Thursday, July 2, 2009

Mahakama ya Kadhi yakoroga Waislamu, Wanasiasa

SIKU moja baada ya serikali kutoa msimamo wake wa kutounda Mahakama ya Kadhi na badala yake kuzijumuisha Sheria za Kiislamu kwenye sheria za nchi, baadhi ya Waislamu na Wanasiasa wamekuja juu na kudai kuwa imeshindwa (serikali) kutekeleza ahadi iliyotoa wakati wa uchaguzi mkuu wa 2005.
Wadau mbalimbali kutoka taasisi za kidini, wanasiasa na wasomi waliambia gazeti hili jana kwamba, uamuzi huo wa serikali unakwenda kinyume na kilichomo katika ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo ina kipengele kinachoruhusu kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Juzi Waziri wa Sheria na Katiba, Mathia Chikawe aliliambia Bunge Tanzania haitaunda Mahakama ya Kadhi badala yake sheria za Kiislamu zitaingizwa katika sheria za nchi ili zitumike katika mahakama ya kawaida.
Katibu wa Kamati ya Kutetea Mali za Waislamu Tanzania, Sheikh Khalifa Khamisi alisema kamati hiyo inatarajia kupinga hatua ya serikali kufuta ombi la kuanzishwa Mahakama ya Kadhi na kutoa tamko lake rasmi Jumapili hii.
Sheikh Khamisi aliliambia gazeti hili jana kuwa, hoja ya serikali kwamba yenyewe haina dini ndiyo maana imeamua kupinga hatua hiyo, siyo sahihi.
"Serikali imesema kuwa haina dini, kwa nini basi iwazuie Waislamu kuanzisha mahakama ambayo wanaitambua kwa mujibu wa imani ya dini yao?"alihoji Sheikh Khamisi na kuongeza:
"Tena mambo haya wanafanyiwa Waislamu tu na sio dini nyingine hasa baada ya maaskofu kutishia kujitoa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kufutiwa misamaha ya kodi," alisema Khamisi.
Alisema kamati yake inaipinga vikali kauli hiyo ya serikali iliyotolewa juzi bungeni na Waziri wa Sheria wakati akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2009/10.
"Serikali inawaogopa sana maaskofu na kuwadidimiza Waislamu hata pale wanapokuwa na haki sawa na wengine na imekuwa ikiwapuuza na kuwasahau," alisema.
Alidai kuwa wameziona taasisi kadhaa za dini ya kikristo zikifanyabiashara kwa kivuli cha kutoa huduma za kiroho, lakini serikali imekaa kimya tena.
“ Tena baadhi ya makanisa yanafanya mambo kinyume na taratibu za nchi, serikali imeshindwa kuyakemea, lakini wanaliona hili la Waislamu ambao wanyonge kuwa halifai," alisema Sheikh.

