Wednesday, November 28, 2007

Mahakama Kuu yasitisha mjadala wa Mahakama ya Kadhi

*Yasema Bunge, Serikali haviruhusiwi kujadili suala hilo
*Ni mpaka kesi iliyoko Mahakamani itapotolewa uamuzi
*Mch. Christopher Mtikila aibwaga serikali mahakani kwa mara nyingine
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri kwa Tume iliyoundwa Rais Jakaya Kikwete kushughulikia suala la uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi nchini isiendelee na shughuli zozote kuhusiana na mahakama hiyo hadi uamuzi wa kesi ya kupinga uanzishwaji wa mahakama hiyo utakapotolewa.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Salum Masati ambaye alitoa amri pia Bunge na Serikali visizungumzie suala la Mahakama ya Kadhi kwa kuwa suala hilo liko mahakamani.
Oktoba 18 mwaka huu, Mchungaji Christopher Mtikila wa Kanisa la Full Salvation alifungua kesi ya kikatiba katika mahakama hiyo kupinga mpango wa serikali wa kuidhinisha kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini.
Katika kesi hiyo namba 80 ya mwaka 2007, Mtikila ambaye anajitetea mwenyewe aliiomba Mahakama kumwamuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusitisha mpango wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi kwa kuwa unakiuka Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mtikila pia aliiomba mahakama kuziwajibisha kisheria Wizara ya Sheria na Katiba, Tume ya Mabadiliko ya Sheria na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushiriki katika kufanikisha mpango huo.
Alisema kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi nchini ni kinyume cha vifungu 107 A,3,9, (a) (f) na (h) 13 na 19 vya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania vinavyozuia kuanzishwa kwa chombo chochote cha sheria chenye misingi ya kibaguzi.
Hati ya mashitaka iliyowasilishwa katika mahakama hiyo, imeitaka mahakama pia kukifuta Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sera yake ya kuanzisha mahakama hiyo huku kikijua kuwa ni kinyume na kifungu cha 20 (2) (a) (i) cha Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari nane mwakani itakapoendelea kusikilizwa tena.
Mapema mwezi huu, Rais Kikwete akizungumzia suala la Mahakama ya Kadhi, kwa mara ya kwanza, alisema hoja ya Kadhi haikuanzishwa na yeye wala CCM bali wapinzani.
Rais Kikwete alisema suala la Mahakama ya Kadhi lilianzishwa bungeni kwa hoja ya binafsi na aliyekuwa Mbunge wa Temeke kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema ambaye alitaka Bunge lijadili na kukubali kuanzishwa kwa mahakama hiyo nchini.
Alisema baada ya Mrema kumaliza muda wa mbunge wake na kuhamia Chama cha Tanzania Labour (TLP, hoja hiyo ilipelekwa tena bungeni na aliyekuwa mbunge wa Moshi Vijijini kupitia chama hicho, Thomas Ngawaiya.
“Mara zote hizo, kwa busara ya aliyekuwa Spika wa Bunge, Pius Msekwa na Waziri Mkuu, Fredrick Sumaye hoja hiyo ilipelekwa kwanza kwenye kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyokuwa ikiongozwa na Arcado Ntangazwa na Baadaye Athumani Janguo kwa uchunguzi wa kina,” alisema Rais Kikwete.
Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete alisema sio sahihi kulihusisha suala hilo la Kadhi na serikali yake wala ilani ya CCM na kwamba ni vema jamii ikasubiri hadi tume hiyo inayotarajiwa kumaliza kazi yake mwezi Februari mwakani itakapotoa tamko.
“Tuwe na subira ili tuipe tume hiyo fursa ya kutafakari jambo hilo nyeti bila shinikizo lolote,” alisema Rais Kikwete na kuahidi kuwa Serikali haitafanya uamuzi wowote kuhusu jambo hilo bila kuwashirikisha wananchi wote.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati wa sherehe ya kumsimika Mkuu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa. Sherehe hizo zilifanyika katika Kanisa la Kuu la Azania Front, jijini Dar es Salaam.

No comments: