digitalbraintz.com/