Tuesday, September 28, 2010

Mzee wa Upako

Haruni Sanchawa na Gladness Mallya
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi – Utashinda, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako usiku wa kuamkia jana alivamiwa kanisani na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kumteka kwa muda kabla ya kumpora mamilioni ya shilingi.

Gazeti hili lilifika eneo la tukio kanisani kwake, maeneo ya Ubungo Kibangu na kufanikiwa kupewa taarifa ya jinsi ujambazi huo ulivyofanyika ambapo mtoa habari alisema kundi la majambazi lilivamia kanisa hilo usiku.

“Kundi hilo la watu lilifika maeneo hayo majira ya saa tisa na kuwateka walinzi ambao walikuwepo hapo hadi saa kumi na moja alfajiri kuamkia jana,” alisema mtoa habari wetu kwa sharti la kutoandika jina lake gazetini.

Imedaiwa kuwa kabla ya kufanya uvamizi huo, mlinzi wa kanisa hilo (jina tulihifadhi kwa sababu za kiusalama ), alivamiwa na kufungwa kamba na baadaye kunyang’anywa bunduki na majambazi hao.

Chanzo chetu hicho cha habari kiliongeza kuwa baada ya kumkamata mlinzi huyo, majambazi hao walienda moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Lusekelo na kumteka kwa muda kabla ya kumuamuru atoe pesa alizokuwanazo vinginevyo wangemuua.

Habari zinasema Mzee wa Upako aliamua kutoa pesa ambazo inadaiwa ni zaidi ya shilingi milioni 20 ambazo inaaminika zilitokana na sadaka za waumini wake. Kiongozi huyo wa kanisa hakujeruhiwa.

Habari za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa Mchungaji Lusekelo hakai kanisani hapo na kwamba ni mara chache hulala katika nyumba hiyo ya ibada hasa anapokuwa na kazi maalum.

Gazeti hili lilipowasiliana na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Elias Kalinga alikiri kutokea kwa tukio hilo na amedai kuwa hadi sasa watu wawili wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.

“Uzoefu unaonyesha kuwa kuna baadhi ya makampuni ya ulinzi hapa nchini yana watumishi ambao si waaminifu, natoa wito kwa wamiliki wa makampuni binafsi ya ulinzi kabla ya kuajiri mlinzi , yahakikishe uaminifu wake kwanza,” alisema Kalinga.

Aliongeza kuwa kampuni za ulinzi zinalinda mamilioni ya mali za watu lakini anashangazwa kuona baadhi ya walinzi wao wanauza siri za muajiri wao kwa watu wasio raia wema.

Waandishi wetu walifanya jitihada za kumtafuta Mzee wa Upako ili kusikia kauli yake juu ya tukio hilo bila mafanikio.
Kwa mujibu wa walinzi waliokutwa kanisani hapo ambao hawakupenda majina yao kuandikwa gazetini, kiongozi huyo alikuwa amekwenda nyumbani kwake Mbezi kupumzika.

Source: www.globalpublishers.info

No comments: