Akizungumza kwa tabu na gazeti hili kutokana na kuzungukwa na kadamnasi iliyokuwa ikihitaji kuponywa, mchungaji huyo alisema kuwa kabla ya kufika katika kijiji hicho Mei, mwaka 2009, alikuwa akiishi mkoani Manyara akitangaza Injili kama mhubiri wa kawaida na baadaye alistaafu.
Mchungaji Mwasapile ambaye ametazamwa na watu kama ‘Nabii mpya’ amekuwa akitoa tiba hiyo kwa staili ya aina yake ambapo mgonjwa anatakiwa anywe maji yenye dawa hiyo hapo hapo kwa kutumia kikombe kidogo.
Aidha, maajabu mengine ni baadhi ya watu kusema kuwa, mti ambao mchungaji huyo anautumia kutibia unajulikana lakini tatizo bila mkono wake kuchimba mizizi yake hakuna kinachoweza kufanyika.
ALIVYOPATA UTABIBU
Mchungaji Mwasapile anasimulia ilivyokuwa hadi akaoteshwa kuhusu mti huo, anasema:
“Ilikuwa mwaka 1999 nikiwa Babati, kuna siku nikiwa nimelala ilinijia sauti ndotoni. Ikaniamuru kuwa, watu wengi wa Kijiji cha Samunge wanakufa na Ukimwi, kisukari presha na magonjwa mengine mbalimbali.
“Sauti hiyo ikanitaka niwatibu watu hao ili waweze kuendelea na maisha yao kama kawaida. Lakini mimi nilipuuzia sauti hiyo na kuendelea na mambo yangu.
“Hata hivyo, mwaka 2009 sauti hiyo ilinijia tena ndotoni ikinipa maagizo yale yale, lakini safari hii ikanipa onyo kuwa, nisipotimiza agizo hilo nitaadhibiwa.
“Niliamka na kutii, nilikuja hapa kijijini na kwenda hadi kwenye mti nilioelekezwa kuwa ndiyo tiba ya magonjwa yote haya.
“Nilianza kazi hiyo mara moja na tangu siku hiyo umati mkubwa wa watu unamiminika kijijini hapa kadiri wanavyopata habari zangu kutoka kwa watu waliofanikiwa kupona,” alisema mchungaji huyo huku wagonjwa wakiona namchelewesha kutoa tiba kwao.
Hata hivyo, mchungaji huyo alifafanua kuwa, ikitokea amekufa leo, Mungu atamtoa mtu mwingine kufanya kazi hiyo na anaweza akawa si ndugu wala mtoto wake.
Alipoulizwa idadi ya wagonjwa aliowatibu, mchungaji huyo alisema ana uhakika na watu 30,000 huku akisema gharama yake ni shilingi 500 tu kama alivyoagizwa kwenye ndoto. Hivi sasa zaidi ya watu 200,000 wanatibiwa hapo.
MUME NA MKE WAFUMANIANA
Mchungaji huyo anapoendelea na tiba hajui kinachofanyika nje ambako kuna umati wa watu.
Mwandishi wetu alishuhudia watu wawili, mke na mume kila mmoja akimuuliza mwenzake amefikaje kijijini hapo bila kutoa taarifa.
Mwanaume aliyejitambulisha kwa mwandishi wetu kwa jina la Isaya John Jeena alisema alikuwa na mpango wa kwenda kwa mtaalamu huyo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya muda mrefu (hakuyataja).
“Nilikuwa safarini Nairobi, nikapanga nikirudi nije huku, sasa, nashangaa kumkuta mke wangu, kwa nini aje bila kunitaarifu mimi mumewe?” Alihoji Jeena.
VIGOGO NAO WAMO
Tangu aanze kutibu watu, idadi kubwa ya vigogo, wakiwemo wana siasa, maofisa wa serikali na wafanyabiashara wa ndani ya nchi wamekuwa wakimiminika kupata tiba.
Mbali na makundi hayo, baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali mbalimbali za mikoa, ikiwemo Kilimanjaro Christian Medical Center (KCMC) ya mjini Moshi, wamekuwa wakiomba ruhusa kutoka wengine wakitumia njia ya kutoroka ili wakatibiwe kwa mchungaji huyo.
Kwa sasa katika Kijiji cha Samunge, watu waliofurika ni wa kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Singida, Mbeya, Manyara , Dar es Salaam na nchi jirani za Kenya na Uganda.
Magari mengi ya kifahari ya vigogo yalionekana mwishoni mwa wiki iliyopita yakiwa yamezungukwa na askari wa FFU wakishirikiana na mgambo kuhakikisha kuwa hakuna mwandishi wa habari ama mtu yeyote atakayeruhusiwa kupiga picha eneo hilo.
Mabasi kutoka Dar, Arusha na Moshi yamekuwa yakianzisha ‘ruti’ za kwenda Loliondo moja kwa moja kutoka katika miji hiyo.
Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya watu wanaokwenda eneo hilo huduma ya vyakula imepanda ambapo wageni wanaofika hapo wamekuwa wakilazimika kubeba vyakula vyao baada ya kujikuta wakiuziwa sahani moja ya chakula kwa shilingi kati ya 5,000 na 10,000.
Awali kulikuwa na watu walikuwa wakichinja mbuzi 50,000 kwa siku lakini sasa wamezuiliwa kutoa huduma hiyo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, katika eneo hilo hakuna idadi kubwa ya vyoo vya kujisaidia, hivyo watu kujikuta wakienda vichakani.
Aidha, imebainika kuwa, hata ‘madada poa’ wanaofanya biashara ya kuuza miili katika maeneo mbalimbali ya starehe mjini Arusha, nao wamepungua baada ya wengi wao kutimkia kwa mchungaji huyo kutokana na kuamini wana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Usafiri wa kutoka mjini Arusha hadi Samunge umepanda ghafla kutoka shilingi 35,000 kwenda na kurudi hadi kufikia shilingi 150,000 kwa magari yanayomudu kufika huko kwani barabara ni mbovu.
Ingawa hakuna taarifa rasmi zilizothibitisha kuwa mgonjwa wa Ukimwi amepona lakini Lilian John (30) mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa aligundua ana maambukizi ya Ukimwi mwaka 2006 baada ya kufiwa na mume na mwanaye.
Alisema mwaka 2009 alibahatika kuonana na mchungaji huyo wakati huo alikuwa siyo maarufu na kumpatia dawa hiyo.
Baada ya kuitumia kwa wiki mbili alikwenda kupima katika Hospitali Teule ya Wasso ambapo madaktari walithibitisha kuwa, hana Virusi vya Ukimwi.
SERIKALI INASEMAJE?
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima amesema serikali haioni sababu ya kuzuia watu kupata tiba za mchungaji huyo kama hazina madhara kwa afya zao.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni amesema wizara yake imeiagiza ofisi ya mganga mkuu wa mkoa ifanye utafiti wa kimaabara juu ya dawa hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Taifa ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili kubaini ukweli wa kisayansi na watatoa taarifa uchunguzi ukikamilika.
Source: Globalpublisherstz.com
No comments:
Post a Comment