Wednesday, November 14, 2007

JK atakiwa kuomba radhi

MZOZO MAHAKAMA YA KADHISUALA la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini linazidi kupanuka, na kwa mara ya kwanza tangu mjadala huo uanze, jina la Rais Jakaya Kikwete limeanza kuingizwa katika mzozo huo. Rais Kikwete ametajwa katika sakata hilo pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, wakidaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mgogoro huo, ambao sasa unazidi kuchukua sura tofauti. Kwa upande wake, Rais Kikwete ametajwa akitakiwa kuwaomba radhi Watanzania, kwa kile kinachodaiwa kuwa, dhamira yake ya kutaka kuigeuza Tanzania kikatiba kuwa nchi ya Kiislamu na hivyo kuirejesha katika mzozo wa miaka ya mwanzo ya 1990 uliohusisha juhudi za baadhi ya viongozi kuiingiza katika kundi la nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC). Aidha, IGP Mwema amepewa siku 21 kumuomba radhi Mchungaji Christopher Mtikila, kutokana na kitendo chake cha kuwatuma askari wamkamate (Mtikila), kumhoji na hatimaye kumfungulia mashtaka ya uchochezi wakati hana kosa. Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mchungaji Mtikila, ambaye ndiye aliyeibua mjadala unaoendelea kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, alitaka tamko la Rais Kikwete la kuomba radhi liambatane na hatua kali za kisheria dhidi ya watumishi wote wa umma, waliohusika kwa namna yoyote katika kitendo hicho cha kuingiza Uislamu katika ilani yake ya uchaguzi, serikali na Bunge. Aliongeza kuwa sambamba na hilo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho alidai ni kikundi cha maslahi ya kibinafsi cha watu fulani, nacho kifutwe kama inavyoagiza katiba. Mtikila alisema, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Halmashauri ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT), walikutana na walitaka kutoa tamko la kupinga mapinduzi hayo ili kulinda katiba ya nchi, lakini serikali iliwahadaa wasifanye hivyo bali wangojee tume yao ilifanyie kazi suala hilo. Hata hivyo, Mtikila alisema, inashangaza kuwa tofauti na ahadi iliyotolewa na serikali kwa taasisi hizo nyeti za kidini nchini, harakati zilianzishwa ili muswada kuhusu Mahakama ya Kadhi upelekwe bungeni bila Wakristo kujua, mpaka Mungu alipowafunulia na kuwawezesha kuwahisha ulinzi wao wa katiba mahakamani. Alisema yeye hapingi kuanzishwa kwa mahakama hiyo, bali anachopinga ni kuingizwa katika katiba ya nchi ambayo kimsingi inapingana na suala hilo. “Tunachopinga vikali sisi ni kuingizwa kwa dini ya Kislamu au Mahakama ya Kadhi katika katiba ya nchi yetu,” alisema na kuongeza kuwa hata kama kutakuwa na harakati za kutaka kardinali, askofu au paroko wa Kanisa Katoliki kuingizwa katika katiba ya nchi, atapinga kama atakavyopinga kuingizwa mtandao wowote wa kidini katika katiba. Aliwataka Waislamu wasidanganywe kwa kuwa Mahakama ya Kadhi ni mradi wa watu wachache, na kuongeza kuwa, kuna nchi kadhaa za Kiislamu zimekataa mahakama hiyo kwa sababu sharia zake ni kinyume cha haki za binadamu. Alisema hoja ya kuwa mahakama hiyo itashughulikia mirathi, hija na ndoa tu, ni ulaghai ili iingizwe katika katiba, baadaye makadhi waue watu wasiokubali dini ya Kiislamu na kuangamiza Wakristo na Wayahudi na kuchinja Waislamu watakaoiacha dini yao. Alisema hivi sasa nchi haina Mahakama ya Kadhi, lakini Waislamu wanaoa, wanaolewa, wanapata mirathi na kesi zao za mirathi zinashughulikiwa na pia wanakwenda hija na kuhoji mahakama hiyo italeta mabadiliko gani katika masuala hayo yanayodaiwa kuwa itayashughulikia. Aidha, Mtikila alisema kitendo cha baadhi ya Waislamu kupinga ziara ya Papa ni kutofahamu kwamba mbali ya Vatican kuwa makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, pia ni nchi huru ingawa ipo ndani ya nchi ya Italia. Alifafanua kuwa Vatican ni sawa na Swaziland na Lesotho ambazo zimezingirwa na nchi ya Afrika Kusini. Alisema Papa atatembelea Tanzania kiserikali sawa na kiongozi mwingine wa nchi na kwa kuwa kuongoza kanisa ni huduma ya kiroho, hawezi kuiweka roho pembeni anapokuwa katika ziara ya kiserikali. Akifafanua kauli zake za awali kuhusu kupinga kwake utaratibu unaotaka kutumiwa kuanzisha Mahakama ya Kadhi, Mtikila alikanusha kutamka kuwa Uislamu ni ugaidi na kusisitiza kuwa Mahakama ya Kadhi ndiyo chombo cha ugaidi ndiyo maana hata baadhi ya nchi za Kiislamu zinaikataa. “Uislamu wa Watanzania usio na ukatili wa Mahakama ya Kadhi hauwezi kuitwa ugaidi kamwe,” alisisitiza. Kwa upande mwingine, alisema mbinu ya kamati inayotetea mali za Waislamu iliyotangaza azma yake ya kumkata kichwa, ni hasira tu, kwa kuona pesa walizokuwa wanataka kupewa hazitakuwepo na suala hilo halitazungumziwa bungeni wala serikalini kwa kuwa lipo mahakamani. Aliongeza kuwa, yeye hawakatalii Waislamu kuabudu, lakini si kuliiingiza suala hilo la kidini ndani ya katiba. Kauli hiyo ya Mtikila inakuja wakati taifa likipita katika kipindi kigumu cha msigano wa hoja zinazokinzana kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi jambo lililogusa hisia za makundi mbalimbali ya Wakristo na Uislamu kiasi cha kutishia amani. Baadhi ya kauli za waumini wa dini hizo mbili, ndizo ambazo kwa upande fulani zilisababisha taasisi za dola kuamua kuingilia kati na kuchukua hatua za kisheria.

1 comment:

Anonymous said...

bwana yesu asifiwe ndugu zangu, mi nadhani wanaomwona mchungaji mtikila mchonganishi wao ndio wanataka kuvuruga hali ya hewa tanzania, ukiangalia kiukweli nchi ya tanzania sio nchi ya kiislam, mungu atawaadhibu wote wanaotaka kuingiza mambo ya ajabu ktk katba ya tz, hata kama ni kikwete maana yeye nae ni mwanadamu tu.

Ruthie