Saturday, April 17, 2010

MADHEHEBU MAPYA YALIYOIBUKA YANA UTATA?

Nakushukuru Mlima Sayuni. Mungu azidi kuwalinda kwa nguvu zake.
Kama tungeweza kurekebisha miaka kama vile kurekebisha mishale ya saa, ikaonyesha wakati tuutakao, tungeirudisha nyuma hadi kiasi cha miaka 2000 iliyopita.
Mfano, tuseme tumefanikiwa na sasa ni mwaka 30 au 33 Baada ya Kristo (30 B.K. au 33 B.K.), kutegemea ni mwaka upi unaotajwa na historia kwamba Yesu Kristo aliuawa. Ikiwa tunaishi katika wakati huo, kwa wale tunaoishi nchini Israeli, dini kuu tunayoifahamu katika mazingira yetu ni dini ya Kiyahudi.
Mwaka huu wa 33 B.K. na miaka michache ijayo, japo kuna wafuasi wengi wa Yesu Mnazarethi katika jamii yetu, lakini bado haijasikiwa imani ya kidini inayoitwa kwa jina la Ukristo. Hivyo ukituuliza habari za dini hiyo tutakujibu kwa usahihi kabisa kwamba, hakuna dini inayoitwa Ukristo, wala madhehebu yanayoitwa ya Kikristo.
Ukituuliza kuhusu Romani Katoliki, Lutherani, Anglikana, Moraviani, Presbyterian, Baptisti, Methodist, Waadventista-Wasabato, Wapentekoste, n.k., kwa usahihi kabisa tutakujibu, hakuna madhehebu hayo hapa Israeli, wala katika ufalme wa Kirumi. Mwaka huu huu wa 33 B.K., ukituuliza kuhusu Uislamu, tutakujibu kwa usahihi kabisa, kwamba, hakuna dini yenye jina hilo. Wala mtu aitwaye Mtume Muhammad. Maana Uislamu ulianza kama miaka 600 B.K. Wakazi wa Makka na Madina wakiutambua kama “madhehebu yaliyoibuka hivi karibuni”.
Ukatoliki ulipoanza yawezekana tarehe haijulikani. Lakini tukio la Mfalme Constantine wa Roma, mnamo mwaka 313 B.K., kuutambua Ukristo na kujaribu kuunda umoja kati ya serikali yake na kanisa ni hatua muhimu katika kuwepo kwa Romani Katoliki; ambapo viongozi wa kanisa waliongezewa na madaraka ya kiserikali. Kinachozaliwa hapa, mwaka huu 313 B.K., sehemu ya jamii inakitambua kama “madhehebu yaliyoibuka hivi karibuni”. Maana kina muundo tofauti na lile kanisa la Yerusalemu la mitume.
Tunasogea. Mwaka 1530 B.K., mvutano mkali unaibuka kati ya Padri Mkatoliki, Mjerumani, Martin Luther na wakuu wa Ukatoliki, hoja mojawapo kuu ni uamuzi wa Vatican kuugeuza msamaha wa dhambi kuwa biashara. Luther anayapinga mafundisho haya na kujiondoa chini ya Papa. Luther na waliomfuata wanaanzisha kundi jipya, hatimaye linajulikana kama Kanisa la Kilutheri, kufuata jina la Luther. Mwaka huu 1530 B.K., jamii inalitambua kama “madhehebu yaliyoibuka hivi karibuni” kutoka Romani Katoliki.
Tunaufikia 1534 B.K. (au 1535 B.K.). Mfalme Henry III wa Uingereza, Mkatoliki, anamtaliki mkewe Catherine. Anamuoa Anne Bolyn licha ya kukatazwa na Papa. Henry anaiondoa Uingereza chini ya mamlaka ya Papa. Anajitangaza kuwa mkuu wa kanisa la Uingereza. Anglikana inaanzishwa. Jamii iliyopo mwaka huu 1534B.K. inaitambua Anglikana kama “madhehebu yaliyoibuka hivi karibuni”.
Kihistoria, dini na madhehebu yote tunayoyafuata viliwahi kutambulika kama “madhehebu yaliyoibuka hivi karibuni”. Yaliyoibuka 300 au 1500 B.K., yana uhalali sawa na yale yaliyoibuka 1900, au sasa 2010 B.K. Hakuna lenye uhalali wa kuyadhibiti wala kuyatawala mengine. Maana YOTE “yameibuka hivi karibuni”. Bali “Aliye juu (Mungu na Kristo) ndiye” anayetawala, Danieli 4:32.

Mwandishi wa makala haya ni:
Elias S. Bilegeya
Box 54655, D’Salaam
+255-765-653 985
eliasb89@hotmail.com

4 comments:

Anonymous said...

He! he! he! Bilegeya umetokea wapi? Karpenaumu? hapan hivi umeshwahi kuishi na waberoya? au ulikuwa mmoja wao? miaka 33 B.K Ina mengi sana ya kueleza, umeeleza kwa kifupi mno natamani sana kama ungeandika nakala ndefu maana nimeanza kusoma tu nashangaa imefika mwisho.

Ubarikiwe kwa kipande hiki kizuri kabisa cha historia na ukweli ambao haupingiki.

Kalenga

Anonymous said...

Katoliki maana yake kwa kiingereza "universal" yaani ya ulimwengu wote kama unapenda. Mwaka 300 Ukatoliki haukuanzishwa na mfalme Constatine wala jina Katoliki halikuanzishwa wakati huu.Kilichotekea mwaka huu ni Mfalme kuutambua Ukristo katika himaya yake jambo ambalo ni mzuri kabisa na pia hata kutoa sehemu ya mali yake kwa kanisa jambo ambalo ni jema sana.

Kumbuka kwamba kundi la wakristo lililokuwepo wakati huu ni moja tu Wakristo. Jina Katoliki limeanza kutumika hasa karne ya 14 baada ya migogoro katika Kanisa iliyopelekea utengano ndipo makundi mbalimbali yakaanza kujiita majina kama Lutheran, Katoliki na kadahalika.

Hivyo kimsingi Kanisa Katoliki ni lile lile lililoanzishwa tangu mwako kwa kufuata succession au mtiririko wa mamlaka ya kitume hadi leo.

Yamekuwapo mabadiliko kadhaa ya kiibada na kimtazamo katika mambo ambayo sio "core" yaani mambo ambayo sio hasa msingi au nguzo ya Imani ya Kikrsto lakini Kanisa Katoliki linabaki lenye msingi ule ule wa Mitume.

Kanisa Katoliki halijajitenga kutoka kikundi chochote kilichokuwapo awali bali Kanisa Katoliki ndilo kanisa la tangu awali. Hata kama Kuna tofauti za kimtimzamo lakini ndilo kanisa lile la Kristo Yesu siku zote.

Anonymous said...

Ukiangalia ufunuo wa yoh unasema yote kuhusu kanisa la leo lilivyogawanyika na udhilisho ni utakatifu hakuna dini

Anonymous said...

Ukiangalia ufunuo wa yoh unasema yote kuhusu kanisa la leo lilivyogawanyika na udhilisho ni utakatifu hakuna dini