ZAIDI ya wanafunzi 20 wa kike wa Shule Sekondari ya Tegeta jijini Dar es Salaam, wamekumbwa na ugonjwa wa kuanguka na kupoteza fahamu.
Wakizungumza na Mwananchi, jana baadhi ya wanafunzi walisema ugonjwa huo ulianza jana saa 5.30 asubuhi baada ya mmoja wao wa kidato cha pili, kuanza kupiga kelele kuwa watu waliokuwa na mapanga, walikuwa wakimfuata.
Walisema mwanafunzi huyo alikumbwa na hali hiyo wakati mwalimu anafundisha.Kwa mujibu wa maelezo yao, mgonjwa huyo alianza kupiga kelele hafla na kuchukua biblia aliyokuwa ameiweka mfukoni na kuanza kukemea mithili ya walokole, katika kufukuza mashetani.
"Tulishangaa mwenzetu alipoanza kukemea na kudai kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanamwendea ili kumkatakata kwa mapanga. Baadhi walimcheka lakini baadaye, wale waliomcheka nao wakaanza kuanguka na kupoteza fahamamu," alisema mmoja wa wanafunzi hao, kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Alisema hali hiyo iliwafanya wanafunzi kuingiwa na hofu hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huo ulikuwa unaendelea kusambaa kwa wengine waliokuwa karibu na mgonjwa wa kwanza na hatimaye kwa wanafunzi wengine waliokuwa madarasani.
Alisema hata hivyo ni jambo la kushangaza kuwa ugonjwa huo, uliwakumba wanafunzi wa kike tu.
Mwanafunzi huyo alisema hofu ilizidi pale wanafunzi walioanguka, walipokuwa wakihema kwa kasi kubwa na kukosa nguvu baada ya kuzinduka.
Mkuu wa shule hiyo, Tailes Ngela alithibitisha habari kuhusu tukio hilo na kwamba wanafunzi waliopoteza fahamu ni wanne na wengine walifadhaika kutokana na mshutuko wa kuona wenzao wakihangaika.
Alisema kufuatia hali hiyo, uongozi wa shule uliamua kusitisha masomo, na kuwaruhusu wanafunzi kurudi nyumbani, ili kutoa nafasi ya kufanyika kwa uchunguzi kuhusu kiini cha ugonjwa huo.
"Aliyeanza kupatwa na ugonjwa huu ni binti ambaye amehamia shuleni kwetu, historia yake inaonekana huwa anakumbwa na matatizo haya mara kwa mara. Tunafanya mawasiliano na uongozi wa juu kujua tufanye nini kudhibiti tatizo hili," alisema Mkuu wa shule.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch, aliishauri serikali kufanya utafiti na kutafuta ufumbuzi juu ya tatizo hilo ambalo bado chanzo chake hakijajulikana.
Source: mwananchi
2 comments:
Bwana Yesu Asifiwe....!Ndio tuseme hii Blog imekufa?Mbona haiwi Updated?Zinatakiwa Blog nyingi iwezekenavyo za Kikristo.
Bwana Yesu Asifiwe....!Ndio tuseme hii Blog imekufa?Mbona haiwi Updated?Zinatakiwa Blog nyingi iwezekenavyo za Kikristo.
Post a Comment