Kundi la watu wanaojiita wa madhehebu ya Wasabato Masalia waliopiga kambi Dar es Salaam, wameendelea kuishi katika mazingira magumu hali iliyosababisha mmojawao kupoteza maisha.
Sambamba na kuishi katika mazingira magumu na machafu, Wasabato Masalia hao wapatao 30 walio katika kambi ya Tabata Sanene, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wamesema licha ya kufukuzwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bado wana mpango wa kwenda tena kwa lengo la kusafiri nje ya nchi kuhubiri Neno la Mungu. Wakielezea maisha wanayoishi, majirani wa eneo hilo walisema wiki tatu zilizopita, walishuhudia mwanaume wa kundi hilo aliyeumwa na nyoka katika kichaka wanamoishi na majirani wakataka kutoa msaada wa kwenda kumtibu, lakini wenzake wanaojiita Wainjilisti walikataa wakidai angetibiwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. “Yule kijana aliumwa na nyoka na akabadilika rangi mwishowe akafariki dunia na wenzake (Wasabato Masalia) wakamzika kwenye mwembe jirani na walipo na sasa hivi kuna mwanamke anaumwa amevimba sana miguu na tunamsikia analia sana, lakini wenzake hawataki apelekwe hospitalini wanamficha,” alisema Paulina Maro anayeishi jirani na kambi hiyo.
Hata hivyo, mmoja wa waumini hao, Fanuel Saasita, aliliambia gazeti hili kuwa hakuna mtu aliyefariki dunia eneo hilo na wao hawatakufa kwani Mungu anawalinda na kuongeza: “Aliyekufa ni kijana wa miaka 30 ambaye alifia katika gereza la Keko na walimzika huko huko, na hapa hakuna aliyekufa”. Mbali na hilo, Saasita alidai kuwa Mungu ameshawaeleza waendelee na mpango wao wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius kupanda ndege bila hati za kusafiria wala tikiti na kwenda nchi mbalimbali kutangaza onyo maalumu kutoka kwa Mungu. “Tunachosubiri sasa ni amri kutoka kwa Mungu kutuambia leo nendeni na ndipo tutakapokwenda huko, Mungu hutuambia kwa njia ya njozi nasi tutatekeleza, tunakwenda kuieleza Dunia, kuwa utawala wa serikali unapaswa kushirikiana na utawala wa dini kukuza uchumi wa Dunia na Jumapili ni siku ya mapumziko na si kuchanganya na kazi,” alisema.
Majirani wa eneo hilo walisema watu hao hawana usumbufu isipokuwa wanawakera kwa kujisaidia hovyo katika maeneo yao, hasa katika bustani za mchicha na kusababisha watu wengi kuacha kununua mboga hiyo katika eneo hilo. Gazeti hili liliwashuhudia zaidi ya Wasabato Masalia 15 waliokuwa eneo hilo huku wengi wao wakiwa na ugonjwa wa ngozi, wakati wenzao wengine wakiwa wamekwenda kutafuta chakula na fedha na kuwaona wakipika chakula, wakichota maji ya kunywa na kwa matumizi yao kutoka kwenye dimbwi la maji yasiyo salama. Katika eneo hilo walilopo kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, wameweka karatasi ndogo ya nailoni wanakohifadhi vyakula huku wenyewe wakilala ardhini, hali wanayoieleza kuwa wamepangiwa na Mungu na kuridhika nayo na kuongeza kuwa wakati wowote watahamia eneo lingine watakaloelekezwa pia na Mungu. Ingawa wenyewe walidai kuwa fedha na chakula wanapelekewa na Mungu, majirani walisema mara kwa mara wamekuwa wakienda katika maduka barabarani kuomba msaada wa fedha na chakula. Akizungumzia hali hiyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema kwa sasa hawezi kuwakamata kwa sababu hawajafanya kosa la jinai na kuahidi suala lao kuliwasilisha katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilala, ili watu wa Ustawi wa Jamii waweze kuwapa elimu na kuwarejesha maeneo walikotoka. Wengi wao wanatokea Kyela, Mbeya na Musoma, Mara. Hata hivyo, alisema watakapokwenda kuweka kambi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, atawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Wasabato Masalia walianza kuweka kambi katika maeneo manne tofauti, matatu eneo la Tabata Sanene na Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere tangu mwaka jana. Waliwahi kukamatwa na kuwekwa rumande kwa siku 40 kwa tuhuma za kuvamia eneo la mtu. Hata hivyo, waliachiwa baada ya aliyewashitaki kuwasamehe. Wamekuwa wakihama maeneo kutokana na kupigwa na wananchi wa maeneo husika kwa uchafuzi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment