SHEIKH Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban bin Simba amesema kuwa hoja ya Mahakama ya Kadhi haijazikwa bali itaendelea kujadiliwa na serikali kwa msaada wa masheikh.
Mufti Simba ametoa kauli hiyo baada ya serikali kutangaza Juni 30 kuwa haitaunda Mahakama ya Kadhi na badala yake itatafsiri sheria za Kiislamu na kuzijumuisha kwenye sheria za nchi ili zitumike kwenye mahakama za kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba alisema walikutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam William Lukuvi juzi usiku na kukubaliana baadhi ya mambo ambayo yataharakisha kuundwa kwa mahakama hiyo.
“Tumekubaliana kwamba hoja ya Mahakama ya Kadhi haijazikwa, ila serikali inahitaji msaada wa masheikh katika suala hilo na sisi tumekubali kutoa msaada huo,” alisema Mufti.
"Hivyo jopo la masheikh litaundwa na serikali itaunda jopo lake la wataalamu halafu tutakutana, ili kuratibu mfumo ambao utatumika katika Mahakama ya Kadhi nchini.”
Hatua ya serikali kutangaza kuzika mpango huo wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi ilipingwa vikali na Waislamu ambao walidai CCM iliwahadaa wakati wa kampeni za mwaka 2005 na hivyo kusema hawatakiunga mkono chama hicho kwenye uchaguzi ujao na pia kupanga kuandamana Ijumaa ijayo.
Lakini Mufti Simba alisema kikao chao na Waziri Pinda, kilichohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 20, likiwemo jopo la masheikh aliloliteua kutoka madhehebu yote ya Kiislamu , wamekubaliana suala hilo liendelee kushughulikiwa.
"Niliandaa jopo la masheikh kutoka madhehebu yote nchini. Nashukuru kwa kuitikia wito wangu. Tulienda kwa Waziri Mkuu tukazungumza kwa mapana zaidi kuhusu Mahakama ya Kadhi na amekubali kuwa mahakama haijafa na mchakato unaendelea,” alisema Mufti Simba.
Alifafanua pia wamekubaliana na Waziri Pinda kwamba atazungumza bungeni kukanusha kauli iliyotolewa na Waziri Chikawe Juni 30 mwaka huu bungeni mjini Dodoma kuhusu uamuzi wa kuzika hoja ya mahakama hiyo.
Mahakama ya Kadhi hushughulikia hasa masuala ya mirathi na ndoa kulingana na misingi ya dini ya Kiislamu.
"Kimsingi serikali haijakataa mahakama ya kadhi, lakini inahitaji msaada wa masheikh na tumekubaliana na Waziri Pinda akafute usemi wa kwamba serikali haitaunda tena mahakama hii na yeye amekubali," alisema Mufti Simba.
"Kitakachoendelea ni kujadili mfumo gani wa mahakama unafaa kutumika.”
"Tunayo matumaini makubwa ya kuipata Mahakama ya Kadhi kwa sababu ni haki yetu na tutaendelea kuidai hadi pumzi yetu ya mwisho (mpaka kufa), mchakato unaendelea.
"Jazba hazifai na tutumie hoja au kwa msemo wa kisasa tutumie nguvu ya hoja.”
Mufti Simba pia alitoa onyo kali kwa Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni, Sheikh Muhammad Idd Muhammad kwa kuzungumza katika vyombo vya habari yale yaliyozungumzwa juzi katika kikao baina ya serikali na jopo la masheikh, kabla ya Mufti kuzungumza.
"Mzungumzaji wa suala la Mahakama ya Kadhi kwa upande wa Waislamu ni mimi tu, hakuna mzungumzaji mwingine. Hivyo namuonya Muhammad Idd kwa kitendo chake cha kutangulia kuzungumzia yaliyojiri katika kikao chetu kabla mimi kuzungumza,” alionya Mufti.
Akizungumza katika kipindi chake cha Arrisala kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Channel Ten juzi usiku, Sheikh Idd alieleza kwa ufupi yale yaliyozungumzwa katika kikao cha masheikh na Waziri Pinda.
Sheikh Idd alikiri kosa na kumuomba radhi Mufti Simba, masheikh wenzake pamoja na Waislamu, lakini aliongeza kuwa hakufanya hivyo kwa nia mbaya.
"Nakiri kosa; lakini pia namuomba radhi Mufti, masheikh na Waislamu licha ya kwamba sikufanya vile kwa nia mbaya. Hata Mufti atajua baadaye kuwa sikufanya kwa nia mbaya,” alisema Sheikh Idd.
Baada ya kumaliza kutoa tamko lake, Mufti Simba alikataa maswali akisema suala hilo la Mahakama ya Kadhi linahitaji umakini wa hali ya juu katika kulizungumza.
"Leo sitaki maswali... sitaki kubabaishwa katika majibu. Nakataa maswali ili haya yakaandikwe kama vile nilivyosema bila ya kupotoshwa,” alisema Mufti.
Kabla ya Mufti kuzungumza na waandishi, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliwatahadharisha waandishi kuacha kuandika na kunukuu kauli za watu wengine, badala yake wachukue yale ya Mufti Simba tu kwa sababu yeye ndiye msemaji mkuu katika tukio hilo.
"Waandishi waondoke na kauli ya Mufti tu yeye ndiye msemaji mkuu wa Waislamu Tanzania kupitia chombo chao cha Bakwata. Hakuna msemaji mwingine,” alisema Sheikh Salum.
Hoja ya Mahakama ya Kadhi imekuwa ikidaiwa na Waislamu kwa takriban miaka 20 sasa huku serikali ikitoa ahadi ya kulipatia ufumbuzi, lakini awamu zote za serikali zimekuwa zikipiga danadana.
Wakati huohuo, katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema maandamano ya amani waliyopanga kuyafanya Ijumaa wiki hii, yatafanyika kama yalivyopangwa.
Sheikh Ponda alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na Mwananchi na kwamba maandamano hayo yataanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhitimishwa katika viwanja vya Biafra vilivyo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Hakuna kitakachotubadili msimamo wetu. Sisi tunafanya maandamano hayo ya amani kuonyesha hisia zetu na kitu gani ambacho Waislamu tunahitaji,” alisema.
Alisema pamoja na kuwapo na kauli mbalimbali za kuwataka Waislamu wawe na subira, hawatakubali kwa kuwa kauli hizo sio mpya na kwamba wameshazizoea.
“Kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara na viongozi," alisema.
Alieleza kwamba maandamano hayo yataanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kupitia barabara za Bibi Titi, Morogoro na Kawawa,” alisema.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya Kutetea Mali za Waislamu, Sheikh Khalifa Khamis alisema maandamano hayatakuwa na maana kwa sababu suala hilo limeshazungumzwa na masheikh na serikali.
“Mimi nipo pamoja na Mufti kwa kuwataka Waislamu wawe na subira kwa kuwa hivi sasa anayesubiriwa ni Mufti kuipeleka timu yake kwa waziri wa sheria,” alisema.
“Nina uhakika mahakama hii itapatikana mapema kwa kuwa mazungumzo tumeshamaliza na kinachofuata ni utekelezaji tu,” alisema Sheikh Khamis.
Sheikh Khalifa aliwataka Waislamu kuendelea kuwa na subira kwa kuwa uanzaji wa mahakama hiyo unaweza kuwa kwa awamu na kutoa mfano kwamba inaweza ikaanza Dar es Salaam ama wilaya ya Ilala na mikoa mingine ikafuata.
Alipotafutwa na Mwananchi, Waziri Chikawe alikataa kuzungumza kwa njia ya simu akidai hana uhakika kama anayezungumza naye ni mwandishi kweli wa gazeti hili.
“Nitajuaje kama wewe ni mwandishi, nitajuaje,” alihoji Waziri Chikawe na kuongeza: “Come to my office (njoo ofisini kwangu),” alijibu na kukata simu.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, ambaye imedaiwa kuwa alikuwemo kwenye kikao hicho, alisema: “Muulize aliyewaita masheikh hao mimi sijawaita.”
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment