MBUNGE wa Kigoma Kusini, Manju Msambya (CCM), ameitaka Serikali kutoa msimamo kuhusu waraka uliotolewa na Kanisa la Kikristo likiwaelekeza Wakristo jinsi ya kuchagua viongozi. Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akichangia hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa bungeni na Waziri Mathias Chikawe.Alisema waraka huo unaonesha kuwa wananchi wametakiwa kumchagua kiongozi Mkristo na kuhoji kama kila dini ikifanya hivyo nchi itakwenda wapi? “Mheshimiwa Spika hivi hata sisi Sheikh akituita msikiti wa Mnyamani kutufundisha jinsi ya kuchagua itakuwaje?” alihoji Msambya.Kwa mujibu wa mbunge huyo, pia kuna waziri ambaye hakumtaja jina, aliyesema anaunga mkono waraka huo kwa kuwa haoni tatizo lolote. Mbunge huyo pia alisema kuna kiongozi ambaye si wa madhehebu hayo, ambaye alipinga waraka huo na kuelezea kushangaa kwake, kwa kuwa katika madhehebu ya Kikristo, ni kanisa moja tu lililochukua uamuzi huo bila kulitaja. Pia Mbunge huyo alisema Serikali inawapaka Waislamu mafuta kwa mgongo wa chupa katika suala la kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa kuogopa makanisa. “Tatizo liko wapi kuunda Mahakama ya Kadhi inayojitegemea, mbona kuna Mahakama ya Ardhi, Mahakama ya Biashara na Mahakama ya Kazi zinazojitegemea ndani ya mfumo wa mahakama?,” alihoji Msambya. “Kwa nini Mahakama ya Kadhi ionekane kikwazo, au ndio lile alilosema Waziri Chikawe katika vyombo vya habari kuwa mpaka upande wa pili ukubali ambao ni makanisa?,” alizidi kuhoji mbunge huyo na kusisitiza kuwa hoja hiyo si yake kama Msambya bali ni ya Waislamu wote. Mbunge huyo pia aliitaka Serikali itoe tamko kuhusu mchakato wa Tanzania kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) na kuongeza kuwa hata Msumbiji ambayo ina Waislamu na Wakristo, imejiunga na kusisitiza kuwa hataunga mkono hoja hiyo mpaka atakapopata majibu ya hoja zake.
Source: Habari leo
No comments:
Post a Comment