Wednesday, July 1, 2009

Mahakama ya Kadhi yayeyuka

SERIKALI imetoa kauli ya kusitisha kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini na sasa mfumo mpya wa sheria wa kukidhi haja ya jamii ya Waislamu, utaingizwa katika sheria za nchi katika mwaka huu wa fedha. Sambamba na hilo, imetangaza nia ya kubadilisha mfumo wa kujiunga na Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Law School), ambapo si wanafunzi wote waliomaliza shahada ya kwanza ya Sheria watakaoruhusiwa kujiunga nayo, huku ikiweka wazi idadi ya talaka zilizotolewa mwaka jana na mzigo wa kesi ‘unavyoiumiza’ Mahakama nchini. Kauli hiyo ya serikali ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, wakati alipowasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, yanayofikia Sh bilioni 107.6. Kwa mujibu wa Chikawe, badala ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi katika mfumo wa mahakama nchini, sasa serikali itaingiza misingi ya dini ya Kiislamu katika mfumo wa sheria za nchi. Uamuzi huo umefikiwa baada ya kumalizika kwa utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria kuhusu uanzishwaji wa mahakama hiyo nchini au la. “Mapendekezo ya Tume ya Kurekebisha Sheria yamepokewa na kufanyiwa kazi na kamati ya wataalamu wa sheria iliyoundwa ambayo pia imetoa mapendekezo yake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Chikawe. Alifafanua kuwa baada ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata mapendekezo ya kamati ya wataalamu, imeanzisha mchakato wa kukusanya maoni kutoka kwa viongozi wa madhehebu yote ya dini ya Kiislamu. “Nia ya mchakato wa kukusanya maoni hayo ni kupata orodha ya misingi ya dini ya Kiislamu hususan inayohusu sheria binafsi, kwa madhumuni ya kuihuisha misingi hiyo katika sheria za nchi yetu,” alisema Chikawe. Kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa na Chikawe bungeni wa kuihuisha misingi hiyo ya dini ya Kiislamu katika sheria za nchi, viongozi wa dini wakishakubaliana kuhusu misingi hiyo, Waziri wa Sheria atatoa tamko litakalotokana na makubaliano ya viongozi hao. “Baada ya hatua hiyo, tamko hilo la Waziri litakuwa sheria itakayotambuliwa na mahakama zote nchini,” alisema Chikawe. Kwa uamuzi huo, Chikawe alisema haki zote binafsi za Waislamu zitalindwa na kusimamiwa na serikali na kutekelezwa na mahakama. Kuhusu uamuzi huo na misingi ya Katiba, Chikawe alisema utaratibu huo hautaathiri misingi ya Katiba ya nchi na kutoa mfano kwa Afrika Kusini ambayo ina waumini wengi wa Kiislamu na inatumia utaratibu huo. Kuhusu Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo, iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chikawe alisema mwaka huu wa fedha, wizara inakusudia kufanya mabadiliko katika sheria iliyoanzisha taasisi hiyo. Baada ya mabadiliko hayo, watakaolazimika kudahiliwa nayo watakuwa wahitimu wa Shahada ya Sheria wanaokusudia kuwa mawakili wa kujitegemea tu na si wahitimu wote wa Shahada ya Sheria. Aidha, Serikali imejipanga kuwajengea uwezo mawakili wa serikali, wahasibu, wachumi, wahandisi na watu wa kada mbalimbali katika majadiliano, uandaaji, uandishi na usimamizi wa mikataba. Akizungumzia uendeshaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Chikawe alisema wakala huyo ameendelea kuboresha huduma zake na kwa mwaka wa fedha uliopita, alisajili talaka 73, ndoa 15,345, vizazi 938,775, vifo 105,482 na watoto wa kuasili 39. Chikawe hakusita kuonesha mzigo wa kesi uliopo mahakamani ambapo katika Mahakama ya Rufaa, kati ya kesi 2,659 zilizokuwapo, ni kesi 560 tu zilizosikilizwa na kumalizika. Katika Mahakama Kuu, kati ya kesi 18,805 zilizokuwapo kesi 9,590 zilisikilizwa na kumalizwa. Katika mahakama za mikoa 23 na za wilaya 100, kulikuwa na kesi 61,237 na kati ya hizo kesi 42,725 tu ndizo zilizosikilizwa na kumalizika. Katika mahakama za mwanzo, kati ya kesi 213,239, ni 151,200 ndizo zilizosikilizwa na kutolewa uamuzi. Baada ya hotuba hiyo, Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mbunge wa Chakechake, Fatma Maghimbi (CUF), aliitaka Serikali itoe ufafanuzi wa kwa nini mahakama haijatengewa fungu la fedha kama ilivyo mihimili mingine ya Dola, ili kuongeza uhuru wa mhimili huo. Maghimbi alisema hata Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wake na watendaji wa mahakama uliofanyika Bagamoyo, aliridhia kuwapo fungu hilo baada ya watendaji hao kumwasilishia ombi hilo rasmi. Hata hivyo, Spika Samuel Sitta, kabla ya kusomwa kwa hotuba za Chikawe na Maghimbi, alipokuwa akimkaribisha Jaji Mkuu Augustino Ramadhani bungeni, alisema bajeti ijayo, mahakama itatengewa fedha zake. Kuhusu Taasisi ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo, Maghimbi alisema taasisi hiyo ina matatizo makubwa mawili, likiwemo la kukosa wafanyakazi wa kudumu. Lingine kwa mujibu wa Maghimbi ni wanafunzi kukosa mikopo ambapo kumekuwa na hali ya kutupiana mzigo kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
source: habari leo

1 comment:

shilindeson said...

mbona comments zako na post zako nyingi unazungumzia mahakama ya kadhi, wewe ni mshabiki wa dini au blogger?