Alisisitiza kuwa suala la kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi ni haki ya Waislamu kama ilivyo katika nchi nyingine ambazo wamepewa uhuru kamili wa kuabudu wanachoamini.
Nalo Baraza kuu la Waislamu Tanzania, (Bakwata) limesema litatoa tamko rasmi kuhusu kauli ya serikali kufuta mpango wa kurudisha mahakama hiyo.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila aliliambia gazeti hili ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es Salaam jana kwamba, tamko hilo litatolewa baada ya Mufti Mkuu, Sheikh Issa bin Shaaban Simba kukutana na baraza la Masheikh, ili kujadili suala hilo.
“Tamko rasmi la Bakwata kuhusu kufutwa kwa mpango wa kurudisha Mahakama ya Kadhi litatolewa na Mufti kesho (leo) saa nne asubuhi baada ya kukutana na Baraza la Masheikh,” alisema Sheikh Lolila.
Sheikh Lolila alisema kuwa, Baraza la Masheikh wa mkoa wa Lindi limemteua, Sheikh Mohammed Said Mushangani kuwa kaimu Sheikh wa Mkoa wa Lindi ili kuziba pengo la Marehemu Sheikh Gorogosi aliyefariki kwa ajali ya gari hivi karibuni mkoani humo.
Kwa mujibu wa Sheikh Lolila, Sheikh Mushangani atashika wadhifa huo hadi uchaguzi utakapokamilika mwezi Agosti.
“Kwa sasa tuko kwenye uchaguzi ambao utakamilika mwezi Agosti, hapo ndipo Lindi watakuwa na Sheikh wao rasmi,” alisema Lolila.
Wakati huo huo aliyekuwa Mwenyekiti wa Bakwata, Sheikh Khamis Mataka alisema kauli ya serikali kuizima hoja ya Mahakama ya Kadhi ina mapungufu mengi na kwamba, wanaisubiri katika mkutano ambao iliahidi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu kujadiliana kuhusu jambo hilo.
"Tunafanya busara sana kuisubiri serikali kwa kuwa imeahidi kukutana na viongozi wa dini ya kiislamu. Ndipo sisi wanazuoni tutakapotoa hoja zetu na kuweka wazi mapungufu ya maamuzi hayo ya kuifuta mahakama,"alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza Kuu, Jumuiya na Taasisi zote za Kiislamu Tanzania, Ramadhani Sanze alisema wameisikia kauli hiyo ya serikali kupitia kwa waziri wake ya Sheria na katiba, Mathias Chikawe.
Alifahamisha kuwa masheikh wanafanya mkutano wa siku mbili kujadili suala hilo na kwamba, watatoa tamko lao Ijumaa wiki hii.
Alisema hawana haja ya kuyafanya mambo hayo kuwa marefu, isipokuwa serikali itaona ni nini Waislamu wanahitaji kifanyike kwa mujibu wa imani ya dini yao na kuridhika nacho.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kutotekeleza moja ya vipengele vya Ilani ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ambayo inaeleza kuwa itaruhusu kuwepo na Mahakama ya Kadhi nchini.
Profesa Lipumba aliliambia gazeti hili jana kuwa moja ya vipengele katika Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, ilikuwa ni pamoja na kuruhusu kuwepo kwa mahakama hiyo; hivyo kitendo cha serikali kushindwa kutekeleza ahadi hiyo, rais Kikwete anatakiwa awajibike kwa kuwaomba radhi Watanzania waliompigia kura.
"Ni jambo ambalo lipo wazi kabisa, kwa sababu ilani ya uchaguzi inajadiliwa na kupitishwa na chama, hivyo kutokana na hili serikali imeonyesha ni jinsi gani ilivyowadanganya Watanzania. Huu ni 'usanii' kabisa wanaonyesha kuwa hawako makini katika masuala mazito kama hili," alisema Lipumba na kuongeza:
"Wananchi humchagua mtu kutokana na sera zake, hivyo wapo watu walioichagua CCM kwa sababu tu katika kampeni zao walisema watatekeleza suala la Mahakama ya Kadhi".
Katika hotuba yake juzi Chikawe alisema mchakato wa kufikia hatua ya kuzijumuisha sheria hizo za Kiislamu kwenye sheria za nchi lazima upate maoni kutoka kwa madhehebu yote ya Kiislamu nchini.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alilieleza gazeti hili jana kuwa Ilani ya CCM katika uchaguzi wa mwaka 2005, ilisema itashughulikia kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi kama moja ya ajenda kubwa za kuwashawishi wapiga kura.
"Hoja hii ilitumiwa na CCM mwaka 2005 na iliungwa mkono na mmoja wa maaskofu wa Kanisa Katoliki ambaye alitamka kuwa Rais Kikwete ni chaguo la Mungu, hivyo watu wengi walimchagua" alisema Ruhuza na kuongeza:
"Siyo kwamba tunalazimisha kuwepo kwa Kadhi Mkuu, lakini kama suala la Mahakama ya Kadhi lilitumiwa katika ilani ya uchaguzi, basi litekelezwe".
Hoja ya kuwepo kwa mahakama ya kadhi ilianzishwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu lakini ilizimwa, baada ya miaka mitatu iliyopita sakata hilo lilifufuliwa tena na kuwagawa wanasiasa na wananchi katika makundi mawili (wanaounga mkono na wanaopinga).
Wako waliounga mkono na wengine waliipinga kwa maelezo kwamba itasababisha vurugu na mgawanyiko katika jamii.
Source: Mwananchi

No comments: