Tuesday, September 28, 2010

Kakobe na uchaguzi 2010


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zakary Kakobe ametangaza kutokuwepo kwa ibada katika makanisa yake kote nchini siku ya Jumapili ambayo ni maalumu kwa ajili ya kupiga kura kumchagua rais, mbunge na diwani.

Alitangaza uamuzi huo jana katika ibada maalumu ambayo ilikuwa kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa waumini wa Kanisa lake.

Alisema amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Wakristo wengi ndio wanaokosa fursa ya kwenda kupiga kura kutokana na siku hiyo ya kupiga kura kwenda makanisani.

Katika ibada hiyo, Askofu Kakobe alitaja vikwazo vitano ambavyo vinakwaza watu kwenda kupiga kura na kati ya hivyo alisema vikwazo viwili vinawakwaza Wakristo wanaosali siku ya Jumapili ambayo imekuwa inatumiwa hapa nchini kama siku ya kupiga kura.

Akitoa na somo la Mkristo na Uchaguzi Mkuu, Askofu Kakobe alisema uamuzi wa kufanya uchaguzi siku ya Jumapili, huchangia Wakristo kutopiga kura.

Alisema umefika muda kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kubadili siku hiyo kama zilivyofanya nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Rwanda, Msumbiji, Burundi na Malawi ambazo uchaguzi unafanyika siku zingine na sio siku za ibada.

"Nadhani kuna watu wanafurahi Wakristo wengi wasipige kura, safari hii tumefanya juhudi nyingi; lakini NEC imeng'ang'ania, na hatuwezi kuacha kwenda kupiga kura kwani tunaweza kuchaguliwa kiongozi asiyefaa tukajutia kwa miaka mitano.

"Hivyo natangaza rasmi siku hiyo ya uchaguzi hakutakuwa na ibada katika makanisa yote ya FGBF, milango ya makanisa hayo siku hiyo ifungwe na ibada ya siku hiyo ifanyike siku ya Jumamosi," alisema askofu huyo.

Pia alitoa mwito kwa maaskofu wa makanisa mengine kuiga mfano wake ili kutoa fursa kwa waumini wao kwenda kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Aliwaomba viongozi wengine wa makanisa kuwa hata kama wakishindwa kuzuia ibada siku hiyo, ni vyema wakawahamasisha waumini wao ili wajitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura siku hiyo.

Alidai katika uchaguzi mkuu uliopita, Watanzania milioni 5 sawa na asilimia 30 ya waliojiandikisha kupiga kura hawakujitokeza kupiga kura wengi wao wakiwa Wakristo.

Alitaja kikwazo kingine kinachochangia Wakristo wasiende kupiga kura siku hiyo kuwa ni kudhani kuwa rais au mbunge wanachaguliwa na Mungu.

Kiongozi huyo wa kidini aliwataka Wakristo kuachana na dhana hiyo aliyoita potofu na akawambia kuwa Mungu amewapa uhuru wanadamu kuchagua viongozi wa kuwatawala.

Alisema Mungu kamwe hawachagulii wanadamu kiongozi bali huwaacha wachague wenyewe na akawaonya waumini wake kuwa wakiacha kwenda kupiga kura, wanaweza kupata kiongozi mbovu na hata kama wakiomba juu ya kiongozi huyo mbovu kamwe Mungu hatajibu maombi yao.

Askofu Kakobe pia alitaja kikwazo kingine kinachowafanya watu wasiende kupiga kura kuwa ni kuwepo mawazo potofu miongoni mwa watu kuwa kura moja haina athari.

Aliwataka watu kuachana na mawazo hayo kwani kwa sheria za Tanzania mgombea anatangazwa kwa wingi wa kura.

Hivyo alisisitiza kuwa kitendo cha mtu kutojitokeza kwa kudhani kuwa kura yake haina thamani, aachane na msimamo huo.

Source: habarileo

No comments: