Mtume na Nabii Josephat Mwingira wa Kanisa la Efatha amemuombea mabaya Mchungaji Ambikile Mwasapile anayetoa tiba ya magonjwa sugu katika eneo la Samunge, Loliondo kwamba anapaswa kulaaniwa hadi kufa kutokana na kutoa huduma hiyo.
Mwingira alisema hayo katika mahubiri ya ibada ya Jumapili aliyoyatoa katika Makao Makuu ya Kanisa hilo lililoko Mwenge jijini Dar es Salaam. “Imeandikwa katika Biblia kwamba,ukipewa bure nawe toa bure. Iweje yeye anauza dawa hiyo, ikiwa Mungu amesema aponye watu. Hakuna sababu ya kuwatoza fedha yoyote wagonjwa.
“Hizi ni roho za kishetani zinazotaka kuwaangusha walio wengi ambao hawamjui Yesu Kristo kwani haiwezekani mtu atumiwe na Mungu halafu hata siku moja asimtaje Yesu. Asitumie Biblia hata kuwahubiria watu wamtumaini muumba wao,”alisema Mwingira.
Mwingira alisema huduma hiyo ni uongo na kwamba haina tofauti na Deci iliyokuja kiujanja ujanja na kuteka watu wengi baadaye walijutia maamuzi yao. “Kama mpakwa mafuta wa Bwana niliyeitwa kwa kusudi lake.
Nailaani Loliondo ife pamoja na Mchungaji wake na itoweke kama Deci ilivyotoweka,” alisema Mwingira. Mwingira alisema Mchungaji Mwasapile ni mwongo, anataka kuwadanganya watu na kuwapoteza kiimani.
Alisema kama alivyoilaani Deci na ikafa, anailaani huduma ya Loliondo ili ife kwa kuwa mchungaji huyo ni roho ipotezayo, inayotaka kuwateka watu walioko gizani na kuwaangamiza. Alisema baadhi ya viongozi tayari wamepigwa ngwara na roho hiyo na kunywa dawa, bila wao kujijua.
“Sitakubali kuendelea kuona roho hiyo ikipoteza watu. Nailaani itoweke Loliondo na iangamie kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,”alisisitiza. Mwingira alisema haiwezekani kwa mtu aliyeitwa na Mungu kuwahudumia watu wake, baadhi ya watu hao wafe kwenye huduma yake.
“Ni wagonjwa wangapi wamepelekwa kule na wengine wamefariki nyumbani kwake kabisa na wengine njiani, je mlishawahi kujiuliza? alihoji Mwingira. Mwingira alitoa kauli hiyo siku chache baada Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kulieleza gazeti hili:"Miujiza haiji kwa urahisi hivyo na watu kuponya kiasi hicho, huenda wanaweza kuponywa kwa ‘Illusion’ na baade ikaleta madhara."
Alisema cha msingi watu wanapaswa kuwa makini na serikali pia kwa sababu, wingi wa watu kuponywa huenda baadaye ukaleta vifo vingi zaidi kutokana na dawa yenyewe.
Pengo alisema: “Ninachoamini miujiza haiji kwa urahisi na watu wakaponywa kiasi hicho kwa mara moja, huenda ikawa ni kuponya kwa ‘illusion’ na baadae watu wakapata madhara makubwa.
“Ila sina jibu la kutoa kuhusu uponyaji huo, nabaki tu kushangaa nayayotendeka kwa Mchungaji huyo hadi kufikia watu kuamini kiasi hicho,”alisema. Pengo alisema huenda akawa ameamua kutumia njia hiyo akawavuta hata wa waumini waingie kwenye imani yake na kuacha dini zao.
Source:mwananchi.co.tz
2 comments:
MZEE WETU MWACHE BABU ATIBU USIMWINGILIE, AMEKUBALIKA
MZEE WETU MWACHE BABU ATIBU USIMWINGILIE, AMEKUBALIKA
Post a Comment