Msafara wa magari kuelekea Loliondo kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile.
WAKATI Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda akieleza kuwa ameagiza Serikali ya Mkoa wa Arusha kuzuia tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapile, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Raymond Mushi amesema ni vigumu kusitisha huduma hiyo.
Mushi alisema pamoja na kutopata barua yoyote inayomwagiza asimamishe huduma za mchungaji huyo, ni vigumu katika mazingira yaliyopo katika Kijiji cha Samunge, Loliondo kufanya hivyo ikizingatiwa kwamba hivi sasa kuna maelfu ya watu hasa wagonjwa walioko hapo na wengine wakiendelea kumiminika.
“Hata mimi nimemsikia Waziri Dk Mponda, lakini siwezi kuanza kufanya kazi bila kupokea barua na maelekezo. Lakini hili jambo ni gumu kidogo kwani watu bado wanakwenda na tukipata barua tutajua jinsi ya kukabiliana na hali hii,” alisema Mushi.
Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa alisema kama akipokea barua na maelekezo watakaa na watendaji wengine kuona ni jinsi gani wataweza kukabiliana na hali ya Loliondo. “Pale yule mchungaji anasema anatoa huduma ya tiba na lile jambo ni la kiimani ndiyo sababu anasema wenye imani watapona sasa sidhani kama wataalamu wakipeleka dawa ile maabara wataona kitu,” alisema Mushi.
Mbali ya Kaimu Mkuu wa Mkoa kuonyesha wasiwasi wake juu ya utekelezaji wa agizo hilo la Waziri, Mbunge wa Ngorongoro (CCM), Saning’o ole Telele amepinga hatua hiyo ya serikali kutaka kuzuia kwa muda tiba hiyo akisema badala yake, inapaswa kusaidia watu kupata tiba.“Sikubaliani na Waziri wa Afya kuzuia tiba eti sijui mchungaji ajisajili kwanza.Tunachoomba ni serikali kusaidia watu wafike Ngorongoro, Samunge na kupata tiba katika mazingira bora,” alisema Telele.
Telele alisema watu wengi wamepona kwa kunywa dawa hiyo, hivyo Serikali inapaswa kuomba msaada wa mashirika mbalimbali kama Msalaba Mwekundu yafike kuweka mahema na kutoa huduma ya kwanza.Jana, Dk Mponda alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, kuzuia mara moja matibabu ya magonjwa sugu yanayoendeshwa na Mchungaji Mwasapile hadi serikali itakapojiridhisha ubora na usalama wake kwa watumiaji.
Akizungumzia tamko hilo la Waziri, Msaidizi wa Mchungaji Mwasapile, Paulo Dudui alisema amepotoshwa kwa vitu vingi: "Kwanza siyo kweli kuwa wagonjwa wote wanatumia kikombe kimoja na pia si kweli kwamba wanatumia maji ya mto."
"Kila mgonjwa anatumia kikombe chake na tuna vikombe zaidi ya 100 ambavyo baada ya kutumika vinaoshwa na wagonjwa wanaona na pale kuna maji ya bomba yanayotoka katika chanzo cha maji cha Samunge.”Lakini Dudui alisema kama wakipokea maelekezo ya serikali kuhusu tiba watakaa na kujadiliana kwani wanaamini huduma ambayo wanatoa ina manufaa makubwa kwa watu na siyo uganga.
“Mchungaji mwenyewe atasema nini cha kufanya ila Waziri kapotoshwa. Hapa serikali ilitakiwa kusaidia huduma kutolewa na siyo kuzuia,” alisema Dudui.Katika hatua nyingine Dudui alisema kwamba mtoto mmoja alifariki dunia jana katika eneo hilo kutokana na kuchelewa kupata tiba.
Source: http://www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment