Monday, May 4, 2009

Azimia baada ya kusikia kishindo cha nyundo-Mbagala

MKAZI wa Mbagala Kuu, Grace Songo jana alianguka chini ghafla na kupoteza fahamu baada ya kusikia kishindo cha nyundo kilichofanana na mlipuko wa mabomu.

Songo alipoteza fahamu baada ya kusikia kishindo cha nyundo wakati mmoja wa waathirika wa mabomu hayo alipokuwa akifanya marekebisho ya nyumba ili apate sehemu ya kuwahifadhi watoto wake baada ya kukosa msaada wa mahema tangu alipokumbwa na maafa hayo.

Hata hivyo saa tatu baadaye Mwananchi ilimfuata mama huyo nyumbani kwake na kuzungumza naye baada ya kupata nafuu alisema "bado tumekumbwa na wasiwasi hasa ukizingatia kwamba wakati mlipuko wa mabomu unatokea nilikuwa hapa nyumbani na nyumba yangu pia imeathirika."

Alisema hali hiyo haimtokei yeye peke yake bali ni watu wengi wanazimia baada ya kusikia mlipuko ama kishindo chochote kinachotokea karibu na maeneo hayo.

Wasiwasi huo umezidi kuwakumba baadhi ya wakazi wa maeneo hayo ikiwa ni siku sita tangu kutokea kwa mlipuko wa mabomu katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania kikosi cha 671 na kuteketeza kaya zaidi ya 800 na watu zaidi ya 20 kupoteza maisha.

Kuhusu hali ya msaada Songo alilalamikia utaratibu unaotumika katika kugawa misaada hiyo.

"Tangu tukumbwe na janga hili hatujapata msaada wowote tunalala nje na tunashinda njaa ingawa misaada inatolewa kila siku, lakini baadhi ya watu wanaonufaika si waathirika halisi wa tukio hili,”alisema Songo.

Hata hivyo Mwananchi pia ilishuhudia baadhi ya waathirika wanaoishi mbele ya kituo cha kugawa msaada wakimlalamikia msimamizi wa chama cha msalaba mwekundu, Stella Marealle pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii Manispaa ya Temeke na mwenyekiti wa ugawaji wa misaada John Bwana kuwa hajapata msaada wowote huku akilala nje na watoto wake.

Mmoja wa waathirika Daniel Kisa ambaye nyumba yake imeharibiwa na mabomu hayo alisema kuwa "tangu nyumba yangu iharibiwe na mabomu ninaishi kwa wasiwasi mkubwa wa bomu kuwepo eneo hili hasa baada ya askari wa JWTZ kuchimbua bomu ambalo halijalipuka nyuma ya nyumba yangu hii inazidi kunipa wasiwasi."

Source: Mwananchi

No comments: